Tarehe 4 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Upendo ili kumuenzi Mama Theresa wa Calcutta aliyejisadaka kwa ajili ya kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu! Tarehe 4 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Upendo ili kumuenzi Mama Theresa wa Calcutta aliyejisadaka kwa ajili ya kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu! 

Siku ya Kimataifa Ya Upendo: Mama Theresa wa Calcutta 5 Sept.

UN tarehe 17 Desemba 2012 ikatangaza kwamba, tarehe 5 Septemba ya kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Upendo ili kumuenzi Mama Theresa wa Calcutta aliyetangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni Mama aliyeonesha huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Septemba 2016 alimtangaza Mama Theresa wa Calcutta kuwa Mtakatifu, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Huruma ya Mungu kwa wafanyakazi wa huruma na wale wa kujitolea. Katika mahubiri yake, alikazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu. Waamini wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huruma iwe ni kielelezo cha sala na imani tendaji inayomwilishwa katika huduma na unyenyekevu. Waamini wanapaswa kuwa na ujasiri na kuthubutu kumwona na kumtambua Kristo Yesu kati ya watu wadogo, wanyonge na maskini. Wote hawa waoneshwe Injili ya matumaini, huruma na upendo. Mama Theresa wa Calcutta alisimama kidete kutangaza na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Aliinama na kuwaganga maskini kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Akasimama kidete kulinda: utu, heshima na haki zao msingi. Alikuwa ni sauti ya maskini na wanyonge duniani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Mungu kati ya maskini. Mama Theresa wa Calcutta awe ni kielelezo cha upendo aminifu wa Mungu usiokuwa na ndoana. 

Mtakatifu Mama Theresa wa Calcuta, lakini jina lake hasa ni “Anjezë Gonxhe Bojaxhiu” alizaliwa tarehe 26 Agosti 1910 huko Skopje, Macedonia ya Kaskazini. Tarehe 5 Septemba 1997 akafariki dunia na kutangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 4 Septemba 2016 na Baba Mtakatifu Francisko. Umoja wa Mataifa tarehe 17 Desemba 2012 ukatangaza kwamba, tarehe 5 Septemba ya kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Upendo ili kumuenzi Mama Theresa wa Calcutta aliyejisadaka bila ya kujibakiza ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni Mama aliyeonesha huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Umaskini wa hali na kipato ni tishio kwa amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani.

Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Upendo katika matendo ni chemchemi ya faraja katika huduma ya afya, elimu, makazi na ulinzi kwa watoto. Upendo unachochea na kunogesha utamaduni, sayansi, michezo pamoja na ulinzi tamaduni na mapokeo asilia. Upendo ni kilolezo cha haki msingi za binadamu. Mshikamano wa udugu wa kivinadamu ni muhimu sana katika kupambana na umaskini duniani.

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis ambaye pia ni anasema, Mama Theresa wa Calcutta ni Msimamizi wa Caritas Internationalis. Kunako mwaka 1950 alianzisha Shirika la Wamisionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta ambao wanajulikana kama mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini. Mama Theresa wa Calcutta awe ni mfano bora wa kuigwa katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kwa kusambana “Virusi vya upendo na mshikamano” ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Janga la UVIKO-19 liaamshe ndani ya watu wa Mungu fadhila ya huruma, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu!

Itakumbukwa kwamba, Mama Theresa wa Calcutta ni kielelezo na shuhuda wa huruma ya upendo wa Mungu unaomwilishwa kwa wagonjwa, maskini na wote wanaosukumwa pembezoni mwa jamii kwani upendo kwa jirani ndicho kipimo ambacho Yesu atakitumia siku ya mwisho kuwahukumu wazima na wafu! Maskini ni kundi lisilopendwa na wengi, kumbe, hili ndilo kundi ambalo Mama Theresa wa Calcutta anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo wao kwao. Huu ni muhtasari wa kitabu ambacho kimeandikwa kwa heshima ya Mama Theresa wa Calcutta “Tuwapende wasiopendeka” na Baba Mtakatifu Francisko kukiandikia dibaji yake! “Amiamo chi non è amato. Testi inediti di Madre Teresa di Calcutta (Editrice Missionaria Italiana) Mama Theresa wa Calcutta anasema Ukoma na Kifua kikuu ni magonjwa ambayo hayawezi kufua dafu kwa upweke hasi unaoweza kumfanya mwanadamu kuchungulia na hata wakati mwingine kuonja kaburi! Upweke ni chanzo cha mipasuko ya kijamii, ukosefu wa amani, vita na majanga yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu hiki anakazia mambo mafuatayo: Sala, upendo, huruma, familia na vijana. Anakumbusha kwamba, Kanisa katika maisha na utume wake linaendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu na kwamba, kuna maskini wanaohitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mama Theresa wa Calcutta anawahamasisha waamini kujichotea nguvu ya huruma na upendo wa Mungu kutoka katika kisima cha: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuweza kumwilisha sala katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Sala iwawezeshe waamini kukutana na kuzungumzana na Kristo Yesu; kuomba rehema na neema ili kuwa kweli ni watu wanaoweza kuthubutu kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao; kwa kuwaangalia wote kwa jicho la upendo linalopyaisha maisha ya watu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, upendo ni fadhila inayomwezesha mwamini kuwa kweli ni Msamaria mwema kwa jirani yake anayeogelea katika shida na magumu ya maisha: kiroho na kimwili.

Upendo uwawezeshe waamini kuwa ni mashuhuda wa huruma inayoganga na kuponya madonda na majeraha ya maisha ya mwanadamu; ni ushuhuda wa faraja ya Mungu kwa madonda ya binadamu! Yote haya yanawezekana ikiwa kama mwamini amefungamanisha maisha yake na Kristo Yesu, tayari kushuhudia uwepo na ukaribu wa Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Mama Theresa wa Calcutta aliyaandika matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha na utume wake, yakawa ni chachu ya utakatifu wa maisha, kumbe, ni jambo linalowezekana hata kwa waamini wengine kuiga mfano huu bora! Mama Theresa alionesha karama na utajiri wa kimama, akawapokea na kuwahudumia watu wote pasi na ubaguzi. Alikuwa na jicho la pekee hasa kwa vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi baada ya familia zao kusambaratika kutokana na sababu mbali mbali. Bikira Maria ni mfano wa Umama unaoguswa na mahangaiko ya wengine, tayari kuyajibu kwa njia ya huduma makini! Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya faraja ya Mungu kwa familia zao kwa njia ya sala. Familia inahitaji kusimikwa katika upendo, umoja na kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa! Kwa kutekeleza yote haya, familia zinakuwa ni zawadi kubwa inayoweza kutolewa kwa Kanisa!

Mama Theresa wa Calcutta anawataka vijana kwa namna ya pekee kujenga maisha na uwepo wao kwa kumzunguka Kristo Yesu, ufunuo wa Huruma ya Mungu; mwamba thabiti na mwaminifu katika ahadi zake hata kama mwanadamu atakengeuka na kuasi. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kukita maisha yao katika matumaini na kamwe wasithubutu kutoa nafasi kwa wajanja wachache kupoka matumaini yao, bali waendelee kushikamana na kumpenda Mungu; huku wakijenga madaraja yanayowaunganisha watu, kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Vijana wawe na ujasiri wa kupambana na changamoto za maisha, daima wakiwa na malengo ya juu pamoja na kuwashirikisha vijana wenzao fursa na mafanikio ya maisha. Vijana wa kizazi kipya warutubishe maisha yao kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Sala ili kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha.

Mama Theresa
04 September 2021, 16:27