Vatican News

Papa Francisko Umuhimu wa Faragha na Huruma ya Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana amekazia umuhimu wa watu wa Mungu kujipatia faragha na kujipumzisha. Wazo la pili ni huruma inayobubujika kutoka katika tafakuri ya kina. Ni fursa ya kukuza na kudumisha ikolojia ya moyo inayokita mizizi yake katika mapumziko, tafakuri na huruma ili kujenga na kudumisha mahusiano ya karibu na Mwenyezi Mungu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Katika Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 16 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Mwinjili Marko kwa namna ya pekee, anapenda kukazia mambo makuu mawili; umuhimu wa wanafunzi wa Kristo Yesu kupata faragha na kupumzika. Pili, ni huruma ya Kristo Yesu kwa umati mkubwa wa watu kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji! Rej. Mk 6:30-34. Mwenyezi Mungu baada ya kukamilisha kazi yake ya uumbaji alijipatia siku ya mapumziko, changamoto kwa binadamu kufurahia siku za likizo na mapumziko ili kupata nafasi ya kutafakari na kujiwekea sera na mikakati kwa siku za usoni. Lakini kutokana na uchu wa mali na faida ya haraka haraka, leo hii binadamu amegeuzwa kuwa ni mtumwa wa kazi na wala hana hata wakati wa kujipumzisha. Ikumbukwe kwamba, Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe, inapaswa kuwa na uhusiano na sehemu nyingine za maisha ya binadamu. Likizo iwe ni fursa ya kuendeleza utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha. Kiwe ni kipindi cha kupyaisha na kunogesha maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili!

Likizo ni nafasi muafaka ya kujenga, kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha. Ni nafasi ya kutafakari kuhusu Fumbo la maisha ya binadamu, ili kubainisha ikiwa kama maisha yana alama na chapa ya uwepo endelevu wa Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza waja wake katika mapito ya maisha. Likizo ni kipindi cha kukuza, kujenga na kudumisha urafiki; umoja na mafungamano ya kifamilia, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Wanafamilia watambue kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha katika maisha na vipaumbele vyao, tayari kumfuasa Kristo Yesu bila woga! Waamini wajifunze kutoka kwa Bikira Maria, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia

Likizo ni muda muafaka wa kukaa pamoja na wanafamilia wote pale inapowezekana, ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Likizo ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwafunda na kuwapyaisha katika maisha yao ya ndoa na familia. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Likizo si wakati wa kumtundika Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu kwani hii, ni hatari kubwa sana!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 18 Julai 2021 amekazia umuhimu wa watu wa Mungu kujipatia faragha na kujipumzisha. Kwa bahati mbaya watu wanajisahau na kujiachia kushikwa na fadhaa ya kufanya mambo kama “wanaharakati”, ambapo jambo la msingi zaidi ni matokeo wanayopata na hisia kwamba, wao ni wahusika wakuu. Hali kama hii inaweza kujitokeza hata katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kujishughulisha na mambo mengi kiasi hata cha kumsahau Kristo Yesu. Ndiyo maana Kristo Yesu katika Injili ya leo anawaalika wafuasi wake kujitenga, kujipatia faragha na kupumzika pamoja naye! Kwa hakika walihitaji mapumziko ya mwili, faraja, amani na utulivu wa roho. Kristo Yesu alitaka wafuasi wake wapumzike barabara kwa kuzama katika mambo msingi ya maisha. Waweze kujipatia ukimya, wasali na hivyo kujenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Huu ni wakati wa kuangaliana machoni, wa kuzima simu, kujenga na kudumisha ukimya mtakatifu, ili kutafakari matendo makuu ya Mungu na hivyo kuendeleza majadiliano na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazo la pili ni huruma inayobubujika kutoka katika tafakuri ya kina. Ni fursa ya kukuza na kudumisha ikolojia ya moyo inayokita mizizi yake katika mapumziko, tafakuri na huruma. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma wa Wakristo unapaswa pia kuenenda. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele.

Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kwa furaha.

Papa Likizo na Huruma
18 July 2021, 14:55

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >