Siku ya Upendo na Mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni tarehe 29 Juni ya Kila mwaka. Siku ya Upendo na Mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni tarehe 29 Juni ya Kila mwaka. 

Siku ya Upendo na Mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro 29 Juni

Kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Kanisa linaungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro kuonesha mshikamano wa udugu wa upendo na ukarimu kwa: kwa njia ya sala na hasa zaidi kwa kuchangia mfuko unaogharimia shughuli mbalimbali za Injili ya upendo zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu sehemu mbali mbali za dunia hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya UVIKO-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Siku ya Upendo na Mshikamano wa Papa ilianzishwa kunako tarehe 8 Agosti 1871 na Papa Pio IX katika Waraka wake wa Kitume “Saepe Venerabilis”.  Na tangu wakati huo, kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Kanisa linaungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro kuonesha mshikamano wa udugu wa upendo na ukarimu kwa: kwa njia ya sala na hasa zaidi kwa kuchangia mfuko unaogharimia shughuli mbalimbali za Injili ya upendo zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu sehemu mbali mbali za dunia hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19: “The Pence of Saint Peter” (L’Obolo di San Pietro). Khalifa wa Mtakatifu Petro anayo dhamana ya kuendeleza: Umoja wa Kanisa; Haki, Amani na Maridhiano Duniani mambo yote haya yanafumbatwa katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Mchango huu unaotolewa na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema unamwezesha Baba Mtakatifu kuwasaidia watu waliokumbwa na majanga pamoja na maafa kama vile: matetemeko ya ardhi, mafuriko, njaa, ukame na vita. Ni msaada unoalenga kumsaidia mtu mzima katika mahataji yake: kiroho na kimwili, kwa kuchangia maboresho katika sekta ya elimu, afya na maendeleo fungamani ya binadamu. Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuwajengea uwezo ili kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu pasi na kukata wala kujikatia tamaa.

“Usiwasahau maskini” ni maneno ambayo Kardinali Claudio Hummes alimwambia Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Maneno haya yakaingia na kunata katika akili na moyo wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye leo hii maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni anawapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake, si kwa maneno tu bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Papa akamchagua Mtakatifu Francisko wa Assis mpenda amani, mazingira na mhudumu wa maskini kuwa msimamizi wake, leo hii mjini Vatican wimbo umebadilika, mwenye macho aambiwi tazama! Hata nawe unaweza kushikamana na Papa kwa kuchangia katika mfuko huu kwa hali na mali. Na kwa njia hii, unashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya kwani maisha na utume wa Kanisa unaendelea kupanuka kila kukicha!

Mshikamano na Papa
29 June 2021, 14:53