Dini mbalimbali duniani zijenge utamaduni wa kukuza na kudumisha uhuru wa kidini, waamini wenyewe wakiwa ni mfano bora wa kuigwa! Dini mbalimbali duniani zijenge utamaduni wa kukuza na kudumisha uhuru wa kidini, waamini wenyewe wakiwa ni mfano bora wa kuigwa! 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa: Majadiliano ya Kidini na Kiekumene

Papa Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu: Umoja wa wafuasi wa Kristo Yesu kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kubomoa kuta za utengano na kuanza mchakato wa ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu na kuwaimarisha kwa pamoja. Mambo mengine ni kuhusu: Agano, dhuluma pamoja na umuhimu wa kuwa na mizizi inayorutubisha kumbukumbu hai!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 baada ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria alipata nafasi ya kukutana na viongozi wawakilishi wa Baraza la Makanisa nchini Hungaria pamoja na baadhi ya viongozi wa Jumuiya za Kiyahudi nchini Hungaria. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia zaidi pamoja na mambo mengine kuhusu: Umoja wa wafuasi wa Kristo Yesu kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kubomoa kuta za utengano na kuanza mchakato wa ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu na kuwaimarisha kwa pamoja. Mambo mengine ni kuhusu: Agano, dhuluma pamoja na umuhimu wa kuwa na mizizi inayorutubisha kumbukumbu hai! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Baraza la Makanisa nchini Hungaria kwa kujenga na kudumisha uekumene wa sala na ushirikiano kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza maisha mapya yanayosimikwa katika umoja na udugu wa kibinadamu na wala si uhasama, ili kujenga umoja na mshikamano kama ilivyokuwa kwa Waisraeli kule Jangwani.

Hiki ndicho kielelezo cha wito wa Ibrahimu, Baba wa imani. Kama waamini wanapaswa kujenga madaraja yanayowaunganisha watu kwa pamoja. Waamini wajitahidi kushikamana kwa kukazia elimu ya udugu wa kibinadamu, ili kudumisha udugu na kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja. Kila mtu ni muhimu sana katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, changamoto ni kujitahidi ili kufahamiana na kuondokana na tabia ya kudhaniana vibaya, kinzani, migogoro na mipasuko mbalimbali! Agano la Kale liwaunganishe na kuwajengea umoja na mshikamano wa kidugu. Dini ziwe mstari wa mbele kukuza na kudumisha uhuru wa kidini, wao wenyewe wakiwa ni mfano bora wa kuigwa, daima wakijitahidi kuwa wazi na kujenga amani, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Agano la Amani ya kudumu katika ulimwengu ambao umegeuka na kuwa kama tambara bovu! Iwe ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu historia, matatizo yaliyojitokeza, kinzani na mipasuko sanjari na madhulumu ya kidini; ili kwa pamoja waweze kushirikishana urithi wa maisha ya kiroho, tayari kuanza kujielekeza katika ujenzi wa Hungaria mpya inayosimikwa katika amani na utulivu, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita!

Kuna watu walioteseka sana kwenye Kambi za mateso na mauaji ya kimbari, lakini bado wakawa mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Kama ilivyokuwa kwenye historia ya Bwana Miklòs Radnòt alishuhudia nguvu ya upendo na imani; dhidi ya chuki na uhasama. Hata katika mateso makali, akapata nguvu ya kushuhudia ujasiri wa kuandika mawazo na matumaini yake, akiwataka watu kupendana na kuachana na uhasama. Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa dini wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini na amani; kwa kujenga utamaduni wa kusikilizana, tayari kurejea katika asili na msingi wa dini yao. Kila mtu anatakiwa kujielekeza zaidi ili awe ni mzizi, ili hatimaye, kuzaa matunda yanayokusudiwa, ili kurutubisha kumbukumbu hai. Mwanadamu anaweza kupata mafanikio makubwa, ikiwa kama maisha yake, yamejengeka katika msingi thabiti. Hii ni changamoto kwa waamini kujikita katika utamaduni wa kumsikiliza Mungu pamoja na jirani, ili kujenga na kurutubisha upendo kati yao. Viongozi wa dini wajitahidi kuwa ni mizizi ya amani na umoja na hivyo wataweza kuaminika mbele ya macho ya walimwengu kuwa ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu.

Umoja wa Makanisa
12 September 2021, 13:30