Tarehe Mosi Julai 2021 ni Siku ya Sala, Tafakari na Kufunga kwa ajili ya Lebanon. Tarehe Mosi Julai 2021 ni Siku ya Sala, Tafakari na Kufunga kwa ajili ya Lebanon. 

Siku ya Sala ya Tafakari Kwa Ajili ya Lebanon 1 Julai 2021: Amani!

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga naye kwa sala tarehe 1 Julai 2021. Hii ni Siku Maalum ya Sala, Kufunga na Kutafakari Kuhusu Lebanon. Siku hii inaongozwa na kauli mbiu “Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani”. Sote kwa pamoja kwa ajili ya Lebanon. Yer 29: 11. Ni Siku ya Sala ya Kiekumene Kuombea Amani na Utulivu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani, ametumia fursa hii, kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga naye kwa sala tarehe 1 Julai 2021. Hii ni Siku Maalum ya Sala, Kufunga na Kutafakari Kuhusu Lebanon. Siku hii inaongozwa na kauli mbiu “Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani”. Sote kwa pamoja kwa ajili ya Lebanon. Yer 29: 11. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye kwa ajili ya kuombea tukio hili muhimu kwa nchi ya Lebanon. Ratiba inaonesha kwamba, viongozi wa Makanisa kutoka Lebanon watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko; kutakuwepo na muda wa sala kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican; vipindi vitatu vya majadiliano na baadaye jioni kwa pamoja, wataadhimisha Liturujia ya Kiekumene kwa ajili ya kuombea amani nchini Lebanon

Kwa kuzingatia ustawi na maendeleo ya Lebanon na Ulimwengu katika ujumla wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, haiwezekani kabisa kwa Jumuiya ya Kimataifa kufumba macho kiasi kwamba, amana na utajiri wote wa Lebanon upotee na kutoweka katika uso wa dunia. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwahamasisha watu wa Mungu nchini Lebanon kujifunga kibwebwe ili kutafuta nguvu na ari mpya itakayowawezesha kuanza upya kuijenga nchi yao. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa kisiasa na kidini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon, huku wakizingatia ukweli na uwazi katika mchakato mzima wa ukarabati wa nchi yao, kwa sasa na kwa siku za usoni. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa pia kuunga mkono juhudi za Lebanon za kutaka kujiondoa katika kipeo hiki ambacho kimeipekenya nchi hii, kiasi cha wananchi wake kukata tamaa. Kuna hatari kubwa kwa Lebanon kutumbukia katika machafuko ya kisiasa yanayoendelea kujionesha kwenye Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wananchi wa Lebanon wameguswa na kutikiswa sana na mlipuko wa Lebanon ambao umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Huu ni wakati wa kuanza upya kwa ujasiri, ari na moyo mkuu. Katika kipindi hiki kigumu, watu wa Mungu waimarishwe kwa nguvu ya imani na sala, daima wakiendelea kupyaisha ndoto ya nchi yao inayopendeza kwa kujikita katika ustawi na maendeleo fungamani ya wananchi wake. Viongozi wa Kanisa wawe mstari wa mbele kuonesha dira kwa waamini wao; kwa kuwa na ari na mwamko wa shughuli za kitume, kwa kujikita katika ufukara wa Kiinjili unaofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, ili kuwashika mkono, watu wa Mungu wanaoteseka na sasa wanataka kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Watu wa Mungu katika ujumla wao, wawe ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano, tayari kusimama kidete kulinda ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga utamaduni wa watu kukutana; kwa kuishi katika hali ya amani, utulivu na udugu wa kibinadamu; chachu muhimu sana katika mchakato wa upyaisho wa mafao ya wengi. Ni katika hali na mazingira kama haya, wataweza kuwa na uhakika wa mwendelezo wa uwepo wa Ukristo pamoja na mchango wa Lebanon katika Nchi za Kiarabu na Ukanda wa Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Udugu wa kibinadamu ni utambulisho wa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Lebanon.

Sala na Tafakari Lebanon

 

 

30 June 2021, 15:10