Papa: Wakati wa Dhoruba za Maisha Mwiteni Yesu Atawaokoa

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa mwamini wa Kristo Yesu na Kanisa haitoshi kuamini kwamba, Mwenyezi Mungu anaishi, lakini mara kwa mara mwamini lazima apige kelele kumwamsha Kristo Yesu katika safari ya maisha yake! Katika hali na mazingira kama haya sala inakuwa ni kilio cha kuomba huruma, msaada na upendo wa Kristo katika maisha. Yesu anataka kushirikishwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mababa wa Kanisa tangu mwanzo kabisa wa tafakari zao, wameliona Kanisa kuwa kama ni Mashua inayosafiri ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kwa kutambua kwamba, Kanisa kimsingi ni Sakramenti ya wokovu. Ndani ya mashua kuna Mitume wenye uzoefu na mang'amuzi ya mapungufu yao ya kibinadamu, wasi wasi na mashaka, lakini kwa pamoja wanajisikia wamoja katika imani wakimzunguka Yesu Kristo. Katika maisha na utume, Kanisa limejikuta lilikabiliana na mawimbi mazito, kiasi hata cha baadhi ya waamini kudhani kwamba, Kristo Yesu, ameuchapa usingizi na kamwe hajali kile kinachoendelea ndani na nje ya Kanisa. Bila kushikamana na kuandamana na Kristo Yesu katika hija ya maisha ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, wafuasi wa Wakristo watajisikia wapweke, waoga na wenye wasiwasi mkubwa. Na kwa nguvu zao wenyewe, hawawezi kufua dafu! Wanapokumbuka kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao, wakimwita anaitikia na kuwaokoa.

Kumbe, hapa jambo la msingi ni kwa waamini kuendelea kukomaa katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Mawimbi mazito ni changamoto, matatizo na fursa mbalimbali zinazoibuliwa katika historia ya maisha na utume wa Mama Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Kanisa lina asili ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa pia lina asili ya kibinadamu kwa sababu Kristo Yesu amelikabihi Kanisa lake chini ya uongozi na usimamizi wa Mitume, ambao wana karama na mapungufu yao ya kibinadamu kama ilivyo hata kwa waandamizi wao! Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 12 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa imenogeshwa na sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Marko 4: 35-41 inayoonesha ukuu, utukufu na mamlaka ya Kristo Yesu dhidi ya dhoruba kuu ya upepo na mawimbi yaliyokuwa yanakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Kristo Yesu alikuwapo katika shetri amelala juu ya mto! Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?” Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?” Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 20 Juni 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameitafakari sehemu hii ya Injili ya Marko kwa kusema kwamba, kuna wakati ambapo waamini wakiwa wamezungukwa na shida na matatizo mengi, wanadiriki kumpigia kelele Kristo Yesu na kumwambia, “Bwana mbona unaendelea kukaa kimya, na wala hata hujishughulishi na mahangaiko yangu? Waswahili wanasema, hapa inaonekana kana kwamba, Mwenyezi Mungu “amekula pini”. Mbaya zaidi ni pale ambapo mwamini anaonekana kuzama kwa sababu upendo au mradi aliokuwa amewekeza matumaini yake, unapoonekana kutoweka kama ndoto ya mchana! Hali hii inatokea pale mawimbi mazito yanapomwandama kutokana na hofu kubwa; pale matatizo yanayopomfika mtu hadi shingoni, bila ya kuwa na matumaini ya usalama au bandari salama. Kuna wakati ambapo mwamini anatindikiwa nguvu na kuanza kunyong’onyea kama mboga ya mlenda kwa kukosa fursa za ajira; kwa kugunduliwa kuwa na maradhi hatari katika maisha au woga kwa wale watu wanaowapenda na kuwathamini.

Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu, waamini wengi wanajikuta wakiwa wamezongwa sana na hofu na woga kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, kiasi hata cha kusahau mambo msingi katika maisha. Mara nyingi Kristo Yesu anawaachia wafuasi wake nafasi ya kumshirikisha katika shida, magumu na mahangaiko yao ya maisha. Kumbe, ni wajibu wa waamini kumkimbilia, kumwita, kumwomba na kuhakikisha kwamba, kwa hakika Kristo Yesu anakuwa ni kiini cha maisha yao ya kila siku. Usingizi wa Yesu ni “janja yake” ili waamini waweze kumwamsha na kumshirikisha katika changamoto za maisha yao. Kwa mwamini wa Kristo Yesu na Kanisa haitoshi kuamini kwamba, Mwenyezi Mungu anaishi, lakini mara kwa mara mwamini lazima apige kelele kumwamsha Kristo Yesu katika safari ya maisha yake! Katika hali na mazingira kama haya sala inakuwa ni kilio cha kuomba huruma, msaada na upendo wa Kristo katika maisha. Baba Mtakatifu anawauliza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, leo hii katika hija ya maisha yao, wanasongwa na dhoruba gani kiasi hata cha kushindwa kusonga mbele? Shida na mahangaiko yote haya, wamwelezee Kristo Yesu kwa sababu anataka waja wake kushikamana na kuandamana naye katika uhalisia wa maisha.

Sehemu ya Injili inasema kwamba, “Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?” Huu kimsingi ni mwanzo wa imani, kwa kutambua kwamba, waamini kwa nguvu zao wenyewe kamwe hawawezi kufua dafu, kwa sababu daima wanahitaji msaada kutoka kwa Kristo Yesu, ili kupata dira na mwelekeo sahihi wa maisha, kama ilivyo pia kwa manahodha baharini. Imani inapata chimbuko lake, pale mwamini anapojiaminisha kwa nguvu na uweza wa Mwenyezi Mungu katika maisha yake, kwa kutambua kwamba, kwa hakika anahitaji uwepo wa Mungu katika maisha yake. Waamini washinde kishawishi cha kutaka kujifungia katika ubinafsi wao na kwa kuwategemea miungu wa uwongo! Waamini wanapomkimbilia na kumlilia Mungu anaweza kuwatendea miujiza katika maisha yao. Hii ni nguvu inayojikita katika fadhila ya unyenyekevu, sala na sadaka inayotenda miujiza! Baada ya Mitume kumwomba Kristo Yesu ili aweze kuwaokoa na dhoruba kuu, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?” Mitume wa Yesu walishikwa na hofu na mahangaiko makuu kwa sababu walikaza macho yao kutaza mawimbi na kumsahau Kristo Yesu aliyekuwa pamoja nao.

Hivi ndivyo inavyotokea kwa wafuasi wa Kristo Yesu, wanapozama na kutopea katika shida na mahangaiko yao binafsi kiasi hata cha kusahau uwepo angavu wa Kristo Yesu katika maisha yao. Je, ni mara ngapi waamini wamemweka Kristo Yesu pembezoni mwa maisha na vipaumbele vyao; wanamwita na kumwamsha pale wanapoanza kuzama na kukosa msaada. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake, kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Kristo Yesu neema ya kuwa na imani thabiti, ambayo kamwe haichoki hata kidogo kumwita na kumtafuta Kristo Yesu, kwa kubisha hodi katika malango ya Moyo wake Mtakatifu. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa katika hija ya maisha yake hapa duniani, kamwe, hakuchoka kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, awe ni kielelezo kwa waamini kutambua umuhimu wa uwepo wa Mungu katika maisha yao, ili mwisho wa siku, waweze kujiaminisha kwake!

Papa Dhoruba
20 June 2021, 15:28

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >