Papa Francisko tarehe 28 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa Patriaki Batholomeo wa kwanza wa Costantinopol kama sehemu ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume. Papa Francisko tarehe 28 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa Patriaki Batholomeo wa kwanza wa Costantinopol kama sehemu ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume. 

Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa Kwanza: Ushuhuda wa Umoja

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amegusia madhara makubwa ambayo yamesababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Upendo katika maisha ya Wakristo, Mchakato wa Umoja Kamili miongoni mwa Wakristo unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Waongozwe na kudumishwa katika upendo kama ulivyotangazwa na kushuhudiwa na Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa hija ya maisha ya watu kila siku! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 28 Juni 2021 amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Ujumbe huu kwa mwaka 2021 katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume tarehe 29 Juni 2021, unaongozwa na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amegusia madhara makubwa ambayo yamesababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Upendo katika maisha ya Wakristo, Mchakato wa Umoja Kamili miongoni mwa Wakristo unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Baba Mtakatifu anasema, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Wakatifu Petro na Paulo, Mitume, tarehe 29 Juni ya kila Mwaka wakati huu ambapo walimwengu wanajikongoja kujikwamua kutoka katika madhara ambayo yamesababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambao umewagusa na kuwatikisa watu wote katika ujumla wao. Jambo la msingi ni kwa watu wa Mataifa kujifunza kwa dhati na katika hali ya unyenyekevu kuhusu madhara ya janga hili, ili kuanza upya kwa ari na moyo mkuu. Ni muda muafaka wa kuondokana na mambo ambayo watu wengi waliyategemea kama kinga na usalama wa maisha yao, mazoea na taratibu za maisha; miradi na tabia ya kutafuta na kukumbatia mali na madaraka kwa ajili ya mafao binafsi. Hii ni tabia ambayo iliwaacha watu wengi nje ya huduma ya maendeleo na bila hata kujishughulisha kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Watu wengi walishindwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na Maskini. Huu ni wito na changamoto hata kwa Wakristo kufanya tafakari ya kina, kuamua kutenganisha chema na kibaya; kwa kufanya manga’amuzi ya kina, ili hatimaye kujikita katika mambo msingi na yale yanayopita, kuacha yapite salama salimini.

Mtakatifu Paulo, Mtume wa Mataifa anasema, “Upendo haupungui neno wakati wote; bali ukiwapo unabii utabatilika, zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika” I Kor 13:8. Upendo unaobainishwa hapa si ule wa mtu kujisikia, bali ni ule upendo uliotolewa na kushuhudiwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Huu ni upendo wa mtu kuyasadaka maisha yake kama mbegu inayopandikizwa ardhini, tayari kufa na hatimaye kuchipuka na kutoa matunda yanayokusudiwa. Huu ni upendo halisi; hautafuti mambo yake; huvumilia, huamini, hutumaini na hustahimili yote. Kwa maneno mengine, Injili ya Kristo inawahakikishia waja wake matunda mengi, wale wote watakaowashirikisha wengine, kwa kuwekeza katika huduma ya upendo inayotekelezwa kwa kujikita katika sadaka na unyenyekevu.

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kuhakikisha kwamba, wanalipatia uzito stahiki janga la Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19, bila kujitafuta wenyewe na wala bila kugubikwa na ubinafsi, bali kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wakristo watambue na kuheshimu tofauti zao msingi sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo na maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kubomolea mbali maamuzi mbele, chuki na uhasama visivyo na mvuto wala mashiko. Yote haya yanapaswa kuelekezwa katika majadiliano yanayokita mizizi yake katika upendo ili kujenga na kudumisha: umoja, mahusiano na mafungamano mema na Makanisa yote ya Kikristo. Huu ni wito wa kutembea, kushikamana na kuwajibikiana kwa pamoja. Yote haya yanawezekana ikiwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu pamoja na upendo mbunifu wa Mungu na amani, vitamwilishwa katika tofauti msingi; hapo kutaonekana njia mpya kwa ajili ya udugu uliopyaishwa!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, ushuhuda unaokita mizizi yake katika umoja wa Wakristo unaokuwa na kupanuka siku kwa siku ni alama ya matumaini kwa watu wengi, wanaojisikia kutiwa moyo ili kuendeleza udugu wa kibinadamu na upatanisho ili kurekebisha mapungufu yote yaliyokitokeza katika historia na maisha ya Kanisa. Hii ni njia inayoelekea katika amani. Itakuwa ni alama ya kinabii, ikiwa kama waamini wa Kanisa la Kiorthodox watashirikiana kwa dhati kabisa na waamini wa Kanisa Katoliki katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na waamini wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru kwa uwepo wao na amewaomba wafikishe salam na matashi mema kwa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kumwalika rasmi, ili kuja Roma, ili kwa pamoja waweze kumwimbia Mwenyezi utenzi wa sifa na shukrani anaposherehekea Miaka 30 tangu alipochaguliwa kuwaongoza watu wa Mungu. Kwa maombezi ya Watakatifu: Petro, Paulo na Andrea Mitume, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwabariki Wakristo na kuwavutia kwenye Umoja wa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Miamba wa Imani
28 June 2021, 13:07