Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Mwanza, Tanzania 1971-2021. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Mwanza, Tanzania 1971-2021. 

Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa Bugando

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Bugando iwe ni fursa kwa: Uongozi, wafanyakazi na wadau wote wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, BMC., kupyaisha nia ya dhati ya kuzuia magonjwa, kuondoa maumivu na kuponya magonjwa katika mwanga wa Injili mintarafu Miongozo ya Mafundisho ya Kanisa! Utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huduma kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka ni utekelezaji wa Injili ya upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Ni sehemu ya mchakato wa kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama alivyofanya Msamaria mwema. Kumbe, ni wajibu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaoteseka. Waamini wamwone Kristo Yesu anayeendelea kuteseka kati pamoja na wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawe ni mashuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, daima wakiwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kama ilivyo kwa Kristo Yesu anayeendelea kujisadaka kila siku katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kristo Yesu, kwa njia ya mateso na kifo chake Msalabani, ametoa maana mpya ya mateso na mahangaiko ya binadamu, mwaliko kwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka, kujiaminisha kwa Kristo Yesu, ili kweli mateso na mahangaiko yao, yaweze kuwa ni chachu ya kulitakatifuza Kanisa kwa kutambua kwamba, maisha yana thamani kubwa sana mbele ya Mungu.

Jambo la msingi ni kujizatiti katika kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za wagonjwa ambao wanapaswa kutambua kwamba, wao ni amana na utajiri wa Kanisa. Wagonjwa wavumilie mateso yao kwa amani na utulivu wa ndani kama chachu ya uinjilishaji. Waamini wanaalikwa kushiriki mateso na mahangaiko ya wagonjwa kwa njia ya imani, matumaini na mapendo yanayotakatifuza na kuwaokoa watu. Kwa njia ya ushiriki huu mkamilifu, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataweza kujenga na kuimarisha mafungamano ya umoja na udugu wa kibinadamu. Wagonjwa, maskini na wale wanaoteseka, wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya huduma na maendeleo fungamani ya binadamu. Huduma kwa wagonjwa inafumbatwa katika sadaka na majitoleo pasi na kujibakiza hata kidogo kwa kutambua kwamba, nguvu ya kweli katika maisha ya mwanadamu ni huduma inayotambua: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni huduma inayotolewa kama mashuhuda wa furaha ya Injili! Kanisa linawataka waamini katika huduma kwa wagonjwa na maskini, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, upendo na mshikamano, ili kuwafunulia watu, upendo na huruma ya Mungu.

Waamini wawe na ujasiri wa kukabiliana na mateso pamoja na mahangaiko yao kwa imani na matumaini thabiti, pasi na kukata wala kukatishwa tamaa, daima wamwone Kristo Yesu Msalabani mbele ya macho yao! Kanisa linapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa na maskini! Kanisa liwe ni jicho kwa vipofu, miguu kwa viwete na nuru kwa wale wanaotembea katika giza la dhambi na mauti! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa matashi mema kwenda kwa Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, anawapongeza watu wa Mungu nchini Tanzania kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, BMC. Baba Mtakatifu anaungana na watanzania wote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa matunda maridhawa yanayotokana na huduma mbalimbali za afya na elimu na kwa namna ya pekee katika miezi ya hivi karibuni katika mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo kwa sasa ni janga la afya duniani na watu wameathirika kwa viwango tofauti.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakaza kusema, maadhimisho ya Jubilei hii iwe ni fursa kwa: Uongozi, wafanyakazi na wadau wote wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, BMC., kupyaisha nia ya dhati ya kuzuia magonjwa, kuondoa maumivu na kuponya magonjwa katika mwanga wa Injili mintarafu Miongozo ya Mafundisho ya Kanisa. Kwa jinsi hiyo, anasema Baba Mtakatifu Francisko, Taasisi hii itaendelea kuwa ishara na kielelezo halisi cha Kanisa linalosafiri, ambalo katika kuishi utume wake, kwa ujasiri linatangaza upendo wa Kristo unaoganga na kuwaponya wale wanaoteseka. Baba Mtakatifu amewahakikishia wote waliohudhuria Jubilei hii sala na aliwapatia neema na baraka zake za kitume! Kwa upande wake, Askofu mkuu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika hotuba yake ya utangulizi mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amegusia kuhusu changamoto za maadui watatu wa Tanzania wakati wa uhuru kunako mwaka 1961 kuwa ni: Ujinga, Umaskini na Maradhi, changamoto iliyotolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kanisa Katoliki likaivalia njuga changamoto hii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na ujenzi ukaanza kunako mwaka 1967 na kukamilika mwaka 1971. Mwaka 1972 Hospitali ilitaifishwa na Serikali. Mwaka 1985 ikarejeshwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kwa makubaliano maalum. Bugando imekwisha kuhudumiwa na wakurugenzi 10. Kanisa katika huduma ya afya, elimu, ustawi wa jamii linapania hasa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa Katoliki Tanzania linaipongeza Serikali kwa ushirikiano katika medani mbalimbali kwa ajili ya huduma kwa watanzania wote! Kwa upande wake, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, BMC., amesema, Hospitali inahitaji kuboresha miundombinu ya huduma kutokana na idadi ya wagonjwa kuongezeka. Kwa sasa kuna ujenzi wa Taasisi ya Moyo, utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 10.5 sanjari na ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto litakalogharimu shilingi bilioni 6.5. Ameiomba Serikali kufikiria upya namna ya kupunguza kodi kwa Taasisi zinazotoa huduma, ili fedha hii itumike katika maboresho ya huduma. Amekiri kwamba, kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya Kanisa na Serikali katika kutoa huduma za kibingwa na bobezi kwa watu wa Mungu Kanda ya Ziwa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, wananchi wanakuwa na afya bora, ili waendelee kushiriki katika ujenzi wa Tanzania.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, BMC. Ilizinduliwa rasmi tarehe 3 Novemba 1971 na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tarehe 18 Novemba 2021 imeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho haya. Hospitali hii inawahudumia watu milioni 18 wanaoishi kwenye Ukanda wa Ziwa Victoria ndiyo maana kiasi cha shilingi bilioni 4.2 za IMF zimeelekezwa Bugando ili kunogesha huduma na maendeleo Hospitalini hapo. Bugando kwa sasa ina idadi ya vitanda 950 na Serikali ya Tanzania itaendelea kulipa mishahara ya watumishi 1200 walioajiriwa na Serikali wanaolipwa kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa mwaka. Serikali pia inatoa ruzuku ya dawa na inaendelea kusogeza huduma za kibingwa na huduma bobezi karibu zaidi na wananchi wa Kanda ya Ziwa Victoria. Rais Samia ametoa wito kwa wataalam wa afya kupunguza kasi ya maradhi yasiyoambukiza hasa Saratani na waathirika wakubwa ni wanawake. Serikali itagharimia ujenzi wa vyumba vya kuhifadhia mashine sita za kutolea tiba ya mionzi kwa gharama ya shilingi bilioni 5.5. Ujenzi wa wodi ya wagonjwa wa Saratani unatarajiwa kukamilika kwa wakati.

Wakati huo huo Dk Fabian Anaclet Massaga, Mkurugenzi Mkuu wa BMC, anasema ni matumaini ya Taasisi yake kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Bugando itakuwa na hadhi ya Kimataifa kwa kuwahudumia watanzania na watu kutoka katika nchi za jirani.  Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Miaka 50 ya Bugando, madaktari bingwa walipita katika hospitali za mikoa ya Kanda ya Ziwa na kutoa huduma za matibabu bure ambapo zaidi ya 35,000 walipatiwa huduma mbalimbali huku wananchi 83 walipatiwa huduma za upasuaji. Dk Fabian Anaclet Massaga, amesema Hospitali ya Bugando ina vitanda 950 na wafanyakazi 1,800 kati ya wafanyakazi 2554 wanaohitajika huku wafanyakazi 1,191 waliopo wanalipwa mshahara na Serikali na waliobaki wanalipwa mshahara na taasisi. “Hospitali hii inahudumia zaidi ya wananchi milioni 18 katika mikoa nane ya Kanda ya Ziwa lakini pia tunahudumia wananchi kutoka nchi za jirani kama vile Uganda, Kenya, Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC,”amesema. Ameishukuru Serikali kuendelea kufanikisha huduma za saratani ambapo awamu ya kwanza ilitoa Sh5.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya matibabu ya saratani na ofisi huku awamu ya pili ikitoa Shilingi bilioni moja katika ujenzi wa wodi unaoendelea.

Papa Bugando
23 November 2021, 15:39