Papa Francisko anatarajia kufanya hija ya kichungaji nchini Slovakia wakati wa maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. Papa Francisko anatarajia kufanya hija ya kichungaji nchini Slovakia wakati wa maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. 

Kongamano la 52 La Ekaristi Kimataifa Sept. 2021: Slovakia!

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Slovakia ili kuitembelea nchi yao. Katika hija hii ya kitume, Papa anatarajia kutembelea na kuzungumza na watu wa Mungu katika miji ya: Bratislava, Prešov, Košice na Šaštin. Ratiba rasmi inatarajiwa kutolewa hivi karibuni. Papa atashiriki pia Kongamano la 52 la Ekaristi Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya upendo kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni shule ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa mwamini anayeshiriki Ekaristi Takatifu, hawezi kuwageuzia kisogo maskini na wale wote wanaopekenywa na baa la njaa duniani. Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) yatayaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 ametangaza kwamba, Mwenyezi Mungu akipenda, atashiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa.  Baadaye, atafanya hija ya kitume nchini Slovakia, kuanzia tarehe 12 Septemba 2021.

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Slovakia ili kuitembelea nchi yao. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutembelea na kuzungumza na watu wa Mungu katika miji ya:  Bratislava, Prešov, Košice na Šaštin. Ratiba rasmi ya hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia, inatarajiwa kutolewa hivi karibuni. Baba Mtakatifu kuanzia sasa, anawashukuru wale wote wanaoendelea kuchakarika usiku na mchana ili kufanikisha maadhimisho haya.  Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza kwa sala na sadaka zao kama sehemu ya maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu sanjari na hija yake ya kitume nchini Slovakia.

Itakumbukwa kwamba, Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Ni Fumbo ambalo lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za waamini.

Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Hili ni Fumbo kubwa linalopaswa kuadhimishwa vyema; Kuabudiwa na Kutafakariwa kikamilifu. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Kaa Nasi Bwana”: “Mane, Nobiscum Domine”, anawaalika waamini kujenga utambuzi hai wa uwepo halisi wa Kristo Yesu, katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu na katika Ibada nje ya Misa.

Papa Slovakia
04 July 2021, 15:28