Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo imechafua maisha na utume wa Kanisa. Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo huko Varsavia 19-22 Septemba 2021. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo imechafua maisha na utume wa Kanisa. Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo huko Varsavia 19-22 Septemba 2021. 

Kashfa ya Nyanyaso za Kijinsia Ndani ya Kanisa! Yaliyotendeka!

Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo kwa kushirikiana na Kituo cha Ulinzi wa Watoto Wadogo Poland, imeandaa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo utakaoadhimishwa huko Varsavia, Poland, Mwezi Septemba 2021. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuwa na sera ya pamoja kwa Makanisa yote mahalia Ukanda huu dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu aliitisha Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo uliofanyika mjini Vatican kuanzia Alhamisi tarehe 21 hadi Jumapili tarehe 24 Februari 2019. Huu ni mkutano uliowajumuisha Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia, pamoja na viongozi waandamizi wa Kanisa Katoliki, ili waweze kukaa kwa pamoja na kupembua kwa kina na mapana kuhusu ulinzi wa watoto ndani ya Kanisa. 

Mkutano huo ulikuwa ni kielelezo makini cha wajibu wa kichungaji ili kuweza kukabiliana na changamoto hii nyeti katika ulimwengu mamboleo. Lengo ni kutoa katekesi kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia, ili Maaskofu waweze kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, watu walionyanyaswa kijinsia wanakabiliana na hali ngumu sana katika maisha yao: kiroho na kiutu. Kwa mara ya kwanza, viongozi wa Kanisa walipembua kwa kina na mapana mbinu mkakati wa kuwalinda watoto wadogo pamoja na kuanzisha miundo mbinu ya kimataifa itakayoshughulikia nyanyaso hizi. Wajumbe walifanya tafakari ya kina kuhusu wajibu wa Askofu mahalia: kichungaji na kisheria. Na Askofu mahalia anawajibika kwa na nani: hapa ni mahali pa kuangalia mfumo mzima, taratibu na kanuni katika mchakato mzima wa utekelezaji wake. Hapa umuhimu wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa unapaswa kuzingatiwa.

Viongozi wa Kanisa walijikita katika dhana ya ukweli na uwazi ndani ya Kanisa, Serikali na kwa watu wa Mungu katika ujumla wao! Changamoto kubwa hapa ni mchakato wa Kanisa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kubadili mwelekeo na mtazamo kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Wajumbe walipata nafasi ya kusikiliza kwa makini shuhuda za baadhi ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia! Ni katika muktadha huu, Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM, kwa kushirikiana na Kituo cha Ulinzi wa Watoto Wadogo Poland “Centrum Ochrony Dziecka / Child Protection Centre, Kraków, Poland” imeandaa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo utakaoadhimishwa huko Varsavia, Poland kuanzia tarehe 19 hadi 22 Septemba 2021 kwa kuzishirikisha nchi 18 kutoka Ulaya ya Kati na Mashariki. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuwa na sera na mikakati ya pamoja kwa Makanisa yote mahalia Ukanda huu dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo. Huu ni muda wa kufanya tafiti makini, kujenga utamaduni wa kusikiliza, ili kubainisha hatua ambazo zimekwisha kuchukuliwa na Mama Kanisa katika mapambano dhidi ya Kashfa ya Nyanyaso za Kijinsia ndani ya Kanisa. Ni fursa ya kuibua mambo msingi ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga ili kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Padre Federico Lombardi, SJ., aliyeratibu Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo kwa mwaka 2019 anasema, katika ulimwengu mamboleo Kanisa halina budi kusimama kidete kupambana na changomoto tete zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wake. Changamoto ya kwanza ni ile inayofumbatwa katika msingi wa imani sanjari na kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mchakato huu wa uinjilishaji mpya ulitiwa “madongo” kwa kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo! Hili ni kosa kubwa! Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo katika ujumla wake ni tatizo na changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo. Kumbe, hii si changamoto ya Kanisa Katoliki peke yake. Kwa Kanisa Katoliki hii ni changamoto inayolishushia Kanisa hadhi yake. Mama Kanisa daima amekuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kashfa hii inapotendeka ndani ya kuta za Kanisa inachafua maisha, utume na dhamana ya Kanisa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Ni kwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu, utu na heshima ya hao walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kashfa hii ni kinyume kabisa cha imani na mwono wa ulimwengu! Baba Mtakatifu amefanya mabadiliko makubwa katika Sheria za Kanisa. Kati ya makosa ya uhalifu, yapo yale ambayo yanatambuliwa kuwa ni makosa makubwa ya uhalifu, “Delicta graviora”, na yametengwa ili kushughulikiwa, sio tena na Askofu Jimbo wala Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume, bali na Mahakama maalumu iliyoundwa kwenye Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo kwa mwaka 2019 ulijikita zaidi katika mchakato wa ukweli na uwazi; utambuzi wa makosa na uwajibikaji kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Tangu wakati huo, kumekuwa na hatua kubwa ambazo zimechukuliwa na Mama Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na wajumbe wa mkutano huo. Sekretarieti kuu ya Vatican imejiwekea Sheria, Kanuni na Taratibu za Kufuatwa.

Tarehe 9 Mei 2019, Baba Mtakatifu Francisko alichapisha Barua Binafsi “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia”. Hii ni mbinu mkakati wa kichungaji kwa ajili ya kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kwa muhtasari, barua hii inawataka Maaskofu na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuwajibika barabara katika kushughulikia tuhuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Hadi kufikia mwezi Juni 2020, Mabaraza ya Maaskofu pamoja na Majimbo yote ya Kanisa Katoliki yalipaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kuwasilisha shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Wakleri na watawa kwa sasa wanatakiwa kisheria kuhakikisha kwamba, wanatoa taarifa kuhusu nyanyaso za kijinsia wanazozifahamu. Tangu sasa hakutakuwepo tena na mwanya wa kuwalinda watuhumiwa wa nyanyaso za kijinsia na kwamba, wale wote wanaotoa habari pamoja na waathirika wanapaswa kulindwa na kamwe wasibezwe na kunyanyaswa!

Mwongozo Unakazia Mambo Makuu Manne: Kipaumbele cha kwanza ni ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Viongozi wa Kanisa wanahimizwa kuhakikisha kwamba, wanajizatiti kulinda heshima na utu wa waathirika pamoja na familia zao. Wakazie umuhimu wa kuwapokea, kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwahudumia kwa hali na mali. Padre Federico Lombardi, SJ., anakaza kusema, Mwezi Julai, 2020, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limechapisha Mwongozo wa Mchakato wa Kesi za Unyanyasaji wa Kijinsia Dhidi ya Watoto Wadogo Ndani ya Kanisa, “Vademecum” ili ukweli uweze kufahamika na haki kutendeka. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendeleza Utume wake wa kutaka kudhibiti uhalifu na kumrekebisha mhalifu; kutenda haki kwa waliokosewa; na kuondoa kashfa! Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2021, Mama Kanisa amechapisha upya Kitabu cha Saba cha Sheria za Kanisa kwa kuingiza mabadiliko yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko. Changamoto kubwa mbele ya Kanisa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, Sheria, Kanuni na Taratibu hizi zinatekelezwa kikamilifu kwa ajili ya ulinzi, ustawi, malezi na makuzi ya watoto wadogo. Ni wakati wa kutenda kwa haki, kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa na hivyo kurejesha tena hadhi ya Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake!

Kashfa ya Nyanyaso
28 August 2021, 15:16