Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 3 Mei 2021 ataongoza Kikao cha Baraza la Makardinali ili kupigia kura majina ya wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu. Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 3 Mei 2021 ataongoza Kikao cha Baraza la Makardinali ili kupigia kura majina ya wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu. 

Papa Francisko Kuongoza Kikao cha Makardinali 3 Mei 2021

Papa Jumatatu tarehe 3 Mei 2021 anatarajiwa kuongoza Baraza la Makardinali ili kupigia kura majina ya Wenyeheri saba wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu na hivyo kuandikwa kwenye Orodha ya Watakatifu wa Kanisa. Hawa ni Mwenyeheri Lazzaro Devasahayam, Mwamini mlei na shahidi. Mwenyeheri Cèsar de Bus, Padre na Mwanzilishi wa Shirika la Mafundisho ya Kikristo.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Waamini wanahimizwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu na wawe ni matunda ya Roho Mtakatifu, ili wafanywe watakatifu. Kutokana na udhaifu wa binadamu, waamini wanahitaji mara kwa mara kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kudadavua kuhusu Fumbo la Kanisa kwa kusema, Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kushiriki utakatifu mmoja, kwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli; kwa kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa ni: mtii, fukara na mnyenyekevu wa moyo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa njia hii, wastahilishwe kushiriki utukufu wa Kristo! Upendo wa dhati ni njia inayoweza kuwapeleka waamini katika utakatifu! Wanapaswa pia kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; huku wakijitahidi kushiriki mara kwa mara Sakramenti za Kanisa; kwa kujitia uthabiti katika kusali, kujinyima pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi.

Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Waraka huu mpya unazinduliwa rasmi, tarehe 9 Aprili 2018, Kumbu kumbu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza safari ya utakatifu wa maisha!

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 3 Mei 2021 anatarajiwa kuongoza Baraza la Makardinali ili kupigia kura majina ya Wenyeheri saba wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu na hivyo kuandikwa kwenye Orodha ya Majina ya Watakatifu wa Kanisa. Hawa ni Mwenyeheri Lazzaro Devasahayam, Mwamini mlei na shahidi. Mwenyeheri Cèsar de Bus, Padre na Mwanzilishi wa Shirika la Mafundisho ya Kikristo. Mwenyeheri Luigi Maria Palazzolo, Padre na Mwanzilishi wa Shirika ya Watawa Maskini wa Palazzolo. Mwenyeheri Giustino Maria Russolillo, Padre na Muasisi wa Shirika la Miito Mitakatifu. Mwenyeheri Charles de Foucauld, Padre wa Jimbo aliyesadaka maisha yake katika sala, maisha ya kidugu na huduma ya upendo kwa maskini. Mwenyeheri Maria Francesca di Gesù, ambaye hapo awali alitambulikana kama Anna Maria Rubatto ni Muasisi wa Shirika la Utawa wa Tatu la Wakapuchin wa Loano. Na hatimaye, ni Mwenyeheri Maria Domenica Mantovani, Muasisi wa Shirika na Mama Mkuu wa kwanza wa Shirika la Masista Watawa Wadogo wa Familia Takatifu.

Watakatifu

 

01 May 2021, 16:36