Maadhimisho ya Siku ya VII ya Dunia ya Kuombea Utunzaji Bora wa Kazi ya Uumbaji Maadhimisho ya Siku ya VII ya Dunia ya Kuombea Utunzaji Bora wa Kazi ya Uumbaji 

Siku ya Dunia ya Kuombea Utunzaji wa Kazi ya Uumbaji 2021

Papa anawapongeza “Wanaharakati wa Laudato si” kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Wanahakati wa Laudato si wako mstari wa mbele kuhamasisha maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira sanjari na maadhimisho ya Kipindi cha Kazi ya Uumbaji kinachoanza tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa tarehe 1 Septemba 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake” Zab 24:1. Siku hii ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015. Hii ni sehemu ya mchakato endelevu na fungamani wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Mama Dunia na Maskini, “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.”

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 29 Agosti 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwashukuru na kuwapongeza “Wanaharakati wa Laudato si”. Hawa wameendelea kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Wanaharakati wa Laudato si wako mstari wa mbele kuhamasisha maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira sanjari na maadhimisho ya Kipindi cha Kazi ya Uumbaji kinachoanza tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini” kinaendelea kusikika sehemu mbalimbali za dunia, kuonesha hatari kubwa inayoikabili Jumuiya ya Kimataifa. Kumbe, kuna haja ya kusikiliza na kujibu kilio hiki, kwa kuibua sera na mbinu mkakati wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kilio hiki iwe ni fursa itakayoisaidia Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuanzisha majadiliano mapya kuhusu namna ya kuujenga mustakabali wa dunia hii, kwa kuwahusisha watu wote kwa sababu changamoto za mazingira zinawahusu na kuwaathiri watu wote. Vipaji vya kila mmoja na ushiriki wake vinahitajika kama vyombo vya Mungu kwa ajili ya kuyatunza maumbile, kila mmoja kadiri ya utamaduni, mang’amuzi, shughuli na vipaji vyake. Rej. “Laudato si”, 14. Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, linatekelezwa katika kipindi cha miaka saba. Mwaka wa kwanza ni mchakato wa ujenzi wa jumuiya, ushirikishanaji wa rasilimali na utengenezaji wa sera na mikakati ya utekelezaji kadiri ya mwono wa ikolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ekolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ekolojia pamoja na ushirikishwaji wa jumuiya! Mwaka wa Saba, utatumika kumsifu na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Kazi ya Uumbaji.

Wanaharakati wa Laudato si wanasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa toba na wongofu wa kiikolojia, kama mbinu mkakati wa kupambana na athari kubwa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Huu pia ndio mwelekeo wa juhudi za kiekumene katika kulinda mazingira nyumba ya wote. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Mkutano wa 26 wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 utafanyika kuanzia tarehe 1-12 Novemba 2021 huko mjini Glasgow nchini Scotland. Hizi ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna maafa na majanga makubwa yanayotokana na ukame wa kutisha, mafuriko pamoja na majanga ya moto sehemu mbalimbali za duniani. Matokeo yake ni watu wengi kuanza kunyemelewa na baa la njaa na utapiamlo.

Papa Mazingira
30 August 2021, 15:34