Papa Francisko akutana na viongozi wa Mfuko kwa Ajili ya Amani "Foundation Leaders Pour la Paix ". Papa Francisko akutana na viongozi wa Mfuko kwa Ajili ya Amani "Foundation Leaders Pour la Paix ". 

Papa Francisko Achambua Mambo Yanayo hatarisha Amani Duniani!

Papa Francisko: UVIKO-19; machafuko ya kisiasa, uharibifu wa mazingira, baa la njaa na ukame wa kutisha; athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na utengenezaji, uhifadhi na matumizi ya silaha za nyuklia ni kati ya mambo yanayoendelea kutishia amani duniani. Jitihada za kutaka kulinda na kudumisha amani duniani ni muhimu sana na zinapaswa kuwa ni jambo la dharura.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Wajumbe wa Mfuko wa Viongozi Kwa Ajili ya Amani "Fondation Leaders pour la Paix", Jumamosi tarehe 4 Septemba 2021 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Huu ni mfuko ambao unalenga kutoa tahadhari kwa dharura zinazotishia amani duniani, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuchukua tahadhari kwa kubainisha sera na mikakati ya kufuata. Kila mwaka Mfuko huu unachapisha taarifa inayoonesha dharura inatotishia amani duniani na kuiwasilisha kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa! Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewashukuru wajumbe wa Mfuko wa Viongozi Kwa Ajili ya Amani "Fondation Leaders pour la Paix" kwa jitihada zao mbalimbali. Athari kubwa za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 bado zinaendelea kuonesha “makucha yake” katika sekta ya uchumi, jamii lakini zaidi kwa maisha ya maskini zaidi duniani. Watu wengi wamepoteza maisha yao kutokana na gonjwa hili. Ikumbukwe kwamba, kila maisha ya mwanadamu ni zawadi ya Mungu isiyokuwa na kifani. UVIKO-19 imepelekea watu wengi kuvunjika moyo na kukata tamaa kiasi hata cha kusababisha kinzani na mipasuko ya kijamii.

UVIKO-19 inaendelea kuchangia katika madhara ambayo tayari yamekwisha sababishwa: na machafuko ya kisiasa, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote, baa la njaa na ukame wa kutisha; athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na utengenezaji, uhifadhi na matumizi ya silaha za nyuklia ni kati ya mambo yanayoendelea kutishia amani duniani. Jitihada za kutaka kulinda na kudumisha amani duniani ni muhimu sana na zinapaswa kuwa ni jambo la dharura. Baba Mtakatifu anakaza kusema, changamoto kubwa ni kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na raia wao wa kutumia changamoto hizi kama fursa kwa viongozi kuwajibika zaidi, huku wakishirikiana kwa karibu zaidi na raia wao. Jambo la kumshukuru Mungu ni kuona kwamba, jitihada za kutafuta amani zinapata chimbuko lake kutoka katika ngazi za juu na wala si katika makundi ya watu ambayo wakati mwingine yanatumiwa zaidi kisiasa na kiitikadi. Baba Mtakatifu anasema hata katika muktadha huu, Wajumbe wa Mfuko wa Viongozi Kwa Ajili ya Amani "Fondation Leaders pour la Paix", wanaweza kutoa mchango chanya. Hii inawezekana kwa kuwasaidia wahusika wakuu kutambua shida, changamoto pamoja na vyanzo vyake. Hii sehemu muhimu sana ya mchakato wa elimu ya amani ambayo kimsingi ni kati ya vipaumbele vyao!

Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, karantini pamoja na athari zake za muda mrefu kijamii, limeathiri hata shughuli za kisiasa. Lakini, hii pia ikitumiwa vyema inaweza kuwa ni fursa ya kuboresha siasa, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamnu unaofumbatwa katika urafiki wa kijamii. Hii ni siasa inayojikita zaidi katika mchakato wa sanaa na ujenzi wa amani duniani. Ni katika muktadha huu, ujenzi wa amani unakuwa ni shirikishi, kwa kuwahusisha watu wote ambao hata pengine hapo awali walitengwa na kutokushirikishwa. Huu ni mchakato unaotekelezwa katika ngazi kuu mbili: kitamaduni na kitaasisi. Baba Mtakatifu anasema, kitamaduni, mchakato huu, unatoa kipaumbele cha kwanza kwa: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; historia; pamoja na makovu yaliyosahauliwa. Hizi ni jitihada za ujenzi wa utamaduni wa kuwakutanisha watu, ili waweze kusikilizana, kuthaminiana, ili kupata kile kilicho chema kutoka kwa jirani. Katika ngazi ya taasisi, kuna haja ya kutoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano na ushirikiano, ili mikataba iliyoridhiwa Kimataifa inajikita zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kuyalinda Mataifa changa zaidi. Majadiliano haya yote yanapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa watu kukutana na kugusa madonda ya waathirika. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwatia shime wajumbe hawa kusimama kidete kwa ajili ya kudumisha amani sanjari na ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki na udugu wa kibinadamu.

Amani Duniani

 

 

04 September 2021, 15:51