Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu "Njoo Uone": Mawasiliano Kwa kukutana na Watu Jinsi na Mahali Walipo Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 unaongozwa na kauli mbiu "Njoo Uone": Mawasiliano Kwa kukutana na Watu Jinsi na Mahali Walipo 

Ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari

Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa waandishi wa habari “kuchakarika usiku na mchana ili kutafuta habari”, tukio lile la kwenda na kuona limekua ni mwanzo na chemchemi ya imani, changamoto na mwaliko kwa waandishi wa habari kuwa na ujasiri. Baba Mtakatifu anagusia fursa na mitego iliyoko kwenye wavuti. Hakuna kitu mbadala cha kuona kama mwanadamu. Shuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Jumapili, tarehe 16 Mei 2021 sanjari na Sherehe ya Bwana Kupaa Mbinguni unanogeshwa na kauli mbiu “Njoo uone” Yn. 1:46, sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane. Haya ni maneno ya Kristo Yesu alipokutana kwa mara ya kwanza na Mitume wake, kielelezo makini cha mawasiliano ya kibinadamu. Ili kutangaza na kushuhudia ukweli wa maisha unaounda historia kuna haja ya kujitosa kimasomaso na kwenda kutazama, kukaa pamoja na wadau mbalimbali, kuwasikiliza, kupokea maoni yao na hatimaye, kufungua macho ili kujionea hali halisi. Mawasiliano hayana budi kuwa wazi na ya kweli katika kurasa za magazeti, kwenye mitandao ya kijamii, wakati wa mahubiri na hata katika mawasiliano katika mambo ya kisiasa na kijamii. Njoo uone ni mchakato ambao imani ya Kikristo imeweza kutangazwa na kushuhudiwa! Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa waandishi wa habari “kuchakarika usiku na mchana ili kutafuta habari”, tukio lile la kwenda na kuona limekua ni mwanzo na chemchemi ya imani, changamoto na mwaliko kwa waandishi wa habari kuwa na ujasiri. Baba Mtakatifu anagusia fursa na mitego iliyoko kwenye wavuti. Hakuna kitu mbadala cha kuona kama mwanadamu.

Wito wa “Njoo uone” ni njia makini ya ujenzi wa mawasiliano ya kijamii, ili kusema ukweli unaogeuka kuwa ni historia, kuna haja ya kuondokana na utendaji wa kazi kwa mazoea. Kumbe, kuna haja ya kuwaendea watu, kukaa nao, kusikiliza habari zao na kuzilinganisha na ukweli, ambao mara nyingi unawaacha watu wengi wakiwa wamepigwa bumbuwazi. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii hawana budi kufungua macho yao ili kuona maajabu ya ulimwengu, wakunjue mikono yao ili kugusa maisha ya watu, ili wengine wanaposoma waguswe na muujiza wa maisha kama alivyowahi kusema, Mwenyeheri Manuel Lozano Garrido kwa waandishi wa Habari. Wito wa “Njoo uone” ni msukumo kwa ajili ya mawasiliano yote yanayopania kuwa wazi na wakweli katika magazeti, kwenye intenet, mahubiri katika siasa ua mawasiliano ya kijamii. Wito huu umekuwa ni njia ambayo imani ya Kikristo imekuwa ikitangazwa na kushuhudiwa, tangu wale Mitume walipokutana kwa mara ya kwanza na Kristo Yesu pale Mtoni Yordan na kwenye Bahari ya Galilaya.

Baba Mtakatifu anawaalika Waandishi wa Habari “kuchanja mbuga” ili kupata habari nzuri zaidi. Kuna upashanaji habari ambao umekuwa ukitumia sauti. Lakini uandishi wa habari za uchunguzi wa kina kwa ajili ya magazeti, luninga, radio na wavuti zinaanza kupungua makali na viwango vyake, kiasi cha kushindwa kutoa ukweli na uhalisia wa maisha ya watu; ni habari ambazo hazina uzito kwa sababu hazipati chimbuko lake kutoka katika maisha ya watu, matatizo na changamoto zao. Matokeo yake ni habari nyingi kutengenezwa kwenye “Vyumba vya habari” kwenye Komputer, mitandao ya kijamii, bila “kuchakarika” kutaka kukutana na watu mubashara katika shughuli zao na kuzifanyia uchunguzi wa kina ili kupata ukweli wa mambo kutoka kwa wahusika. Bila ya kujenga utamaduni wa watu kukutana, tasnia hii itabaki kama watazamaji kwa maendeleo makubwa ya teknolojia kushindwa kuzama katika uhalisia wa maisha ya watu. Vyombo vinaweza kutumika na kuwa na thamani, ikiwa kama vitawasukuma watu kutoka nje na kwenda kujionea ukweli wa mambo ulivyo. Vinginevyo ingelikuwa vigumu kufahamu yale yanayoendelea kujiri na hatimaye, kurusha habari hizi kwenye mitandao ya kijamii. Na wala kusingekuwepo mchakato wa watu kukutana.

Njooni nanyi mtaona ni maneno ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake wa kwanza waliotaka kufahamu mahali alipokuwa anaishi. Na huo ukawa ni mwanzo wa kujenga mahusiano na mafungamano kati yao. Yohane Mwinjili, tayari akiwa mzee anayakumbuka maneno haya ya Kristo Yesu na kuyafanya kuwa ni ushuhuda unaopaswa kuwa ni Habari kwa sababu alikuwepo mubashara. Anakumbuka hata na wakati kwamba, “ilikuwa yapata saa kumi”. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Nathanaeli aliyethubutu kuuliza, “Laweza neno jema kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia “Njoo uone.” Nathanael akaenda, akaona na tangu siku ile maisha yake yakabadilika kabisa. Hivi ndivyo imani ya Kikristo inavyopata chimbuko lake na hatimaye, kutangazwa na kushuhudiwa kama maarifa ya moja kwa moja yanayopata chimbuko lake kutokana na uzoefu wa maisha na wala si kile ambacho wamekisikia tu! Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa wananchi wa Samaria baada ya kukutana na kumsikiliza Kristo Yesu, wakamwambia yule mwanamke Msamaria, si kwamba, wana mwamini Kristo Yesu kwa sababu ya maneno yake, bali kwa sababu wamemsikia wao wenyewe, tena wanajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Rej. Yn. 4:39-42. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili kuweza kufahamu vyema, kuna haja ya kuona ili kupata ushuhuda wa moja kwa moja!

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Waandishi wa Habari kwa ujasiri wao, kwa kutia nia ya kutaka kusikia na kuona, hata pale ambapo pengine, watu wengine wasingethubutu kwenda! Kwa hakika wadau wa tasnia ya mawasiliano wanastahili kupewa pongezi. Hii ni kutokana na juhudi pamoja na ujasiri wao, leo hii, walimwengu wanafahamu zaidi kuhusu: nyanyaso na dhuluma za kidini sehemu mbalimbali za dunia. Wamesaidia kuonesha shida na mateso wanayokabiliana nayo maskini. Hawa ni wadau ambao wameshuhudia athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; mipasuko na vita ambavyo visingeweza kufahamika kama si kwa juhudi za wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii. Bila ujasiri wao, yote haya yasingefahamika na hivyo kuwa ni hasara kubwa si tu kwa vyombo vya mawasiliano kukosa habari, bali hata kwa jamii, demokrasia na sauti ya wanyonge isingeweza kusikika hata kidogo. Na kwa hakika, familia kubwa ya binadamu ingebaki kuwa ni maskini wa kutupwa!

Kutokana na matatizo na changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo, hususan janga na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, linawahitaji wadau wa tasnia ya mawasiliano, kwenda kujionea wao wenyewe hali halisi. Kuna hatari kwamba, janga la UVIKO-19 likaangaliwa kwa “miwani” ya Mataifa tajiri peke yake, kwa kuzama katika chanjo, vifaa tiba na huduma kwa wagonjwa na kusahau umati mkubwa wa maskini kutoka katika Nchi maskini zaidi ulimwenguni. Tofauti za kiuchumi na kijamii sehemu mbalimbali za dunia zinaweza kugeuka na kuwa ni kigezo msingi katika chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hii ni hatari anasema Baba Mtakatifu Francisko kwani maskini wataendelea “kuogelea katika dimbwi la umaskini”. Kigezo kwamba, afya bora ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kitabaki kuwa katika maandishi peke yake. Baa la umaskini linaendelea kupekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu hata katika Nchi Tajiri zaidi ulimwenguni. Leo hii, kuna maelfu ya watu kutoka katika Nchi tajiri zaidi, wanaojipanga kusubiri mgao wa chakula kutokana na ukata mkubwa wa fedha na umaskini! Kwa bahati mbaya, umaskini miongoni mwa Nchi tajiri zaidi ulimwengu si sehemu ya habari.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kuna fursa na matatizo pamoja na changamoto nyingi ambazo zimefichama kwenye wavuti “Web”. Kumekuwepo na mafuriko makubwa ya habari kwenye vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Watu wanaweza kujionea kwa macho yao na kusikiliza shuhuda za watu mbalimbali. Watu wanaweza kupata habari motomoto, kitu ambacho ni vizuri kabisa. Mfano hai ni taarifa rasmi za majanga asilia pamoja na matukio ambayo yamewajengea uwezo watumiaji wa vyombo hivi vya mawasiliano ya jamii. Ni kwa njia ya wavuti kwamba vyombo vya mawasiliano ya jamii vinaweza kutoa taarifa na kuona kile kinachoendelea kujiri, mbele ya macho yao na hatimaye, kuwashirikisha wengine. Kuna hatari kubwa kwamba, kile kinachoonekana kwenye mitandao ya kijamii ndio ukweli wa mambo na kusahau kwamba, wakati mwingine, kuna habari za kughushi zinazokita mizizi yake katika ubinafsi. Kumbe, kuna haja ya kuwa na udadisi mkubwa unaokwenda sanjari na mang’amuzi pamoja uwajibikaji wa maudhui yanayotumwa na kupokelewa na walaji. Kila mtu anawajibika katika mchakato wa mawasiliano, kwa kushirikishana habari, kwa kudhibiti habari dhidi ya habari za kughushi na kuzianika hadharani. Kila mtu anapaswa kuwa ni shuhuda wa ukweli: kwa kwenda, kuona na kushirikishana.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hakuna kitu kinachoweza kuwa mbadala kwa ushuhuda wa awali wa wale waliokuwa kwenye tukio husika, kwani haya ni mang’amuzi ya mtu binafsi. Kuna njia mbalimbali za kuweza kufikisha ujumbe unaokusudiwa; kwa kutumia macho, sauti pamoja na vitendo. Kristo Yesu alikuwa na mvuto kwa watu wengi kutokana na mahubiri yake yaliyosheheni ukweli, mahusiano na mafungamano na watu mbalimbali; jinsi alivyowapokea na kuwatendea na hata katika ukimya wake, bado watu waliweza kusoma ujumbe wake. Mitume wa Yesu, walibahatika kumsikiliza, wakaonja jinsi alivyokuwa anahubiri na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na wengi wao wakaguswa na majadiliano kati yao na yeye, kiasi cha kuamua kumfuasa. Hata leo hii, Wito wa “Njoo uone” bado ni endelevu na muhimu sana!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni anasikitika kusema kwamba, hata leo hii katika ulimwengu mamboleo, kuna watu wanaendelea “kupiga maneno tu” katika maisha ya hadhara, kwenye biashara na hata katika siasa. Lakini ikumbukwe kwamba, Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudiwa ulimwenguni kama matokeo ya kukutana mubashara na wafuasi wa Kristo Yesu, waliotikia mwaliko wa njoo uone na wao sasa wamekuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu. Bila shaka, Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa angekuwepo wakati huu, angelitumia pia njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii kufikisha Habari Njema kwa watu wa Mataifa. Watu wengi walivutwa na maisha na utume wa Mtakatifu Paulo kutokana na imani, matumaini na mapendo yake, kiasi cha kutaka kukaa na kumsikiliza au kuandamana pamoja naye! Maisha na utume wake, ulikuwa ni ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, Neema na Baraka za Mungu na kwamba, kwa hakika, alikuwa ni mwanafunzi na shuhuda wa njia ya maisha ya Kristo Yesu. Biblia Takatifu ni utimilifu wa Torati na Unabii.

Injili Takatifu ni chachu ya mabadiliko na mageuzi makubwa kwa kukutana na Kristo Yesu katika maisha. Changamoto mamboleo ni kujikita katika mawasiliano yanayowakutanisha watu, mahali walipo na jinsi walivyo! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kutoka katika ubinafsi wao, tayari kutafuta ukweli. Awafundishe kuona, kusikiliza, ili kuelewa na kuondokana na maamuzi mbele au hitimisho la jumla. Mwenyezi Mungu awafundishe waamini kuzingatia mambo msingi katika maisha, na kamwe wasivutwe na malimwengu yanayoelea kwenye ombwe. Wawe na uwezo wa kutofautisha yale mambo yanayowadanganya watu kwa kuwavutia kwa macho, bali wazingatie ukweli. Mwenyezi Mungu awajalie waamini wake neema ya kutambua mahali anapoishi Mwenyezi Mungu katika ulimwengu huu na hivyo kuwa wakweli ili kusimlia kile walichoona!

Papa Ujumbe 55

 

 

13 May 2021, 16:28