Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuendelea kujiandaa kiroho kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2021 huko Lisbon, Ureno. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuendelea kujiandaa kiroho kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2021 huko Lisbon, Ureno. 

Maadhimisho Ya Siku Ya Vijana Ulimwenguni, Lisbon Ureno 2023

Kumekucha! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Mt. Yosefu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Kuhusu Mtakatifu Yosefu katika Historia ya Wokovu, Jumatano tarehe 24 Novemba 2021, amewakumbusha waamini kwamba, Jumapili ya 34 ya Mwaka wa Kanisa sanjari na Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu, kwa mara ya kwanza Mama Kanisa pia ameadhimisha Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2021. Hii ni sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu. Awe ni mfano bora wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu katika maisha! Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika huduma ya upendo!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 umenogeshwa na kauli mbiu “Inuka. Nimekuteua uwe Shahidi wa mambo haya uliyoyaona.” Mdo 26: 16. Siku hii kwa ngazi ya kijimbo imeadhimishwa tarehe 21 Novemba 2021, Sherehe ya Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia changamoto ambazo zimejitokeza kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na umuhimu wa kuinuka na kuendelea na safari ya maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2021 yanaongozwa na ushuhuda wa Mtakatifu Paulo Mtume mbele ya Mfalme Agripa, baada ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka na kujitambulisha kwake akisema kuwa ni Yesu Mnazareti, kweli mang’amuzi haya yana umiza. Baba Mtakatifu anawataka vijana kutambua upofu wa maisha yao, kuwa tayari kutubu na kumwongokea Mungu, na hatimaye kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ni muda muafaka kwa vijana kuinuka na kuanza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Huu ni wakati wa kuinuka na kuanza kusherehekea Siku ya Vijana Ngazi ya Kijimbo!

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kufanya hija ya pamoja, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Ujumbe wa Mwaka 2020 ulinogeshwa na kauli mbiu “Kijana, nakuambia: Inuka.” Rej. Lk. 7:14. Ujumbe huu ulikuwa ni sehemu ya maandalizi mahususi ya kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo hasa kutokana na maabukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kumekuwepo na athari kubwa kutokana na maambukizi haya katika sekta ya elimu, kazi na makusanyiko ya kijamii. Kuna baadhi ya vijana walishindwa kupata msaada wakati wa kipindi hiki kigumu. Matatizo mengi yaliibuliwa ndani ya familia, ukosefu wa fursa za ajira, sonona, upweke, na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kinzani na milipuko ya hasira na ongezeko la vurugu! Licha ya gonjwa hili kusababisha madhara makubwa kwa watu, lakini pia limesaidia vijana kukuza na kudumisha mshikamano wa kidugu katika jitihada za kuokoa maisha; kwa kupandikiza mbegu ya matumaini, uhuru, haki, amani pamoja na kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa kawaida pale ambapo kijana anaanguka, utu wake pia unaanguka; anapoinuka, anauinua pia utu wa watu wengine ulimwenguni kote. Hii ni nguvu maridhawa ambayo iko mikononi mwa vijana. Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anapenda kuwaambia vijana “Inuka” ujumbe mahususi ambao utawasaidia vijana kujiandaa kwa nyakati na kuwa tayari kuandika kurasa mpya katika historia ya mwanadamu, jambo ambalo linahitaji: nguvu, hamasa na ari kubwa, ili kuinuka, tayari kuwa shuhuda wa mambo hayo aliyoyaona. Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa aliweza kutangaza na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake mbele ya Mfalme Agripa baada ya kufungwa gerezani. Mtume Paulo ambaye alilitesa na kulidhulumu Kanisa anashuhudia kuhusu nuru angavu kutoka mbinguni na sauti ya Kristo Yesu aliyemwita kwa jina lake. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuzama zaidi katika tukio hili la kuitwa kwa Saulo mara mbili kama alivyofanya Musa na Samuel. Paulo Mtume alishuhudia ufunuo na nguvu ya Mungu, kuonesha kwamba, Kristo Yesu alimfahamu vizuri sana kama mtu aliyekuwa na chuki dhidi ya Wakristo kutokana na ujinga wake. Kristo Yesu alitaka kumwonjesha, huruma na upendo wake wa daima. Hii ni neema, kielelezo cha upendo usiokuwa na kifani na mwanga mpya utakaomletea wongofu.

Paulo aliuliza wewe u nani Bwana? Hili ni swali ambalo vijana wanapaswa kujiuliza kila siku ya maisha yao, kama njia ya kuzungumza na Kristo Yesu kutokana katika undani wa maisha ya mtu, kielelezo cha sala makini inayomwezesha mwamini kuzungumza moja kwa mnoja na Kristo Yesu jinsi alivyo! Hili ndilo swali linalopaswa kuulizwa na vijana; We u nani Bwana? Hii ni njia ya kutaka kufahamiana na Kristo Yesu. Jibu ni kwamba, ni Yesu ambaye anamuudhi. Paulo Mtume alikuwa hajapata nafasi ya kukutana mubashara na Kristo Yesu, bali alibahatika kuonana na Wakristo aliowadhulumu na kwa hakika, alikuwa amekutana na Kristo Yesu kati ya watu aliowadhulumu. Kumfahamu Kristo Yesu na Kanisa lake ni kama chanda na pete. Wakristo wanaweza kupata mang’amuzi haya, ikiwa kama wamejenga umoja wa Kikanisa. Kristo Yesu anataka vijana nao kutubu na kumwongokea, tayari kusikiliza na kujibu wito na mwaliko wake! Kristo Yesu aliamua kumwita Mtume Paulo aliyelitesa Kanisa na kwamba, machoni pa Mwenyezi Mungu hakuna mtu anayeweza kupotea! Jambo la msingi ni vijana kujibidiisha kukutana na Kristo Yesu, ili kuonja  neema na msamaha wake, na hatimaye, waweze kumpenda kwa moyo na akili zao zote, tayari kukumbatia na kuambata mtindo mpya wa maisha na kupokea utume kama ilivyokuwa kwa Sauli.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutambua upofu wa maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Sauli aliyedhani kwamba, ni kitambulisho na kilele cha maadili na elimu, kiasi cha kushindwa kutambua upofu wake wa kimwili na kiroho; anatambua kosa la mauaji na dhuluma dhidi ya Wakristo na kwamba, yeye hakuwa ni kielelezo cha ukweli wote; mambo yote haya yalimfanya kujisikia mnyonge na mdogo kuliko hata “ kidonge cha pilton.” Unyenyekevu ili kutambua udhaifu na mapungufu ya binadamu ni muhimu sana. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mang’amuzi ya Dameski yalikuwa na nguvu kiasi kwamba, Saul akaamua kubadili jina na kuanza kuitwa Paulo, maana yake “Mdogo” kama anavyosimulia mwenyewe akisema, “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu.” I Kor 15:9. Watakatifu wengi walipenda kusema na kushuhudia ukweli wa mambo, leo hii mambo yamebadilika sana, watu wengi hawataki kutangaza na kushuhudia ukweli, ili wapendwe kama walivyo! Toba na wongofu wa Mtakatifu Paulo ulimwezesha kuendelea na safari kuelekea Dameski, huku akiwa ni mtu mpya kabisa. Wongofu wa ndani ni hija ya maisha ya kila siku, jambo la msingi ni kumtii Kristo Yesu, na kumwachia nafasi ili aweze kufanya mabadiliko katika nia na malengo yao, ili waweze kuwa ni mitume, mashuhuda na watangazaji wa Injili. Ni fursa ya kuimarisha fadhila ya ukimya na sala kama Paulo alivyokirimiwa na Kristo Yesu. Hii ni changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanamfuasa Kristo, ili kupata mwanga halisi wa maisha.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, vijana ndio waathirika wa kwanza pamoja na wale wanaowazunguka, kwa kukumbatia itikadi zinazobomoa utu na heshima ya binadamu. Kwa kuwa na misimamo mikali ya kidini na kiimani inayopelekea vurugu na uvunjifu wa amani. Kwa baadhi ya vijana, mitandao ya kijamii imekuwa ni silaha za mapambano dhidi ya wengine, kiasi hata cha kuthubutu kutumia habari za kughushi kama silaha ya kuwachafulia wengine sifa njema na hatimaye, kusambaza sumu. Baba Mtakatifu anawaomba vijana wamwachie Kristo Yesu nafasi ili kuwasaidia kuibua na kukuza karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kwa toba na wongofu wa ndani, Mtakatifu Paulo, akabahatika kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa ya watu aliowanyanyasa na kuwadhulumu. Hata leo hii, Kristo Yesu anawaamini sana vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo. Wakristo wanaitwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, ili kutangaza na kushuhudia hayo walioyaona, kwa kuzingatia uzoefu na mang’amuzi yao ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana “Kuinuka” na kuwa mashuhuda wa maisha yao ya Kikristo! Wawe ni nuru kwa jirani zao, kwa kudumisha ushirika ndani ya Kanisa ili kuvunjilia mbali upweke hasi. Vijana wanapaswa kuinuka ili kujenga mahusiano na mafungamano katika familia; kwa kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika medani mbalimbali za maisha. Huu ni wakati kwa vijana kuinuka na kuanza kujikita katika haki jamii, ukweli, utu wema na haki msingi za binadamu. Vijana wasimame kidete kutetea maskini na wanyonge; wawe ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti katika jamii, yaani wakimbizi na wahamiaji. Vijana wainuke na kuanza kuangalia mazingira nyumba ya wote kwa macho angavu, kwa kuonesha ujasiri wa kulinda ikolojia fungamani. Vijana wawe na ujasiri wa kuinuka kwa kutambua kwamba, hata katika udhaifu wao, wanaweza kuanza upya; kwa wale waliokuwa wamekufa kiroho, wanaweza kufufuka tena; wale waliokuwa wameelemewa katika vifungo mbalimbali, wanaweza sasa kuwa huru; wenye huzuni, wanaweza kugundua tena matumaini. Huu ni wakati wa vijana kuinuka na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ni mzima, kwa kueneza ujumbe wa upendo na wokovu kati ya vijana wenzao, maeneo ya shule, kazi na hata katika ulimwengu wa kidigitali. Watambue kwamba, Baba Mtakatifu na Kanisa katika ujumla wake linawathamini sana vijana wa kizazi kipya na kwamba, linawatuma kuwa ni mashuhuda wa Habari Njema kwa wale wote watakaokutana nao kwenye barabara ya Dameski.

Vijana wasisahau kwamba: “kwa kweli, kila mmoja ambaye ameuonja kiukweli upendo wa Mungu unaookoa haitaji muda mrefu wala mafunzo marefu ili aweze kwenda nje kutangaza na kushuhudia huo upendo. Kila Mkristo ni mmisionari kwa kiwango ambacho amekwisha kutana na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu.” Evangelii gaudium, 120. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuinuka na kuanza kuadhimisha Siku ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo! Hii ni hija ya maisha ya kiroho, itakayowasindikiza hadi mwaka 2023 katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Siku hii kwa ngazi ya kijimbo imeadhimishwa tarehe 21 Novemba 2021, Sherehe ya Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu. Hatimaye, mwishoni mwa Ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anaonesha matumaini kwamba, hatua zote hizi zitawawezesha waamini kuwa ni mahujaji wa kweli, daima wakiendelea kujiweka wazi kwa mshangao wa Mungu katika mapito ya maisha yao. Wawe tayari kusikiliza na kujibu sauti ya Mungu kwa njia ya sauti ya ndugu zao. Kwa njia hii wataweza kusaidiana kuinuka katika nyakati za taabu na mahangaiko makubwa katika historia; watakuwa ni mashuhuda wa matumaini mapya kwa ajili ya siku za usoni!

Lisbon 2023
24 November 2021, 15:22