Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 31 Mei 2021 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa "Federazione Italiana Pallacanestro" Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwao! Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 31 Mei 2021 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa "Federazione Italiana Pallacanestro" Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwao! 

Papa: Umuhimu wa Michezo Katika Maisha: Kiroho na Kimwili!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia: Umuhimu wa umoja na mshikamano, ili waweze kucheza kama timu, huku wakijenga na kudumisha nidhamu na utu wema, daima wajitahidi kuyaangalia yaliyo juu! Michezo hata kama ni binafsi, daima inamsaidia mwanamichezo kukutana na kujenga mahusiano na wengine wanaotoka katika maeneo na mazingira tofauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Yesu Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali: uchoyo na ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii fungamani na shirikishi! Ni katika muktadha wa umuhimu wa michezo katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 31 Mei 2021 amekutana na kuzungumza na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Nchini Italia “Federazione Italiana Pallacanestro” kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.

Kunako mwaka 1955, kumbukumbu zinaonesha kwamba, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Papa Pio XII alishuhudia “mpambano” wa Mpira wa Kikapu, wakati “wanaume wakitoana kijasho na kupigana vikumbo”. Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho Mama Kanisa alianza kuwa karibu zaidi na Ulimwengu wa wanamichezo, kama sehemu ya mchakato wa ukuaji na ukomavu wa mtu mzima, ili waweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amejielekeza na kukazia zaidi, umuhimu wa umoja na mshikamano, ili waweze kucheza kama timu, huku wakijenga na kudumisha nidhamu na utu wema, daima wajitahidi kuyaangalia yaliyo juu! Michezo hata kama ni binafsi, daima inamsaidia mwanamichezo kukutana na kujenga mahusiano na wengine wanaotoka katika maeneo na mazingira tofauti. Wanaungana pamoja, lakini pia wanapambana ili kuweza kufikia lengo la jumla.

Kumbe, ni muhimu kuungana na kushikamana, huku wakiwa na lengo moja. Katika hali na mazingira kama haya, michezo inakuwa ni dawa ya kuganga na kuponya uchoyo na ubinafsi unaotawala katika jamii ya mwanadamu, hali ambayo inapelekea baadhi ya watu kujikuta wakitumbukia katika upweke hasi, mwanzo wa kuchungulia kaburi! Wanamichezo wajifunze kujenga umoja, ili kukuza ari na moyo wa kutafuta mambo mema zaidi. Na kwa njia ya michezo tunu ya udugu wa binadamu kiini cha Injili unaweza kudumishwa na wote! Jambo la pili ambalo wanamichezo wanapaswa kulizingatia ni nidhamu na utu wema. Haya ni mambo msingi wakati wa mazoezi ya kiroho na kimwili. Nidhamu inahitaji umakini katika maisha, kwa kuzingatia ratiba ya shughuli pamoja na kuratibu chakula. Nidhamu ni shule ya majiundo endelevu na elimu makini hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Huu ni mwaliko kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanajikita katika nidhamu na utu wema, ili kuweza kuwajibika barabara pamoja na kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, kama sehemu ya maboresho ya maisha!

Nidhamu ni muhimu sana hata katika maisha ya kiroho yanayosimikwa katika uaminifu, udumifu na maisha ya sala kila kukicha. Bila ya nidhamu na mazoezi ya kudumu, imani inaweza kuchauka na kuzimika! Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo kuangalia na kuyatafuta yaliyo juu, kama sehemu ya changamoto yao ya maisha. Wasithubutu kuangalia na kuambata yaliyo ya chini, watageuka na kuwa ni nguzo ya chumvi! Wanamichezo wajitahidi kurithisha tunu msingi kwa watoto na vijana, daima wakiwa na malengo makubwa. Watambue kwamba, maisha ya mwanadamu yanasimikwa katika kushinda na kushindwa; kuanguka, kusimama na kuendelea na maisha. Katika maisha hata kama hukubahatika kufunga, lakini bado kuna nafasi ya kuweza kufanya vyema zaidi!

Papa Michezo
31 May 2021, 17:02