Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna Wazazi wake Bikira Maria: Injili ya familia na shule ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia! Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna Wazazi wake Bikira Maria: Injili ya familia na shule ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia! 

Watakatifu Joakim na Anna Wazazi wa Bikira Maria: Injili ya Familia

Ibada na heshima kwa watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria ni mwendelezo wa Ibada kwa Bikira Maria na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Matukio yote haya yanapaswa kuangaliwa katika mwanga wa Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia.” ili kuboresha sera na mikakati ya tunu msingi za familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai. Hii ndiyo familia ambamo Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa amechota fadhila mbalimbali zilizomwezesha kupata upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kumbe, Ibada na heshima kwa watakatifu Joakim na Anna ni mwendelezo wa Ibada kwa Bikira Maria na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Matukio yote haya yanapaswa kuangaliwa katika mwanga wa Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni muda muafaka wa kuanza kuvuna matunda yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano katika medani mbalimbali za maisha: kikanisa na kijamii. Ni nafasi muafaka ya kutafakari changamoto, fursa na matatizo yaliyopo na kuendelea kuyafanyia kazi na hatimaye, kuyapatia majibu muafaka kwa mwanga wa tunu msingi za Kiinjili. Changamoto ya kwanza ni kuubali na kuupokea Wosia ambao umesheheni maneno ya ujasiri, chachu ya mabadiliko na upyaisho wa maisha na utume wa ndoa na familia sanjari na mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi na watu wa Mungu.

Kimsingi, familia zinahitaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, zitakazowawezesha wanandoa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia katika ujumla wake. Familia inapaswa kusimikwa katika upendo wenye huruma, kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linayotangaza na kushuhudia uwepo mwanana wa Mwana wa Mungu. Katika shida na magumu, familia zisaidiwe kwa hali na mali, ili kuweza kupita vipindi hivi vigumu kwa kusindikizwa na upendo wenye huruma. Familia zinazoogelea kwenye shida na ugumu wa maisha zisikilizwe na zisaidiwe. Wazazi na walezi wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani miongoni mwa watoto wao. Wazazi na walezi warithishe imani hii kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha yao.

Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani, wazazi wawasaidie watoto wao kutambua na kuthamini zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, ni mwendelezo wa maadhimisho ya Siku ya Wazee na Wajukuu duniani, iliyoadhimishwa kwa mara ya kwanza na Mama Kanisa, Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Wazee ni sehemu muhimu sana kwa jamii yoyote ile. Uzoefu na busara za wazee ni kiungo na hamasa kwa maisha ya wanajamii. Pamoja na changamoto mbalimbali za maisha ya uzeeni bado wazee wana nafasi na mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii. Wazee ni alama ya utimilifu wa maisha ya mtu na jamii katika ujumla wake. Wazee ni walezi kwa watoto na vijana. Wazee ni: urithi, amana na utajiri kwa jamii kwani uzoefu na busara zao ni ushuhuda wa kinabii kwa siku za usoni.

Vijana wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanatenda tendo jema la huruma na mapendo kwa wazee wanaowazunguka. Upendeleo wa pekee utolewe kwa wazee wanaoishi peke yao au kwenye nyumba za kutunzia wazee, ambao kwa muda mrefu uliopita hawajapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki zao. Vijana watambue na kuthamini nafasi na dhamana ya wazee katika jamii na kamwe wasiwaache kuelemewa na upweke hasi unaoweza kuwafanya wachungulie kaburi mapema pengine hata kabla ya wakati. Vijana wahakikishe kwamba, wanatumia uzoefu na mang’amuzi yao ili kuwaonjesha upendo kwa njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii pale inaposhindikana kuwatembelea mubashara! Vijana watenge muda wa kuweza kuwasikiliza kwa dhati na pale ambapo inawezekana kwa kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, wawatembelee ili kuwajulia hali.

Baba Mtakatifu Francisco anasema, Bwana Luis Bernárdez, Mshairi maarufu kutoka Argentina aliwahi kusema, mti ambao mizizi yake imeng’olewa, hautaweza kukua, kuchanua na hata kutoa matunda. Ni katika mantiki hii, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwapongeza wazee kwa uwepo na ushiriki wao katika maisha na utume wa jamii. Upendo ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu utaweza kukua na kuzaa matunda. Hakuna familia inayoweza kukua na kustawi, ikiwa kama inasahau mizizi yake, yaani asili yake. Watoto na vijana wajifunze kutoka kwa wazee, ili hatimaye, mizizi yao iweze kuzama zaidi katika maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB., linasema wazazi wake Bikira Maria, wanaonesha umuhimu wa familia kama shule ya upendo, imani na utakatifu wa maisha. Kumbukumbu hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwani ni fursa ya kuwashukuru na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Brazil. Hawa ni mashuhuda amini wa imani. Matukio kama haya ni fursa ya kukuza na kudumisha ndani ya nyoyo za watu: faraja, upendo, huruma, imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu aliye asili ya wema na utakatifu wa maisha. Maadhimisho haya yanayoendelea yanachukua nafasi ya pekee sana kwa wazee ambao wamekumbwa, wameguswa na kutikiswa sana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wazee wengi nchini Brazil wamefariki dunia katika hali ya majonzi mazito na upweke. Wazee wanahitaji faraja, upendo na mshikamano wa dhati katika hija ya maisha yao hapa duniani!

Watakatifu Joakim na Anna
25 July 2021, 15:37