Kardinali Charles Maung Bo: Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Uvumilivu wa Mungu kwa waja wake! Kardinali Charles Maung Bo: Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Uvumilivu wa Mungu kwa waja wake! 

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Uvumilivu wa Mungu Kwa Waja Wake

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Uvumilivu wa Mungu. Ni uvumilivu ambao umeliwezesha Kanisa kuadhimisha Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, kipindi cha neema na baraka. Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika fadhila ya uvumilivu. Licha ya matatizo na changamoto mbalimbali katika utume Kanisa, bado linaendelea kushamiri kutokana na fadhila ya uvumilivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, (Council of Bishops’ Conferences of Europe (CCEE), Jumapili tarehe 5 Septemba 2021 amezindua Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC), kwa Ibada ya Misa Takatifu, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria.  Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu Francisko anategemea kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa hapo tarehe 12 Septemba 2021. Baadaye anatarajia kutembelea nchini Slovakia hija inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa Pili kutembelea Hungaria na Slovakia. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Hungaria mwaka 1991 na mwaka 1996. Alifanya pia hija ya kitume nchini Slovakia kati ya Mwaka 1990, 1995 na Mwaka 2003.

Kardinali Charles Maung Bo., SDB, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Yangon nchini Myanmar na Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC., katika katekesi yake amesema, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Uvumilivu wa Mungu. Huu ni uvumilivu ambao umeliwezesha Kanisa kuadhimisha Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, kipindi cha neema na baraka. Hiki ni kielelezo cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba, Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika fadhila ya uvumilivu. Licha ya matatizo na changamoto mbalimbali katika maisha na utume wa Kanisa, bado Kanisa linaendelea kushamiri kutokana na fadhila ya uvumilivu. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu katika ujumla wao, kufahamu maana ya uvumilivu katika maisha yao, ili hatimaye, kuweza kuvuka kipeo cha Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Historia nzima ya Ukombozi inafumbatwa katika uvumilivu wa Mungu unaomwilishwa katika upendo wake usiokuwa na mipaka. Uvumilivu ni nguvu na mwanzo mpya katika maisha ya mwanadamu. Kristo Yesu anawasubiri waja wake kwa uvumilivu mkubwa katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, ili aweze kuwapatia chakula cha njiani.

Fadhila ya uvumilivu huwawezesha waamini kutunza neema ya utakaso wanayo ipokea kutoka kwenye Ekaristi Takatifu. Mwishoni mwa katekesi yake kuhusu Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Uvumilivu wa Mungu ametoa Amri 10 kuhusu fadhila ya uvumilivu! Kardinali Charles Maung Bo., SDB, anasema, Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, kipindi cha neema na baraka inayowawezesha watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuweza kukutana, kusali, kuabudu Ekaristi Takatifu na kutafakari kuhusu matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Kanisa Katoliki nchini Hungaria ni kielelezo cha ushuhuda wa imani inayokita mizizi yake katika mateso ya watoto wake kama vile Mtakatifu Stephano wa Hungaria. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha uvumilivu ambao umeiwezesha Hungaria kuvuka walau kipeo cha Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kuambatana na Kristo Yesu, atakayewaonesha maajabu.

Fadhila ya uvumilivu iwasaidie watu wa Mungu kushinda kishawishi cha udini, ukabila na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uvumilivu uliwezeshe Kanisa kuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu ya Kipadre na kitawa. Uvumilivu uwawezeshe watu kukabiliana kikamilifu na changamoto ya Ugonjwa wa UVIKO-19, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano bora wa kuigwa katika fadhila ya uvumilivu. Kardinali Charles Maung Bo., SDB, anasema, Bikira Maria Mfungua Mafundo, awaombee waamini kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ili aweze kuwaonea huruma na hatimaye, kuwaondolea janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limepelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Awawezeshe kuanza tena upya na hatimaye, kuendelea na maisha yao ya kila siku katika hali ya amani na usalama.

Bikira Maria Mfungua Mafundo awafungulie watu wa Mungu mafundo yanayokwamisha maisha na shughuli zao za kila siku. Lakini zaidi, afungue mafundo ya uchoyo na ubinafsi; hali ya kutowajali wala kuwathamini wengine. Afungue mafundo ya kiuchumi na kijamii; ghasia na vita, ili hatimaye, asaidie kuimarisha imani, ili waamini waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu. Bikira Maria Mfungua Mafundo, awafungulie mafundo yanayokwamisha mahusiano na mafungamano ya kijamii katika ngazi mbalimbali, ili kukoleza na kudumisha furaha ya maisha ya kijumuiya, ili kuvuka vikwazo vya ubinafsi na hali ya kutojali! Kanisa linatambua kwamba, ukombozi ni matunda ya uvumilivu wa Bikira Maria. Uvumilivu ni hali ya kustahimili magumu kwa saburi. Kuna uvumilivu wa kimwili na kiakili unaohitajika ili kukabiliana na mahangaiko ya kijamii, ili kufikia muafaka. Uvumilivu wa kiroho huhitajika katika mambo yote ya kiroho, kwa kumwekea Mwenyezi Mungu matumaini yao. Familia ziwafunde watoto uvumilivu na saburi kwa maneno na matendo. Uvumilivu husaidia kuleta amani katika jamii ya watu. Mama Theresa wa Calcutta anahimiza fadhila ya uvumilivu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana na huduma, tayari kujielekeza katika njia iendayo mbinguni.

Uvumilivu unaunganisha nyoyo za watu “Bila Connection” mambo ni mazito wanasema Waswahili! Kukosekana kwa uvumilivu katika maisha ya watu wengi, kumepelekea: kinzani, mipasuko, vita, kutoweka kwa amani na utulivu wa ndani sanjari na kuwatengenezea watu madonda ya maisha ya kiroho. Uvumilivu ni changamoto kubwa katika maisha ya kiroho na kimwili. Uvumilivu ni chachu ya upendo na mshikamano wa familia, Kanisa dogo la nyumbani. Uvumilivu huwasaidia watu kuonja uwepo angavu na endelevu wa Mungu katika maisha yao, kwa kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mungu ni upendo! Historia nzima ya ukombozi ni ufunuo wa huruma, upendo na uvumilivu wa Mungu kwa mwanadamu. Kimsingi Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha uvumilivu wa Mungu anayejifunua kwa waja wake taratibu. Wanafunzi wa Emau walibahatika kuandamana na Yesu katika safari yao ya matumaini ya Kikristo bila kumtambua kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu?

Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Uvumilivu unawawezesha waamini kuwa ni Ekaristi ya imani, matumaini na mapendo kwa jirani zao! Uvumilivu ni kielelezo cha ufunuo wa haki ya Mungu kwa binadamu inayomwezesha mwanadamu kutubu na kumwongokea Mungu; tayari kujikita pia katika msamaha kwa jirani zake. Ili kuweza kukuza na kudumisha Injili ya Unyenyekevu, waamini wanapaswa kuzingatia Amri hizi zifuatazo: Kujivumilia wao wenyewe; kujenga na kudumisha maisha katika fadhila ya uvumilivu; kujenga amani kwa kujikita katika unyenyekevu. Waamini wajifunze fadhila ya unyenyekevu; Upendo wa kweli unarutubishwa na uvumilvu pamoja na imani. Uvumilivu ni fadhila yenye mvuto na mashiko na ni ngazi ya mafanikio katika maisha na msingi madhubuti wa amani duniani!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Stanisław Gądecki, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Poland amekazia kuhusu Injili ya matumaini, kama chemchemi ya haki na amani inayobubujika kutoka katika Amri 10 za Mungu, dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Amani ya kweli ni matunda ya toba na wongofu wa ndani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, amani haina budi kuchukuliwa katika mapana yake na wala si ukosefu wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu. Ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi.

Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Mamlaka sharti yaongozwe kwa sheria ya kimaadili. Heshima yake inatokana na kutekelezwa kwake katika muktadha wa taratibu ya kimaadili. Mamlaka sharti yatambue, yaheshimu na kukuza tunu muhimu za kiutu na kimaadili. Kristo Yesu ni kielelezo makini cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kujenga maisha yao kuzunguka Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani maisha yao yawe ni kielelezo cha shukrani na ushuhuda wa uwepo angavu na fungamani wa Kristo Yesu. Haki jamii inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani. Bila mambo haya sera na mikakati ya uchumi itakuwa ni hatarishi na kandamizi. Ekaristi Takatifu iwawezeshe waamini kujenga utamaduni wa upendo na amani ya kweli. Binadamu wote ni watoto wapendwa wa Mungu na wanapaswa kutambua kwamba, zawadi kubwa na ya kwanza ambayo wameipokea kutoka kwa Mungu ni uhai. Rej. AL 188.

Ekaristi Takatifu
09 September 2021, 14:19