Hayati Kardinali Albert Vanhoye, S.I alikuwa ni Gwiji wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Hayati Kardinali Albert Vanhoye, S.I alikuwa ni Gwiji wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu. 

Kardinali A. Vanhoye, SJ. Gwiji la Sayansi ya Maandiko Matakatifu

Kardinali Albert Vanhoye alikuwa ni Gwiji na Jaalimu wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Akabahatika kuteuliwa kuwa ni Gambera wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi ya Maandiko Matakatifu, Biblicum. Alishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mjini Vatican! Kardinalii Vanhoye alikuwa mhubiri safi “kiasi kwamba, hata wasela wa kijiweni walizikubali nondo zake za uhakika.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Maandiko Matakatifu yanasema kwamba, imani inapata chimbuko lake kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kiasi kwamba, Biblia inapaswa kuwa ni Maktaba ya kwanza kabisa kuwamo ndani ya Familia ya Kikristo, ili familia hizi ziweze kuonja uwepo fungamani na endelevu wa Kristo Yesu mkombozi wa dunia katika maisha na vipaumbele vyao. Kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia kuna maanisha mchakato wa kurithisha imani inayofumbatwa katika ukimya wa Mwenyezi Mungu aliyefunuliwa na Kristo Yesu.  Mapokeo ya Mama Kanisa yanaonesha kwamba, usomaji, tafakari na umwilishaji wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia ni kati ya vipaumbele vya shughuli na mikakati ya kichungaji iliyotolewa na Mababa wa Kanisa. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, umeliwezesha Kanisa kuwarudishia tena waamini Biblia mikononi mwao, ili Neno la Mungu liweze kuwa ni dira na mwanga katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza waamini kujitaabisha: kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, wakianzia kwenye Familia, Jumuiya ndogondogo za Kikristo pamoja na vyama vya kitume katika ngazi mbalimbali!

Utangulizi huu ni kwa heshima ya Kardinali Albert Vanhoye, SJ., Gwiji wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu, Gambera wa zamani wa Taasisi ya Sayansi ya Maandiko Matakatifu, Biblicum;  na Katibu Mstaafu wa Tume ya Kipapa ya Biblia aliyefariki dunia tarehe 29 Julai 2021 akiwa na umri wa miaka 98. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumamosi tarehe 31Julai 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Kardinali Albert Vanhoye, SJ. Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambirambi alizomtumia Padre Manuel Morujao, SJ, Mkuu wa Nyumba ya “San Pietro Canisio, Roma anasema, amesikitishwa na taarifa za msiba wa Kardinali Albert Vanhoye, SJ. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa salam za rambirambi na uwepo wake wa karibu kwa wale wote walioguswa na msiba huu mzito! Anawakumbuka Wayesuit, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wale wote waliobahatika kumfahamu.

Hayati Kardinali Albert Vanhoye alikuwa ni kiongozi aliyemtumikia Mwenyezi Mungu pamoja na Kanisa lake kwa ari, moyo mkuu na majitoleo mazito. Kwa hakika, alikuwa ni kati ya watoto wapendwa wa maisha ya kiroho wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, Kardinali Albert Vanhoye alikuwa  ni Gwiji na Jaalimu wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Akabahatika kuteuliwa kuwa ni Gambera wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi ya Maandiko Matakatifu, Biblicum. Alishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mjini Vatican! Kardinali Albert Vanhoye alibahatika kuwa na kipaji cha kuhubiri vizuri sana “kiasi kwamba, hata wasela wa kijiweni walizikubali nondo zake za uhakika.” Huu ni utume ambao aliutekeleza kwa moyo wa upendo hali akitaka kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linafahamika na kupendwa na wengi, ili liweze kuwa ni dira na mwongozo sahihi wa maisha na vipaumbele vya waamini.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii kumkumbuka na kumwombea Hayati Kardinali Albert Vanhoye, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo na kwa maombezi ya Bikira Maria, aweze kumpokea miongoni mwa wateule wake huko mbinguni! Hatimaye, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wale wote wanaosikitika kutokana na msiba huu mzito, lakini kwa namna ya pekee wale ambao wamemtunza na kumsindikiza katika safari yake ya mwisho hapa duniani! Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, katika mahubiri yake amesema Hayati Kardinali Albert Vanhoye amebahatika kutimiza miaka 98 tangu alipozaliwa. Akamtumikia Mungu na Kanisa kama Padre kwa miaka 67 na kama Kardinali kwa miaka 15. Alikuwa ni kiongozi aliyejitambulisha na Kanisa kwa ajili ya Kanisa “Sentire cum Ecclesia.” Kwa hakika alikuwa ni Gwiji wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu hususan kuhusu huruma na upendo wa Mungu. Aliadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa ibada na uchaji mkuu wa Mungu, kama chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Albert Vanhoye alizaliwa tarehe 24 Julai 1923 huko Hazebrouck, Jimbo Katoliki la Lille, Kaskazini mwa Ufaransa. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa katika Shirika la Wayesuit, tarehe 15 Novemba 1944 aliweka nadhiri zake za muda na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 26 Julai 1954. Alijipatia Shahada ya Uzamivu katika Maandiko Matakatifu kunako mwaka 1961. Tangu mwaka 1959 hadi mwaka 1993 amekuwa akifundisha Sayansi ya Maandiko Matakatifu. Ni mwandishi mashuhuri wa vitabu na Makala ya kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 22 Februari 2006 alitia nia ya kumtangaza Padre Albert Vanhoye kuwa Kardinali kwani Mama Kanisa alikuwa anatambua mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa. Ni Padre aliyeonesha uaminifu na udumifu katika maisha na utume wake. Tarehe 24 Machi 2006 akamtangaza na kumsimika kuwa ni Kardinali.

Fumbo la Kifo
31 July 2021, 15:53