Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani na Mashuhuda wa Upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani na Mashuhuda wa Upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake 

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani na Upendo

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani na Mashuhuda wa Upendo wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu wakuu wa Majimbo makuu watapewa Pallio Takatifu watakazovishwa majimboni mwao na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika. Kwa Mwaka 2021 Afrika inawakilishwa na Askofu mkuu Fulgenze Muteba Mugali wa Jimbo kuu la Lubumbashi. Ni Siku ya Kiekumene!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, walioyamimina maisha yao kama sadaka safi na ushuhuda wa upendo na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni.  Baba Mtakatifu Francisko amesema, watakatifu Petro na Paulo, Mitume, walikuwa wamoja, lakini ni watu waliokuwa na taaluma tofauti kabisa. Mtakatifu Petro alikuwa ni mvuvi na muda wake mwingi aliutumia kutengeneza nyavu zake, wakati ambapo Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa Mataifa alikuwa anafundisha kwenye Masinagogi. Katika maisha na utume wao, Petro aliwaendea Wayahudi, wakati ambapo Paulo, alijielekeza zaidi kwa wapagani na watu wa Mataifa ili kuwatangazia na kuwashuhudia Habari Njema ya Wokovu baada ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka! Katika Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko atabariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wa Majimbo makuu walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2020-2021.

Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki. Kinavaliwa pia na Mapatriaki wa Makanisa ya Mashariki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya waamini na Mchungaji wao mkuu, kama Kristo Yesu, anayependa kuwabeba mabegani mwake, ili waendelee kuunganika pamoja naye. Hii ni alama ya umoja wa Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa mwaka 2020-2021, Maaskofu wakuu walioteuliwa ni 12 na kati yao, kuna Askofu mkuu Fulgenze Muteba Mugalu wa Jimbo kuu la Lubumbashi nchini DRC. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Fulgenze Muteba Mugalu alizaliwa tarehe 9 Julai 1962 huko Kongolo, nchini DRC. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 5 Agosti 1990 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 18 Machi 2005 Mtakatifu Yohane Paulo II akatemteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kilwa Kasenga, DRC na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 23 Julai 2005. Tarehe 22 Mei 2021 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lubumbashi, DRC.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, kumekuwepo na utamaduni wa ujenzi wa umoja, ushirikiano na udugu wa kibinadamu na Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol. Makanisa haya mawili yanatambua kwamba, Petro na Andrea walikuwa ni ndugu wamoja. Huu ni ushuhuda wa uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa mwaka 2021 unaongozwa na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia. Anafuatana na Askofu mkuu Iosif Bosch wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina pamoja na Shemasi Barnabas Grigoriadis kutoka kwenye Upatriaki huo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, zawadi ya maisha ya Mtakatifu Petro yameugeuza Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuwa ni uwanja wa matumaini. Kumbe, waamini wanapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema na baraka si kwa ajili ya wakati huo huo, bali neema ya maisha. Mtakatifu Petro aliweza kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Na Kristo Yesu akamwambia “Heri wewe Simoni Bar-yona, kwa maneno mengine ni kusema, heri wewe Petro uliyebahatika kuwa na furaha katika maisha!” Yaani kumtambua Kristo Yesu, kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Kumbe, haitoshi kwa mwamini kufahamu kwamba, Kristo Yesu alikuwa mtu maarufu sana katika historia, aliyetenda miujiza mingi, bali jinsi ambavyo mwamini anamtambua Yesu katika undani wa maisha yake. Ni katika utambuzi huu, Kristo Yesu anampatia Mtakatifu Petro dhamana kwamba, juu ya mwamba huu, atalijenga Kanisa lake. Ni mtu aliyekuwa na imani thabiti na aliyeaminika!

Hata katika dhamana hii, bado Mtakatifu Petro aliendelea kuandamwa na udhaifu wake wa kibinadamu, kiasi cha kufanya makosa, hadi kudiriki kumkana Yesu mara tatu! Mtakatifu Petro, alijitahidi kujenga maisha yake juu ya Kristo Yesu na wala hakujimwambafai kutokana na nguvu zake mwenyewe. Kumbe, Kwa Petro Mtume, Yesu akawa ni mwamba thabiti uliomtegemeza Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuchunguza hali ya maisha yao na hivyo kujiangalia ni wapi ambapo wamejielekeza, wamejiegamisha na kutua nanga ya matumaini yao!

Warumi Juni 29
28 June 2021, 13:29