Papa Francisko anakazia majiundo na malezi makini ya Mapadre. Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa. Papa Francisko anakazia majiundo na malezi makini ya Mapadre. Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa. 

Papa: Malezi na Majiundo Makini ya Kipadre: Mt. Yosefu Msimamizi!

Papa amegusia kuhusu Mwongozo wa Malezi ya Kipadre mintarafu maisha ya Mtakatifu Yosefu. Maaskofu ni walezi wa kwanza wa waseminari ambao wanapaswa kujiachilia mikononi mwa walezi wao ili wawafinyangwe kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Waseminari wakite maisha yao katika kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre: “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” unabainisha kwamba, Seminari ndogo na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wadogo wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili. Ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili. Walezi wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo! Mwongozo pia unaangalia wito kwa Daraja takatifu wa watu wenye umri mkubwa, wasaidiwe na kupatiwa malezi makini katika nyumba maalum, ili waweze hatimaye, kufanya maamuzi muhimu katika maisha na wito wao. Jumuiya ya Seminari ya Pio XI Kanda ya Marchigiano, huko mjini Ancona, Alhamisi tarehe 10 Juni 2021 imemtembelea Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican na mazungumzo yao yamejikita zaidi katika Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu katika maisha na utume wake. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu Mwongozo wa Malezi ya Kipadre mintarafu maisha ya Mtakatifu Yosefu. Maaskofu ni walezi wa kwanza wa waseminari na kwamba, hata waseminari wenyewe wanapaswa kujiachilia mikononi mwa walezi wao kama udongo wa mfinyanzi ili wafinyangwe barabara kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Waseminari wakite maisha yao katika kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wake na hatimaye, ametaja mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi na makuzi ya wito wa Kipadre. Baba Mtakatifu anasema, Familia Takatifu ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosefu ilikuwa kama Seminari, mahali ambapo Kristo Yesu alipokelewa, akapewa hifadhi na malezi ili kutekeleza dhamana na wito kutoka kwa Baba yake wa milele. Akafundishwa na Mtakatifu Yosefu na Bikira Maria mambo msingi katika maisha. Alionesha utii na unyenyekevu mkubwa mambo muhimu katika malezi. Walezi wa Seminari wanahamasishwa kuiga na kufuata mfano bora wa maisha na utume wa Mtakatifu Yosefu.

Maaskofu ni walezi wa kwanza wa vijana wao seminarini, utume unaopaswa kutekelezwa kwa ujasiri na ubunifu mkubwa; katika hali ya unyenyekevu na utii; kwa kujitosa bila ya kujibakiza; kwa wema na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Walezi wanapaswa kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu, kwa kukazia useja na upendo kamili unaowawezesha kuwa watu huru katika huduma. Baba Mtakatifu anawataka waseminari kuonesha fadhila ya unyenyekevu, ili waweze kufundwa na hatimaye, kupokea na kuanza kutekeleza majukumu yao kwa wakati wake. Kristo Yesu katika maisha na ujana wake, alijiaminisha kwa malezi na tunza ya Mtakatifu Yosefu na Bikira Maria; akajadiliana na Baba yake wa mbinguni, ili kutambua wito wake hapa duniani. Waseminari wasiridhike na mafanikio makubwa wanayopata kwa kutumia vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii. Neno la Mungu liwafundishe tunu msingi za maisha, ili kuonja wema na upendo wa Mungu; kwa kukimbilia huruma yake isiyokuwa na kifani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Katika maisha kuna kusimama na kuanguka; kuna utakatifu na dhambi. Waseminari wanaweza kuonja na kuchota nguvu za ubinadamu wa Kristo Yesu katika Injili na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Daima wajifunze kutoka kwa watakatifu, mashuhuda na waungama imani, bila kuwasahau wale wote walioshiriki katika mchakato wa kuwarithisha imani. Wajitahidi kusoma vitabu vya watu ambao wamejitahidi kufunua uzuri wa upendo unaookoa! Maisha ya seminari yawasaidie kutambua na kuonja ukweli wa mambo, kwa kujiweka karibu zaidi na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wanaowakutanisha watu na Mungu. Wajitahidi kuondokana na upweke hasi na ubaridi wa moyo. Baba Mtakatifu Francisko amekazia malezi yanayo toa tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kujielekeza katika majiundo ya: kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili. Katika majiundo ya kiutu wajitahidi kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa kukuza fadhila na utu wema ulioko ndani mwao. Wajitahidi kujenga na kudumisha mahusiano mema na matakatifu, wawe ni watu wenye furaha na huru katika maisha na maamuzi yao.

Wakuze na kujenga tasaufi inayosimikwa katika sala, tafakari na Liturujia mbalimbali zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Wajikite katika masomo bila woga wala wasiwasi ili mwisho wa siku, waweze kupata tunu msingi za Kiinjili. Utume unaowasubiri huko mbeleni unahitaji maandalizi thabiti pamoja na umakini zaidi. Malezi ya shughuli za kichungaji, yawawezeshe kujiandaa kuwa ni wahudumu wa watu wa Mungu kwa kumuiga Kristo Yesu, mchungaji mwema. Jumuiya ya Seminari iwe ni kielelezo cha ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati, tayari kukabiliana na changamoto mamboleo katika malezi na makuzi. Seminarini ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili.

Papa Malezi Seminarini

 

10 June 2021, 16:13