Papa Francisko tarehe 13 Septemba 2021 amekutana na kuzungumza na wakleri, watawa na waseminari wa Slovakia: Fadhila ya unyenyekevu! Papa Francisko tarehe 13 Septemba 2021 amekutana na kuzungumza na wakleri, watawa na waseminari wa Slovakia: Fadhila ya unyenyekevu! 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Viongozi wa Kanisa!

Papa Francisko amekazia: Umuhimu wa Kanisa kuambata fadhila ya unyenyekevu katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika mchakato wa uhuru kamili unaowajibisha na kudumu. Kipaji cha ubunifu katika uinjilishaji na utamadunisho kinahitajika sana! Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. Uinjilishaji

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 13 Septemba 2021 katika hija yake ya kitume nchini Slovakia, baada ya kukutana na kuwahutubia viongozi wa Serikali, Vyama vya kijamii, Mabalozi na Wawakilishi mbalimbali waliko nchini Slovakia alipata bahati ya kuzungumza na Wakleri, Watawa, Waseminari na Makatekista kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Martin, Jimbo kuu la Bratislava. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia umuhimu wa Kanisa kuambata fadhila ya unyenyekevu katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika mchakato wa uhuru kamili unaowajibisha na kudumu. Kipaji cha ubunifu katika uinjilishaji na utamadunisho kinahitajika sana! Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini Slovakia kwa matamanio na matumaini waliyo nayo kwa Kanisa nchini mwao kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo waliokuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali na kutenda yote kwa umoja. Rej. Mdo1:2-14. Kanisa linahitaji kufanya hija ya pamoja ili kuwasha moto wa Injili. Kanisa ni jumuiya ya waamini ambao wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, upendo na amani duniani.

Kanisa halina budi kufuata mfano wa Kristo Yesu katika unyenyekevu. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” I Kor 8:9. Ni katika muktadha huu, Kanisa litakuwa na uwezo wa kufahamu na kushiriki matatizo, changamoto, matumaini na matarajio ya walimwengu. Hii ni changamoto kwa Kanisa kutoka katika hali ya kujitafuta lenyewe na kuanza kuhangaikia matatizo ya watu wa Mungu. Je, watu wa Mungu wanatarajia nini kutoka kwa Mama Kanisa? Baba Mtakatifu anajibu swali hili msingi kwa kusema ni uhuru kwani binadamu katika hulka yake ameumbwa kuwa huru. Lakini historia ya maisha ya mwanadamu inaonesha kwamba, kumekuwepo na mashambulizi dhidi ya uhuru, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikasiginwa, kiasi kwamba, uhuru wenyewe ukatoweka. Uhuru ni mchakato unaopaswa kupyaishwa kila wakati kwa kuwajibika kwa maamuzi yanayotolewa; kwa kufanya mang’amuzi pamoja na udumifu. Hii ndiyo historia ya Waisraeli katika Agano la Kale, walipopewa uhuru, wakakinai na kuanza kukumbuka “masufuria ya nyama na vitunguu swaumu utumwani Misri”.

Kanisa linaweza kujikuta katika hali na mazingira haya hususan katika maisha yake ya kiroho na hivyo, waamini kuwa wagumu na kuanza kujifungia katika ubinafsi wao. Hatari hii ni kubwa sana kwa vijana wa kizazi kipya ambayo wanaonekana kutovutwa sana na mambo ya imani, hali inayowakosesha uhuru wa ndani. Mama Kanisa anapaswa kuwahamasisha waamini kukuza na kuimarisha uhuru wao kwa kujenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Misimamo mikali ya kidini na kiimani haina budi kurekebishwa, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, chemchemi ya ukombozi wa mwanadamu. Kanisa halina budi kuwa ni alama ya uhuru na ukarimu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Familia ya Mungu nchini Slovakia ina urithi mkubwa katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho wa imani katika uhalisia wa maisha ya watu. Watakatifu Cyril na Method walitangaza na kushuhudia Injili kiasi cha kuanzisha herufi kwa ajili ya kutafsiri Biblia, Liturujia na Mafundisho ya Kanisa na hivyo wakawa ni Mitume wa Utamadunisho wa imani kati ya watu wa Mungu nchini Slovakia!

Huu ndio ubunifu unaotakiwa hata kwa watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo. Kanisa halina budi kutafuta njia na mbinu mpya ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, ili watu waweze kuonja ile furaha ya Injili. Watakatifu Cyril na Method walishtakiwa kwa kosa la ukanimungu kwa sababu waliweza kutafsiri imani yao katika Maandiko! Uinjilishaji maana yake ni mchakato wa utamadunisho, matunda ya upya wa maisha na karama ya Roho Mtakatifu anayepyaisha mambo yote! Kanisa linalowawezesha waamini kuwa na uhuru wa ndani na kuwajibika ni Kanisa ambalo haliwezi kushindwa kujitosa kikamilifu katika historia na tamaduni za watu, kwa kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kutangaza Injili ya upendo, umoja na urafiki kati ya watu! Umoja, muungano na majadiliano katika ukweli na uwazi ni mambo ambayo yanahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee kabisa, ili kuondokana na utamaduni wa kutaka kulipizana kisasi.

Hii ni changamoto kwa waamini kusali na kuwaombea huruma na upendo wa Mungu watesi na wale wote wanao wadhulumu! Hivi ndivyo Injili inavyotamadunishwa kwa kujikita katika unyenyekevu na upendo kamili. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewatakia watu wa Mungu nchini Slovakia ujasiri wa kudumu katika safari ya uhuru wa Injili; Ubunifu wa imani na majadiliano yanayobubujika kutoka katika huruma ya Mungu, ili kujenga haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Kanisa Slovakia
13 September 2021, 16:02