Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari: Kauli mbiu: Habari kwa ajili ya mafao ya umma: Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi, uhuru na amani! Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari: Kauli mbiu: Habari kwa ajili ya mafao ya umma: Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi, uhuru na amani! 

Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari: Haki na Amani Duniani!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anabainisha kwamba, kuna haja ya kutumia vyombo mbaliambali, lakini zaidi vyombo vya mawasiliano ya jamii kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kuimarisha amani kwa ajili ya mafao ya wengi. Amani ya kweli inakita mizizi yake katika: Ukweli, haki, upendo na uhuru. Amani ni jina jipya la maendeleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1993 liliridhia kuanzishwa kwa Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Mei. Ni siku maalum kwa vyombo vya habari kujinadi kwa kuonesha umuhimu wa vyombo vya habari katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kauli mbiu ya mwaka 2021 inasema, habari ni kwa ajili ya mafao ya umma. Kumbe, kuna umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari duniani sanjari na kuwalinda wadau wa mawasiliano ya jamii ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Lengo ni kuimarisha mchakato wa uzalishaji, ugawaji na hatimaye, matumizi yake, kwa kuimarisha uandishi wa habari, ukweli na uwazi pamoja na kuwajengea uwezo walaji. Mchakato wa mawasiliano ya jamii umekuwa na mabadiliko makubwa katika miaka ya hivi karibuni, kiasi kwamba athari zake zinasikika katika sekta ya afya, utu, heshima na haki msingi za binadamu, demokrasia, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anabainisha kwamba, kuna haja ya kutumia vyombo mbaliambali, lakini zaidi vyombo vya mawasiliano ya jamii kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kuimarisha amani kwa ajili ya mafao ya wengi. Amani ya kweli inakita mizizi yake katika: Ukweli, haki, upendo na uhuru. Naye Mtakatifu Paulo VI anasema, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu haki msingi za binadamu na uwajibikaji, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani kwa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni anasema, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kiasi cha kuwa na uwezo wa kushirikisha kile kilicho: kweli, chema na kizuri ili kuweza kuunda kumbukumbu ya kihistoria pamoja na kuelewa matukio mbalimbali yanayomzunguka mwanadamu.  

Lakini kutokana na ubinafsi, mwanadamu amejikuta akiharibu uwezo wake wa kuwasiliana na wengine, hali ambayo inapata chimbuko lake hata kutoka katika Maandiko Matakatifu. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kusimama kidete kupinga habari za kughushi, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na weledi wa uandishi wa habari kwa wanahabari wenyewe kuwajibika kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia ukweli! Baba Mtakatifu anasema, amani ndiyo habari ya kweli inayomlenga mtu mzima ili kumjengea uwezo wa kusikiliza, kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa kuvutwa na: ukweli, wema na uzuri ili hatimaye, kuwajibika barabara. Wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wanao wajibu na utume mzito wa kulinda ukweli wa habari kwa kutambua kwamba, mlengwa mkuu ni binadamu.

Habari inalenga kuwaunda watu wengine katika jamii, kugusa maisha yao ili kudumisha wema na uaminifu unaofungua njia ya umoja na amani. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawataka waandishi wa habari kujikita katika uandishi wa habari wa amani kwa kuondokana na habari za kughusi zinazochezea vionjo na hisia za watu kama alivyokuwa nyoka, Ibilisi katika Agano la Kale. Uwe ni uandishi wa habari kwa ajili pamoja na watu, yaani uandishi wa habari kwa ajili ya huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu; ili kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti. Waandishi wa habari wasijikite tu kwa kutoa “Breaking News”, bali wawe na ujasiri, ari na moyo wa kupembua kwa kina na mapana sababu msingi zinazopelekea vita, kinzani na migogoro ya kijamii, ili kujenga uelewa mpana zaidi utakaosaidia mchakato wa suluhu na amani ya kudumu. Uandishi wa habari anaoutaka Baba Mtakatifu Francisko ni ule usiokuwa wa vita ya maneno na makelele kibao! Waandishi wa Habari wawe ni vyombo na mashuhuda wa mchakato wa maridhiano, haki na amani duniani akiwataka kurejea katika Sala ya Mtakatifu Francisko kwa Assisi, ili kweli waandishi wa habari waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vinavyodumisha haki, amani, utu na heshima ya binadamu.

Na habari kutoka Tanzania zinabainisha kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo tayari wakati wowote kushirikiana na vyombo vya habari na waandishi wa habari katika utekelezaji wa majukumu yao. Uhuru wa vyombo vya habari na waandishi watalindwa, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu, huku wakizingatia sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa kwa ajili ya kusimamia tasnia hii muhimu. Siku hii iwakumbushe waandishi wa habari kuhusu: taaluma, haki na wajibu sanjari na kutanguliza maslahi ya Taifa. Waandishi wa habari waoneshe weledi mkubwa kwa kuzingatia maudhui wanayotoa kwa jamii.

Vyombo vya Habari
03 May 2021, 15:13