Papa Francisko mshikamano wa udugu wa upendo na waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Haiti. Watu waoneshe kwa hali na mali mshikamano huo wa upendo! Papa Francisko mshikamano wa udugu wa upendo na waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Haiti. Watu waoneshe kwa hali na mali mshikamano huo wa upendo! 

Papa: Mshikamano wa Udugu & Upendo na Wananchi wa Haiti!

Hadi kufikia Jumatatu asubuhi tarehe 16 Agosti 2021 zaidi ya watu 1, 297 wamekwisha kufariki dunia na majeruhi ni zaidi ya 1, 800. Baadhi ya hospitali ambazo bado zinafanya kazi zinaendelea kuwahudumia majeruhi 5, 700, wengi wao wakiwa hawana mahali pa kulazwa. Vikosi vya ulinzi na usalama vinaendelea na jitihada za kuwaokoa watu ambao bado wamefukiwa na vifusi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea nchini Haiti, Jumamosi, tarehe 14 Agosti 2021, hadi kufikia Jumatatu asubuhi tarehe 16 Agosti 2021 zaidi ya watu 1, 297 wamekwisha kufariki dunia na majeruhi ni zaidi ya 1, 800. Baadhi ya hospitali ambazo bado zinafanya kazi zinaendelea kuwahudumia majeruhi 5, 700, wengi wao wakiwa hawana mahali pa kulazwa. Vikosi vya ulinzi na usalama vinaendelea na jitihada za kuwaokoa watu ambao bado wamefukiwa na vifusi baafa ya kuangikiwa na majengo. Takwimu zinaonesha kwamba, nyumba 13, 694 zimeporomoka na pengine idadi hii ikaendelea kuongezeka zaidi. Hofu kubwa kwa sasa ni dhoruba kali Kitropikali iliyopewa jina la “Grace” ambayo kwa kawaida inaambatana na maporomoko ya udongo, hatari kwa maisha!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Jumapili tarehe 15 Agosti 2021 ameonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini Haiti ambao wamekumbwa na tetemeko la ardhi. Anasema, mshikamano wa udugu na upendo kutoka kwa watu wote, ulete faraja kwa waathirika wa maafa haya nchini Haiti. Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Haiti. Akatoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa watu wa Mungu nchini Haiti.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB katika ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti, linapenda kuonesha mshikamano na uwepo wake wa karibu kwa watu wote wa Mungu nchini Haiti kwa kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwili na roho. Katika nyakati hizi za majaribu na hali ya kukata tamaa, watu wa Mungu nchini Haiti, waonje faraja, huruma na upendo wa Bikira Maria. Bikira Maria Msaada wa Daima, Mlinzi wa Haiti, aendelee kuwaombea kwa Kristo Yesu! Maaskofu Katoliki Marekani wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchangia kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Haiti. Jimbo Katoliki la Jérémie lenye Parokia 55 ni kati ya maeneo yaliyoathirika sana na tetemeko hili. Watu wengi wamekata tamaa na kupoteza matumaini ya kuendelea kuishi.

Itakumbukwa kwamba, hadi kufikia Jumatatu asubuhi tarehe 16 Agosti 2021, watu waliokuwa wameambukizwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 walikuwa wamefikia 20, 556. Waliokwisha kufariki dunia ni 576 na waliolazwa hospitalini ni 16, 004 na huko hali ni tete sana baada ya tetemeko la ardhi. Haiti kunako mwaka 2010 ilikumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha watu 220,000 kupoteza maisha. Watu zaidi ya milioni 1.5 wakakosa mahali pa kuishi na wengine 300, 000 wakapata majeraha na ulemavu wa kudumu. Haiti katika siku za hivi karibuni imekumbwa na machafuko ya kisiasa kutokana na uchu wa mali na madaraka baada ya mauaji ya kikatili dhidi ya Rais Jovenel Moïse wa Haiti yaliyofanyika nyumbani kwake usiku wa kuamkia Jumatano tarehe 7 Julai 2021, Baba Mtakatifu Francisko kwa nguvu zote alilaani ghasia na matumizi ya nguvu kama njia ya kutafuta suluhu ya migogoro na changamoto za maisha nchini Haiti. Baba Mtakatifu anaendelea kuiombea Haiti pamoja na watu wake kuanza kujikita katika ujenzi wa umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Papa Haiti
16 August 2021, 14:42