Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiandaa kikamilifu kuadhimisha Kipindi cha Majilio, ili hatimaye, waweze kufurahia Sherehe ya Fumbo la Umwilisho katika maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiandaa kikamilifu kuadhimisha Kipindi cha Majilio, ili hatimaye, waweze kufurahia Sherehe ya Fumbo la Umwilisho katika maisha yao! 

Kipindi cha Majilio 28 Novemba Hadi 24 Desemba 2021: Kesheni!

Papa Frabncisko: Kipindi cha Majilio ni hija ya maisha ya imani, matumaini na mapendo; inayowakumbusha waamini, Fumbo la Umwilisho na Siku ya ile ya mwisho, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, kama waamini wanavyosali katika Kanuni ya Imani. Kipindi cha Majilio kinawaandaa waamini kuweza kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa tena katika nyoyo zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, tarehe 28 Novemba 2021 inaufungua rasmi Mwaka Mpya wa Kanisa na kwamba, Kipindi cha Majilio kitapata hitimisho lake tarehe 24 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wanajiandaa kuadhimisha kwa namna mbalimbali Kipindi cha Majilio na hatimaye, kusherehekea Fumbo la Umwilisho, huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kukesha. Majilio ni hija ya maisha ya imani, matumaini na mapendo; inayowakumbusha waamini, Fumbo la Umwilisho na Siku ya ile ya mwisho, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, kama waamini wanavyosali katika Kanuni ya Imani. Kipindi cha Majilio kinawaandaa pia waamini kuweza kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa tena katika nyoyo zao! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwa kweli ni watoto wa Mwanga, ili waweze kuupokea mwanga na kutembea katika mwanga wa utakatifu wa maisha, mwaliko wa kwanza kwa kila Mkristo, kwani wanapomwona Mtoto Yesu akiwa amelazwa kwenye Pango la kulishia wanyama, hapo wanaweza kuonja ukuu na utukufu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Mwanga unaoletwa na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili unawaamsha waamini kutoka katika usingizi, ili kuwasaidia kutembelea katika ulimwengu huu kwa moyo wa unyenyekevu, huku wakiendelea kukua na kuongezeka katika kimo na busara kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu. Majilio na hatimaye Sherehe ya Noeli ni kipindi cha matumaini na mwanzo wa maisha mapya yanayojikita katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huu ni mwendelezo wa mchakato wa majiundo endelevu, fungamani na angavu katika azma ya uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo. Katika kipindi cha Majilio, Mama Kanisa anapenda kumwonesha kwa namna ya pekee Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu, aliyejitaabisha kuhakikisha kwamba, Familia Takatifu ya Nazareti inapata mahitaji yake msingi, huku akijiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumwongoza kadiri ya mpango na haki yake ya Kimungu, tofauti kabisa na haki ambayo wakati mwingine binadamu anapenda kumsingizia Mungu, changamoto kwa Wakristo kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.

Kristo Yesu alizaliwa mjini Bethelehemu, maana yake “Nyumba ya Mkate”, pembezoni mwa Utawala wa Kirumi, ndivyo Mwenyezi Mungu katika Fumbo la Umwilisho, amependa kujinyenyekesha na kuzaliwa kama binadamu, lakini zaidi katika Pango la kulishia wanyama. Noeli ni Sherehe inayoonesha: Utakatifu, ukuu na utukufu wa Mungu katika mambo ya kawaida. Hapa mwamini anajifunza kwamba, Mwenyezi Mungu anatekeleza mpango wa ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Kipindi Majilio
24 November 2021, 16:09