Papa Francisko amemteua Kardinali Giovanni Battista Re kuwa Mwakilishi wake wa kitume kwenye kumbukuzi la Jubilei ya Miaka 500 tangu Bikira Maria wa Oropa alipovikwa taji la dhahabu. Papa Francisko amemteua Kardinali Giovanni Battista Re kuwa Mwakilishi wake wa kitume kwenye kumbukuzi la Jubilei ya Miaka 500 tangu Bikira Maria wa Oropa alipovikwa taji la dhahabu. 

Madhabahu B.Maria wa Oropa: Kumbukizi la Miaka 500 Taji la Dhahabu!

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kuwa Mwakilishi wake wa Kitume katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Kuvikwa Taji kwa Bikira Maria wa Oropa, kwenye Madhabahu ya Jimbo Katoliki Biella, lililoko Kaskazini mwa Italia. Kilele cha Jubilei hii ni hapo tarehe 29 Agosti 2021. Ulinzi na tunza ya Bikira Maria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya utimilifu na utakatifu wa maisha. Hapa ni mahali pa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu! Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya Wakristo, daima wako chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Wao ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, kama sehemu ya Kanisa wanao wajibu na dhamana ya kuliombea Kanisa zima; kuwaombea watu wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali; watu wanaoogelea katika dimbwi la huzuni na machungu ya maisha; wagonjwa na wale wote walioko kufani; wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau watu wanaoteseka kutokana na athari za majanga asilia.  Haya ni maeneo yanayodhihirisha ufunuo wa: Upendo, ukuu, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake. Hapa kipaumbele cha kwanza ni uwepo wa Mungu ndani ya Kanisa na maisha ya kila mwamini. Mwenyezi Mungu ndiye anayepanga na kuamua mahali na muda wa kujifunua kati ya waja wake!

Waamini wanapaswa kubaki katika ukimya ili kumsikiliza Mwenyezi Mungu kwa umakini mkubwa, pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati kwa njia ya matukio mbalimbali yanayoweza kusaidia mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kuwa Mwakilishi wake wa Kitume katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Kuvikwa Taji kwa Bikira Maria wa Oropa, kwenye Madhabahu ya Jimbo Katoliki Biella, lililoko Kaskazini mwa Italia. Kilele cha Jubilei hii ni hapo tarehe 29 Agosti 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Kardinali Giovanni Battista Re, anataja uzuri na sifa za Bikira Maria zinazosimuliwa na Malaika kwa kusema: “Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili.” Ufu: 12:1.

Bikira Maria ni Malkia na Mama anayeendelea kuwaangalia na kuwatunza watu wa Mungu kwa upendo wenye huruma. Wafuasi wa Kristo Yesu wamekuwa wakikimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika kipindi cha zaidi ya Miaka 600 iliyopita. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha waamini kupata neema na baraka kwa maombezi ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu anasema, anamfahamu vyema Askofu Roberto Farinella wa Jimbo Katoliki la Biella, lakini angependa Kardinali Giovanni Battista Re, kuwa Mwakilishi wake wa Kitume, tarehe 29 Agosti 2021 wakati Sanamu Bikira Maria wa Oropa itakapokuwa inavikwa taji la dhahabu, tukio linalorudiwa kila baada ya miaka mitano, kuanzia mwaka 1620. Ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na taji la dhahabu litawekwa tarehe 29 Agosti 2021. Anamwomba amfikishie salam zake kwa waamini watakaohudhuria Ibada hii ya Misa takatifu. Baba Mtakatifu anapenda kuhakikishia uwepo wake kwa njia ya sala, maombezi na tunza ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu ambaye kwa Mwaka huu, Kanisa linaadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu na kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Eusebio wa Vercelli alivyotangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu. Mwishoni. Baba Mtakatifu anampatia baraka zake za kitume!

Dekano wa Makardinali
21 August 2021, 15:13