Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Oktoba 2021 amekutana na kuzungumza na mahujaji wa kiekumene kutoka Ujerumani. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Oktoba 2021 amekutana na kuzungumza na mahujaji wa kiekumene kutoka Ujerumani.  

Papa: Majadiliano ya Kiekumene Yajenge Utamaduni wa Kusikilizana

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Dhamiri nyofu ni mahali patakatifu palipowekwa na Mungu ndani mwao. Wajitahidi kumfungulia Mwenyezi Mungu maskio na nyoyo zao. Anayeimba kwa moyo ulio wazi, hata bila ya kujitambua, anagusa fumbo la maisha ya Mungu ambalo kimsingi ni upendo uliofunuliwa na Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 25 Oktoba 2021 amekutana na kuzungumza na mahujaji wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri kutoka Ujerumani, waliongozwa na kauli mbiu “Ni Bora Wote Tukiwa Pamoja.”. Hija kama hii, iliwahi kufanywa na mahujaji wengine, miaka mitano iliyopita huku wakiongozwa na kauli mbiu “Wakiwa wa Luter Kwenda Kwa Papa”.

Hija ya mwaka 2021 imepambwa na nyuso mpya zaidi. Amewashukuru mahujaji wote kwa kuendelea kujenga ari na mwamko wa kiekumene! Amewashukuru kwa kumpokea na wimbo wa pamoja kama Jumuiya, kwani kwaya inaunganisha watu. Katika kwaya hakuna mtu ambaye yuko pweke, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni wa kusikilizana. Huu pia ndio unaopaswa kuwa ni mtindo wa maisha na mwelekeo wa Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema njia ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, Kanisa limerejea tena “darasani” ili kujifunza sanaa ya kusikilizana.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Dhamiri nyofu ni mahali patakatifu palipowekwa na Mungu ndani mwao. Wajitahidi kumfungulia Mwenyezi Mungu maskio na nyoyo zao. Anayeimba kwa moyo ulio wazi, hata bila ya kujitambua, anagusa fumbo la Mungu. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Fumbo la Maisha ya Mungu ni upendo ambao unapata utimilifu wake kwa njia ya Kristo Yesu, iwe ni kwa kiwango cha mtu mmoja mmoja au wote! Baba Mtakatifu, amekazia umuhimu wa kusikiliza wimbo wa Mungu katika maisha yao. Ili kutokana na mwingiliano wa sauti nyingi, wanaweza kutengeneza wimbo mmoja. Hivi ndivyo inavyojitokeza hata pia katika mchakato wa kiekumene, nchini Ujeruman na sehemu mbalimbali za dunia. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume pamoja na familia zao!

Majadiliano ya Kiekumene

 

25 October 2021, 15:48