Papa Francisko asikitishwa na vifo vya watu 92 na majeruhi zaidi ya 100 waliofikwa na janga hili tarehe 12 Julai 2021 wakati Hospitali ya wagonjwa wa UVIKO-19 ilipoteketea kwa moto! Papa Francisko asikitishwa na vifo vya watu 92 na majeruhi zaidi ya 100 waliofikwa na janga hili tarehe 12 Julai 2021 wakati Hospitali ya wagonjwa wa UVIKO-19 ilipoteketea kwa moto! 

Papa Francisko Asikitishwa na Janga la Moto Nassiriya, Iraq

Janga la moto lililotokea Jumatatu tarehe 12 Julai 2021 kwenye Hospitali ya “Imam Al Hussein” iliyoko mjini Nassiriya, Kusini mwa Iraq. Janga hili limesababisha watu 92 kufariki dunia na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa vibaya. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, hii ni hospitali iliyotengwa maalum kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na taarifa za janga la moto lililotokea Jumatatu tarehe 12 Julai 2021 kwenye Hospitali ya “Imam Al Hussein” iliyoko mjini Nassiriya, Kusini mwa Iraq. Janga hili limesababisha watu 92 kufariki dunia na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa vibaya. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, hii ni hospitali iliyotengwa maalum kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hii ni ajali ya pili kutokea katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita na kwamba, haya ni matokeo ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Mitja Leskovar, Balozi wa Vatican nchini Iraq, anawaombea marehemu wote pumziko la milele na faraja kwa wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika janga hili la moto. Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa hospitalini. Anawaombea heri na baraka, faraja, nguvu na amani ya ndani wanapoendelea kutoka huduma kwa wagonjwa.

Wachunguzi wa mambo wanasema, Hospitali hii haikuwa na vifaa vya kuzuia wala kupambana na janga la moto kama lilivyotokea, kwa kisingizio cha ukata kutoka kwa wahusika wakuu. Itakumbukwa kwamba, Mwezi Aprili 2021 mlipuko kama huu ulitokea huko Baghdad katika Hospitali maalum kwa ajili ya waathirika wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na kusababisha watu 82 kufariki dunia na wengine 110 kujeruhiwa vibaya. Mapungufu makubwa yanayojitokeza katika mfumo wa huduma ya afya ni matokeo makubwa ya vikwazo vya kiuchumi na madhara ya vita ya muda mrefu chini Iraq. Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Iraq Bwana Mustafa Al Kadhimi amewasimamisha kazi wafanyakazi na walinzi wa Hospitali hii na wengine wametiwa nguvuni, ili kujibu tuhuma zinazo wakabili. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 hadi kufikia Jumatano asubuhi tarehe 14 Julai 2021 watu zaidi ya 17,630 walikuwa wamekwisha kufariki dunia. Watu 1,447,557 walikuwa wameambukizwa ugonjwa wa UVIKO-19 nchini Iraq na wale waliopona ni 1,320,260.

Ajali ya Moto Iraq
14 July 2021, 14:58