Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Septemba 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria wa Mateso. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Septemba 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria wa Mateso. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Bikira Maria wa Mateso

Papa amejikita zaidi kuhusu: Safari ya imani ya Bikira Maria; Imani kama kielelezo cha unabii na huruma inayomwilishwa katika huduma ya mapendo. Madhabahu ya Bikira Maria wa Šaštin ni kitovu cha imani na ibada kwa Bikira Maria anayewaongoza waamini kuelekea kwenye Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, aliyeyamimina maisha yake kama kielelezo cha upendo mkuu kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, madhabahu yana umuhimu wa pekee kabisa katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa ni mahali pa hija na kiri ya imani, ni chemchemi ya imani na matumaini yanayobubujika kutoka katika undani wa mtu! Ni kielelezo cha umisionari wa watu wa Mungu, mahali pa sala, tafakari ya Neno la Mungu na kujiaminisha katika huruma na upendo wa Mungu unaoganga, kuponya na kuokoa. Tangu mwanzo madhabahu yamekuwa ni mahali pa kwenda kutafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Pasaka kiasi cha kuibua ibada kwa Bikira Maria, Mitume, Watakatifu na Wenyeheri. Baba Mtakatifu anaendelea kukaza akisema, madhabahu ni mahali ambapo waamini wanashuhudia imani na kuonja uwepo wa daima wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Uwepo wa Bikira Maria na Watakatifu unawaonjesha huruma na upendo ambao ni kazi kubwa ya Roho Mtakatifu. Madhabahu yameunda na kujenga utamaduni wa baadhi ya familia na mataifa. Kumekuwepo na makundi makubwa ya mahujaji, yanayotaka kusali, kuadhimisha Liturujia ya Kanisa na kumshukuru Mungu kwa neema na baraka zake katika safari ya maisha yao. Kimsingi madhabahu ni mahali pa uinjilishaji mpya!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mateso Saba, Jumatano tarehe 15 Septemba 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Šaštin nchini Slovakia. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia mambo makuu matatu: Safari ya imani ya Bikira Maria; Imani ya Bikira Maria kama kielelezo cha unabii na huruma inayomwilishwa katika huduma ya mapendo. Madhabahu ya Bikira Maria wa Šaštin ni kitovu cha imani na ibada kwa Bikira Maria anayewaongoza waamini kuelekea kwenye Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, aliyeyamimina maisha yake kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Bikira Maria baada ya kupaswa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu aliondoka kwa haraka kwenda kumtembelea binamu yake Elizabeti. Kwa unyenyekevu na furaha yake ya ndani, alitambua kwamba, alikuwa amekabidhiwa utume ambao alipaswa kuumwilisha katika huduma ya upendo, kiasi kwamba, imani yake ikawa ni zawadi kwa jirani zake.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee amemwonesha Bikira Maria akiwa ameambatana na mchumba wake Mtakatifu Yosefu kwenda Yerusalemu, ili kumpeleka Mtoto Yesu Hekaluni. Katika safari ya maisha yake yote, Bikira Maria ataendelea kumsindikiza Kristo Yesu katika maisha na utume wake, hadi atakaposimama chini ya Msalaba pale mlimani Kalvari. Kwa watu wa Mungu nchini Slovakia, Bikira Maria ni kielelezo cha imani inayomwilishwa katika ibada, kielelezo cha safari ya maisha ya kiroho ili kumtafuta Mwenyezi Mungu. Katika safari kama hii, vishawishi na magumu havikosekani, lakini yote haya yanasaidia kunogesha hija ya upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu amewashukuru waamini wote kwa ushuhuda huu wenye mvuto na mashiko, unaoendelea kudumishwa! Baba Mtakatifu ameongeza kusema, Kanisa likisimama na kubweteka, linaugua, Maaskofu wakisimama, Kanisa linaugua na mapadre nao wakisimama bila kujishughulisha, watu wa Mungu wanaugua!

Imani ya Bikira Maria ni kielelezo cha unabii unaonesha na kushuhudia uwepo wa Mungu katika historia ya mwanadamu na huruma yake inayowaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi na kuwakweza wanyonge. Bikira Maria anajitambulisha kuwa ni kati ya maskini wa Bwana. Huyu ndiye Mama wa Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na kukaa kati ya waja wake. Huyu ni Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Bikira Maria ni kielelezo cha wito wa Wakristo wote wanaohamasishwa kuwa ni watakatifu wasiokuwa na mawaa katika upendo kwa mfano wa Kristo Yesu! Rej. Efe 1:4. Unabii wa Agano la Kale unapata maana na utimilifu wake katika maisha ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa anayeshiriki kutekeleza mpango wa kazi ya ukombozi. “Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.” Lk 2:34-35. Maisha ya imani yanachangamoto zake na kamwe si raha mustarehe!

Kristo Yesu ni alama ya kinzani, kwani ni mwanga unaofukuzia mbali giza! Kwa wale wanaothubutu kumpokea wanatembea katika mwanga wa maisha na wale wanaomgeuzia kisogo, wanabaki wakielemewa na giza. Kristo Yesu anakaza kusema, “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.” Mk 10:34. Huu ni upanga unaotenganisha mwanga na giza na unaotaka maamuzi makini ya maisha. Kwa wale wanaompokea na kumkubali katika maisha anawasaidia kuona ukweli wa maisha yao na hivyo kuwakirimia neema na baraka za kuweza kufufuka tena; kusimama na kuwaongoza katika mapito mapya. Slovakia inahitaji manabii wapya, wakristo watakaosimama kidete katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni! Slovakia inahitaji mashuhuda wa mshikamano, ukarimu na udugu wa kibinadamu, ili kushinda ubinafsi na kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anasema, Bikira Maria ni Mama wa huruma inayomwilishwa katika huduma ya mapendo. Bikira Maria aliweza kuwarejeshea tena wanaharusi wa Kana ya Galilaya furaha baada ya kutindikiwa na divai. Akathubutu kufuata ile Njia ya Msalaba hadi kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye mpendwa, Kristo Yesu! Upanga wenye makali, ukapenya moyoni mwake! Kristo Yesu ndiye yule Mtumishi mwaminifu wa Mungu aliyetabiriwa na Nabii Isaya akisema “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Is 53: 3-5. Bikira Maria aliteseka sana moyoni mwake kama Mama mwenye huruma na bado anaendelea kufuta machozi ya watoto wake na kuwafariji hadi pale ushindi wa kishindo utakapopatikana. Bikira Maria wa mateso amebaki chini ya Msalaba, hataki kukimbia au kujiokoa mwenyewe wala kukwepa mateso yake ya ndani.

Huu ni uthibitisho wa mateso, kwa kusimama chini ya Msalaba, huku akilia, lakini kwa imani anatambua kwamba, Mwanaye, Kristo Yesu ana uwezo wa kugeuza mateso na magumu hadi kupata ushindi dhidi kifo na mauti! Huu ni mwaliko kwa waamini kufungua nyoyo zao kwa imani inayomwilishwa katika huruma; imani inayowatambua wale wote wanaoteseka na kulazimika kubeba misalaba mizito katika maisha. Lakini, anageuka kuwa ni rafiki kwa wale wote wenye mahitaji msingi. Hii ni imani inayojitahidi kuiga jinsi anavyotenda Mungu, polepole anapowaondolea walimwengu na kuirutubisha historia ya nchi kwa wokovu! Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia heri na baraka watu wote wa Mungu nchini Slovakia. Anawaombea ili Mwenyezi Mungu aendelee kutunza ndani mwao mshangao na shukrani ya zawadi kuu ya imani. Bikira Maria wa Mateso awaombee neema ya imani inayopyaisha maisha yao kwa kuwazamisha katika imani thabiti yenye unabii na wingi wa huruma!

Bikira Maria wa Mateso
15 September 2021, 15:29