Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Slovakia inaongozwa na kauli mbiu: Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu. Maaskofu wametoa Waraka wa Kichungaji! Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Slovakia inaongozwa na kauli mbiu: Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu. Maaskofu wametoa Waraka wa Kichungaji! 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Waraka wa Maaskofu

Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia linawaalika watu wa Mungu kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya ujio wa Papa Francisko nchini mwao. Kipaumbele cha kwanza ni maandalizi ya kiroho kwa njia ya sala na sadaka, iliMwenyezi Mungu aweze kuwakirimia neema na baraka wakati wa ujio wa Papa Francisko nchini mwao, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) yatayaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu Francisko anategemea kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa.  Baadaye, atafanya hija ya kitume nchini Slovakia, kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Slovakia ili kuitembelea nchi yao.

Hija inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Kwa hakika Familia Takatifu ilionesha upendo wa dhati kabisa kwa Kristo Yesu katika maisha yake. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutembelea na kuzungumza na watu wa Mungu katika miji ya: Bratislava, Prešov, Košice na Šaštin. Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia, KBS katika Waraka wake wa kichungaji linawaalika watu wa Mungu nchini Slovakia kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao. Kipaumbele cha kwanza ni maandalizi ya kiroho kwa njia ya sala na sadaka, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia neema na baraka wakati wa ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo.

Hija hii inafanyika wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020. Mwaka huu unatarajiwa kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake sanjari na kutambua uwepo wake endelevu katika maisha ya waja wake.

Kilele cha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ni katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu mjini Šaštín na Ibada ya Liturujia Takatifu kwa Mapokeo ya Kibizantini ya Mtakatifu Yohane Chrysostom huko mjini Prešov. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na wawakilishi wa Makanisa ya Kikristo kwenye Ukumbi wa Kumbukumbu ya Mauaji ya Kinyama mjini Bratislava. Lengo ni kuendeleza mchakato wa ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu kama kielelezo cha Mchungaji mwema, atatembelea Jumuiya ya Watawa wa Shirika la Wamisionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta wanaoishi huko Petržalka na Luník.

Baba Mtakatifu Francisko kama Baba, Mwalimu na Mtume atazungumza na wakleri na watawa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Martin mjini Bratislava na baadaye “atachonga” na vijana wa kizazi kipya kwenye Uwanja wa Michezo wa Košice. Hija hii ya kitume wanasema Maaskofu wa Slovakia inalenga kuimarisha: imani, matumaini, maadili na utu wema kielelezo makini cha imani tendaji. Waamini wanahamasisha kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mikutano hii, ili kujenga umoja, mshikamano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu. Kwa wale watakaoshindwa kuhudhuria wanaweza kufuatilia matukio haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Huu ni muda wa kutangaza na kushuhudia imani kwa matendo adili na matakatifu. Kwa namna ya pekee kabisa, tarehe 15 Septemba 2021 Mama Kanisa ataadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria, Mama wa Mateso saba. Kwa mara ya kwanza, kumbukumbu hii kitaifa, itaadhimishwa kwa uwepo pia wa Baba Mtakatifu Francisko. Leo hii, Bikira Maria anawaonesha huruma wale wote wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini sanjari na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na wakuu wa ulimwengu huu. Bikira Maria Mama wa Mateso awe ni faraja kwa wale wanaoteseka; matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo na awe ni chemchemi ya huruma na mapendo kwa wenye huzuni na mahangaiko makubwa!

Maaskofu Slovakia
30 August 2021, 16:12