Papa Francisko ametuma ujumbe maalum kwa washiriki wa mkutano mkuu wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko: Kupyaisha dira na kupokea yajayo kwa moyo wa toba. Papa Francisko ametuma ujumbe maalum kwa washiriki wa mkutano mkuu wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko: Kupyaisha dira na kupokea yajayo kwa moyo wa toba. 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Mkutano Mkuu wa Wafranciskani

Papa Francisko anasema kwamba, hiki ni kipindi muafaka cha kujikita katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu; wito na mwaliko wa kuwa ni mashuhuda wa uwepo wa kinabii kati pamoja na watu wa Mungu; kwa kuishi katika umoja na udugu wa kibinadamu pasi na makuu. Watawa wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili na wakumbuke kuwa hapa ni wapita njia tu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Wafrancisko wa Assisi wamemchagua Mheshimiwa Padre Giovanni Fusarelli kuwa Mkuu mpya wa Shirika kwa kipindi cha miaka sita yaani kuanzia mwaka 2021 hadi mwa 2027. Anakuwa ni mkuu wa Shirika wa 121 kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Kauli mbiu ambayo imenogesha maadhimisho haya ni “Tupyaishe dira yetu, tuyapokee yajayo”. Ni kauli ambayo inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu “Amka… na Kristo atakuangaza.” Hii ni sehemu ya Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso 5:14. Mkutano unafungwa rasmi Jumapili tarehe 18 Julai 2021. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Shirika, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia wajumbe ujumbe na matashi mema akikazia kwa namna ya pekee kabisa: madhara ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Umuhimu wa kupyaisha dira ya Shirika lao; Roho Mtakatifu ni nguvu ya Mungu inayochochea mabadiliko ya kweli katika maisha ya watawa sanjari na changamoto zake.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kazi na utume uliotekelezwa na Padre Michael Perry ambaye ameliongoza Shirika kwa kipindi cha Miaka sita. Ameonesha moyo mkuu, utu na udugu wa kibinadamu na anamtakia utumishi mwema Padre Giovanni Fusarelli, bila kuwasahau wanashirika wote walionea sehemu mbalimbali za dunia! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anasema, maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamepelekea madhara makubwa kwa watu wengi, kiasi cha kuishi katika hali ya hatari, karantini pamoja na mateso yake. Changamoto na mahangaiko yote haya, yawakumbushe binadamu wote kwamba, hapa duniani ni wapita njia na wala hawana makazi ya kudumu! Kumbe, hawana budi kuachana na mambo yanayowaelemea na kuanza kukumbatia na kuambata mambo msingi katika maisha. Hiki ni kipindi muafaka cha kujikita katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu; wito na mwaliko wa kuwa ni mashuhuda wa uwepo wa kinabii kati pamoja na watu wa Mungu; kwa kuishi katika umoja na udugu wa kibinadamu pasi na makuu. Watawa wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili.

Katika kipindi cha maambukizi makubwa ya UVIKO-19, Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu kwa kuwawezesha Wanashirika hawa kuadhimisha Mkutano mkuu, huku wakiongozwa na kauli mbiu “Amka… na Kristo atakuangaza.” Ef 5:14. Haya ni maneno yanayogusa Ufufuko ambao unakita mizizi yake katika Fumbo la Pasaka. Hakuna upyaisho wa maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji bila ya Kristo Yesu Mfufuka! Huu ni wakati wa kusoma alama za nyakati, kwa kutambua kazi ya Mungu, kugundua amana na utajiri wa karama ya Shirika sanjari na utambulisho wao kama Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu anawataka Watawa hawa kupyaisha dira ya maisha na utume wao kama ilivyojitokeza kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi katika ujana wake, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa ajili ya huduma kwa maskini.

Hivi ndivyo alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyekuwa kijana tajiri na jeuri, akaishia kuwahudumia wakoma wa mji wa Assisi. Kiini cha karama na tasaufi yao ni huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu! Huruma ya Mungu ilimletea Mtakatifu Francisko wa Assisi toba na wongofu wa ndani, akaacha yote kwa ajili ya huduma kwa maskini. Huu ni mwaliko kwa wanashirika kuwatafakari maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii kama Sakramenti ya uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na waja wake. Waguswe na kupyaishwa kutoka katika undani wao na madonda ya maskini katika ulimwengu mamboleo. Watambue kwamba, wao ni Ndugu wadogo wa Mtakatifu Francisko, jina ambalo alilichagua kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya Wanashirika wake.

Roho Mtakatifu ni nguvu ya Mungu wanayohitaji ili kuwaletea mageuzi makubwa katika maisha, kiasi cha kujivika fadhila ya unyenyekevu, tayari kukutana na wakoma kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Maskini ni chachu ya mabadiliko ya ndani, ikiwa kama watawaruhusu kuwagusa kutoka katika undani wa maisha yao. Huu ni mwaliko wa kutoka na kuwaendelea maskini wanaoteseka: kiroho na kimwili, ili kushuhudia uwepo wao mwanana unaosimikwa katika utu na udugu wa kibinadamu. Ni wakati wa kujifunga kibwebwe kumwendea ili kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama. Leo hii kuna kuna matumizi mabaya ya mali na rasilimali za dunia; watu wachache wanaendelea kutajirika wakati ambapo kundi la “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi” linazidi kuongezeka kila kukicha!

Baba Mtakatifu anawataka Ndugu wadogo wa Mtakatifu Francisko kuwa ni watu wa majadiliano katika ukweli na uwazi; wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu. Waendelee kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho; chemchemi ya matumaini na ukweli; tunu msingi za Kiinjili. Wawe tayari kupambana na changamoto za maisha ya kitawa na hasa kutokana na kupungua kwa miito ya kitawa pamoja na watawa wengi kuendelea kuzeeka. Changamoto hii wanaweza kuikabili kwa kuzama zaidi katika maisha ya sala, udugu wa kibinadamu; ufukara, unyenyekevu katika udogo pamoja na kutambua kwamba, hapa duniani wao ni mahujaji!

Upyaisho wa dira yao, uwawezeshe kutambua uwepo wa Mungu na umuhimu wao wa kuwapokea na kuwakirimia maskini, waathirika wa mifumo ya utumwa mamboleo; wakimbizi, wahamiaji pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maskini wawe ni shule na walimu katika maisha na utume wao; wawapokee na kuwakumbatia kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Wafrancisko kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili; watu wanaosimika maisha yao katika mshikamano na udugu wa kibinadamu; tayari kupandikiza mbegu ya matumaini na Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia.

Papa Ndugu Wadogo

 

17 July 2021, 14:57