Papa Francisko kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Slovakia. Papa Francisko kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 anafanya hija ya kitume nchini Slovakia. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Slovakia 12-15 Septemba 2021

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Kwa hakika Familia Takatifu ilionesha upendo wa dhati kabisa kwa Yesu. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu ni watakatifu wasimamizi wa Slovakia. Bikira Maria wa Mateso saba, anaheshimiwa sana nchini Slovakia. Imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) yatayaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu Francisko anategemea kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa.  Baadaye, atafanya hija ya kitume nchini Slovakia, kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Slovakia ili kuitembelea nchi yao. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutembelea na kuzungumza na watu wa Mungu katika miji ya: Bratislava, Prešov, Košice na Šaštin. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia inanogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Kwa hakika Familia Takatifu ilionesha upendo wa dhati kabisa kwa Kristo Yesu katika maisha yake.

Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu ni watakatifu wasimamizi wa Slovakia. Bikira Maria wa Mateso saba, anaheshimiwa sana nchini Slovakia. Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia linasema kwamba, kwa hakika, Bikira Maria alimpenda sana Mwanaye wa pekee tangu alipopashwa habari ya kutungwa kwake mimba, akamsindikiza katika safari ya maisha na utume wake. Wakati wa raha kama ilivyokuwa kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya. “Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai… Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.” Yn 2:3-11. Bikira Maria alimfuata Mwanaye Mpendwa hata akadiri kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye mpendwa!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu. Anasema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. Baba Mtakatifu Francisko anafanya Hija ya Kitume nchini Slovakia, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Mwaliko kwa waamini kumtazama Mtakatifu Yosefu, tayari kukaza mwendo kumwelekea Kristo Yesu.

Ni matumaini makubwa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia kwamba, Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia itasaidia kupyaisha na kuimarisha imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kufuata nyayo zake katika huduma kwa watu wa Mungu. “Kama vile, Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” Mt 20: 28. Historia inaonesha kwamba, mara ya mwisho Slovakia kutembelewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, imekwisha gota miaka 18 na tangu wakati huo, kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana. Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujiandaa kiroho zaidi kama sehemu ya maandalizi ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021.

Slovakia ni nchi ambayo imekita mizizi yake katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni nchi ambayo imebahatika kuwa na jeshi kubwa la watakatifu, waungama dini na wamisionari wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa Katoliki nchini Slovakia, linaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini humo. Kwa namna ya pekee kabisa, tarehe 15 Septemba 2021 Mama Kanisa ataadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria, Mama wa Mateso saba. Kwa mara ya kwanza, kumbukumbu hii kitaifa, itaadhimishwa kwa uwepo pia wa Baba Mtakatifu Francisko. Leo hii, Bikira Maria anawaonesha huruma wale wote wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini sanjari na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na wakuu wa ulimwengu huu. Bikira Maria Mama wa Mateso awe ni faraja kwa wale wanaoteseka; matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo na awe ni chemchemi ya huruma na mapendo kwa wenye huzuni na mahangaiko makubwa!

Baba Mtakatifu Francisko anakwenda nchini Slovakia kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo thabiti. Rej. Lk 22:32. Ni hija inayobeba matumaini na changamoto za maisha. Iwe ni hija ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia kama sehemu ya maandalizi ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao, linapenda kujielekeza katika maeneo makuu matatu: Kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa. Pili, ni kwa ajili ya Kanisa nchini Slovakia kama kielelezo cha uwajibikaji. Tatu ni kwa ajili ya walimwengu wote kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa Kiinjili.

Slovakia

 

 

22 July 2021, 14:59