Papa Francisko anaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti kuwataka wadau wote katika mgogoro huu kuweka chini silaha na kuanza mchakato wa majadiliano. Papa Francisko anaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti kuwataka wadau wote katika mgogoro huu kuweka chini silaha na kuanza mchakato wa majadiliano. 

Mshikamano wa Papa Francisko na Wananchi wa Haiti: Amani na Umoja

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti CEH, kuwataka wadau wote kuweka silaha chini na kuanza kujikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ni matumaini yake kwamba, hali tete ya vurugu na ghasia itakoma na wananchi wa Haiti wataanza safari ya kuelekea kwenye amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kutoka kwenye Hospitali ya Gemelli iliyoko mjini Roma, Jumapili tarehe 11 Julai 2021 aliyaelekeza mawazo yake nchini Haiti. Anasema, katika siku za hivi karibuni, mara nyingi sala zake amezielekeza zaidi kwa watu wa Mungu nchini Haiti na hasa baada ya mauaji ya kikatili ya Rais Jovenel Moïse na hatimaye mkewe, Martine Moïse aliyeponea chupuchupu kufariki dunia baada ya kupata majeraha makubwa mwilini mwake usiku wa kuamkia Jumatano tarehe 7 Julai 2021. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapenda kuungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti CEH, kuwataka wadau wote kuweka silaha chini na kuanza kujikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Haiti kwamba, yuko karibu nao. Ni matumaini yake kwamba, hali tete ya vurugu na ghasia itakoma na wananchi wa Haiti wataanza safari ya kuelekea kwenye amani na utulivu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti, CEH, linasema, ghasia haziwezi kuwa ni suluhu ya kumaliza ghasia na changamoto zinazowakabili wananchi wa Haiti. Jambo la msingi katika hali hii tete ni kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Haiti. Huu ni wakati wa kuvunjilia mbali uchu wa mali na madaraka na masilahi ya mtu binafsi na kuanza kujikita katika kutafuta suluhu ya kudumu, kwa kuzingatia upendo, amani na tunu msingi zinazowaunganisha watu wa Mungu nchini Haiti. Ni muda wa kuweka silaha chini ili kuondokana na utamaduni wa kifo na kuanza kujichimbia katika Injili ya uhai, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu nchini Haiti. Usiue ni Amri ya Mungu!

Rais Jovenel Moïse aliapishwa na kushika madaraka tarehe 7 Februari 2017. Hata kabla ya mauaji ya Rais Jovenel Moïse, Haiti imekuwa ikikabiliwa na kiwango kikubwa cha rushwa; ufisadi, ghasia, vitisho pamoja na kiwango cha juu kabisa cha umaskini. Mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma ni mkubwa mno kiasi cha wananchi wa kawaida kushindwa kumudu gharama hizi. Mambo haya yaliwalazimisha wananchi wa Haiti kuingia barabarani kupinga Serikali ya Rais Jovenel Moïse. Kabla ya kifo chake, Rais Jovenel Moïse alikuwa amemteuwa Bwana Ariel Henry kuwa Waziri mkuu wakati huo huo Bwana Claude Joseph anadai kwamba, ndiye Waziri mkuu halali wa Haiti kwa wakati huu. Hoja hii inaungwa mkono na viongozi wakuu wa Umoja wa Mataifa.

Hadi sasa watu 17 wamekwisha kutiwa mbaroni kuhusiana na mauaji ya Rais wa Haiti. Serikali ya Marekani inasema, itaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Haiti ili kuimarisha demokrasia, utawala wa sheria, amani na usalama. Itakumbukwa kwamba, Haiti kunako mwaka 2010 ilikumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha watu 220,000 kupoteza maisha. Watu zaidi ya milioni 1.5 wakakosa mahali pa kuishi na wengine 300, 000 wakapata majeraha na ulemavu wa kudumu. Haiti katika siku za hivi karibuni imekumbwa na machafuko ya kisiasa kutokana na uchu wa mali na madaraka.

Papa Haiti

 

 

12 July 2021, 14:55