Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuwa ni mashuhuda wa unabii, kwa kuonesha umoja, upendo na mshikamano na maskini zaidi duniani! Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuwa ni mashuhuda wa unabii, kwa kuonesha umoja, upendo na mshikamano na maskini zaidi duniani! 

Papa Francisko: Watawa Onesheni Ushuhuda wa Kinabii Ulimwenguni

Papa Francisko aliwaalika watawa kuwaamsha walimwengu kwa njia ya ushuhuda wao wa kinabii, kwa kuonesha mshikamano wa dhati kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watawa katika umoja na mshikamano wao, wawe ni mashuhuda wake amini na vyombo vya huruma ya Mungu kwa maskini. Daima Mwenyezi Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kardinali Joào Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume “CICLSAL” anasema maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, 2015, kilikuwa ni kipindi cha neema na baraka. Ulikuwa ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Jubilee ya Miaka 50 tangu Hati kuhusu Mapendo Kamili, yaani Perfectae caritatis ilipochapishwa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikazia kuhusu umuhimu wa kufanya mabadiliko ya kina katika maisha na utume wa watawa. Waliwataka watawa kusoma alama za nyakati, kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na kuwa waaminifu kwa karama za mashirika yao, na hatimaye, kumwangalia mwanadamu katika ulimwengu mamboleo! Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ilikuwa ni kutambua kwa unyenyekevu mkubwa mapungufu yanayojitokeza katika maisha ya kitawa, lakini pia kupaaza sauti kwa nguvu na furaha kwa utakatifu na uhai wa maisha ya kitawa katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Watawa wanajitahidi kumwonesha Mwenyezi Mungu ambaye ni Mtakatifu sana katika ubinadamu, licha ya uwepo wa dhambi, lakini bado neema ya Mungu inaendelea kutenda kazi!

Lengo la Pili la Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani lilikuwa ni kuwa na matumaini kwa siku za usoni kwa kutambua changamoto na kinzani zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa watawa kama ambavyo aliwahi kudokeza Mtakatifu Yohane Paulo II. Mmong'onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema ndani ya jamii unagusa pia hata Kanisa na maisha ya kitawa, changamoto ya kufanya mageuzi na matumaini si katika nguvu na uwezo wa kibinadamu, bali kwa Kristo Yesu mwenyewe anayeongoza mchakato wa mabadiliko ndani ya Kanisa. Ni matumaini kwamba, licha ya magumu na changamoto mbalimbali zilizopo, maisha ya kitawa ndani ya Kanisa yataendelea kuwapo na hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuwapokonya watawa matumaini waliyo nayo! Baba Mtakatifu Francisko aliwaalika watawa kuwaamsha walimwengu kwa njia ya ushuhuda wao wa kinabii, kwa kuonesha mshikamano wa dhati kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watawa katika umoja na mshikamano wao, wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa maskini. Mwenyezi Mungu anawaita, kuwatakasa na kuwatuma sehemu mbalimbali za dunia, ili waweze kuwa ni mashuhuda wake amini. Daima Mwenyezi Mungu ni mwaminifu.

Huu ni mwaliko wa kuendelea kuandika historia yenye mvuto na mashiko kwa sasa na kwa siku za usoni. Kamwe watawa wasijiridhishe na historia kubwa iliyoandikwa na Mashirika yao kwa miaka iliyopita! Watawa waendelee kufanya mabadiliko na mageuzi ya ndani mintarafu changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Waoneshe ujasiri, uaminifu na kipaji cha cha ubunifu! Haya ni mambo makuu ambayo wajumbe wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika Nchi za Afrika Mashariki na Kati, yaaani ACWECA, wamekumbushwa tena na Kardinali Joào Braz de Aviz! ACWECA kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 27 Agosti 2021 inaadhimisha Mkutano wake wa 18 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kupyaisha Jukumu Letu la Kinabii: Mwaliko wa Kufanya Mabadiliko Kamili katika Ukanda huu”. Kauli mbiu hii inanogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu lisemalo: “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Rum 12: 1-2.

Kardinali Joào Braz de Aviz katika hotuba yake elekezi ametoa salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa 18 ACWECA, ambao kwa mwaka 2021 unaadhimishwa kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu amewaweka watawa wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, watawa wanapaswa kuonesha uwepo endelevu na angavu wa Mungu katika maisha na utume wao wa kinabii. Watawa wawasaidie watu wa Mungu wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na UVIKO-19 kwa kukosa maarifa. Watawa wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Watawa wawaelimishe waamini kutambua uwezo wa Mungu unaofanya kazi kwa kutumia watu wa kawaida. Uongozi katika maisha ya kitawa ni huduma makini sanjari na kujifunza kusikiliza kwa umakini na upendo mkuu, tayari kuwasindikiza wale waliokata tamaa na kuvunjika moyo. Viongozi wa Kanisa wasaidie watu wa Mungu kupata suluhu ya matatizo na changamoto za maisha. Wawasaidie watawa wenzao kujisikia kwamba wako nyumbani na wala si utumwani kiasi hata cha kutamani kuachana na maisha ya kitawa! Tunu msingi za Kiinjili ziwe ni dira na mwongozo wa maisha.

Kwa upande wake Mheshimiwa Padre Anthony Makunde, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, amewataka watawa kusimama kidete kupambana na: umaskini wa hali na kipato; ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Wawe makini dhidi ya nyanyaso mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika maisha na utume wao. Wawe mahiri kupambana na mifumo mbalimbali ya rushwa; uchu wa mali na madaraka. Watawa wawe ni mfano wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watawa wapyaishe jukumu lao la kinabii kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wao! Amri za Mungu ziwe ni dira na mwongozo wa maisha tayari kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu sanjari na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Pamoja na mambo yote hayo, washikamane katika umoja na udugu wa kibinadamu. “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.” Yn 17:15-18.

Naye Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Sr. Cecilia Njeri, (LSOSF), amesema, wanaadhimisha mkutano huu wakati ambapo janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 linaendelea kupamba moto kutokana na maambukizi makubwa. Baa la njaa, umaskini, magonjwa na ukosefu wa usawa pamoja na haki msingi za binadamu; ni mambo yanayoendelea kushamiri katika ulimwengu mamboleo. Kuna watu wengi wamepoteza fursa za ajira na matokeo yake wamejikatia tamaa ya maisha kutokana pia na hali ngumu ya maisha. Mashirika mengi ya kitawa na kazi za kitume yameathirika pia. WATAWA wanapaswa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, watazozivalia njuga kama sehemu ya mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.  ACWECA imeendelea kujikita zaidi katika masuala ya: Malezi na majiundo ya kitawa; utume wa familia na vijana; maendeleo fungamani ya binadamu bila kusahau dhamana na utume wa watawa katika maisha ya Kanisa. Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika Nchi za Afrika Mashariki na Kati, yaaani ACWECA linaundwa na: Eritrea, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Kenya, Uganda, Tanzania, Zambia, Malawi na Zimbabwe.

Watwa Afrika

 

 

26 August 2021, 14:33