Baba Mtakatifu Francisko tarehe 16 Mei 2021 ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea haki,amani na upatanisho wa kitaifa nchini Myanmar. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 16 Mei 2021 ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea haki,amani na upatanisho wa kitaifa nchini Myanmar. 

Papa Francisko: Ibada ya Misa Takatifu Watu wa Mungu Myanmar

Hii itakuwa ni Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Myanmar. Huu ni ushuhuda wa upendo wa dhati wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini Myanmar. Ni Ibada itakayowashirikisha watu wa Mungu kutoka Mynamar wanaoishi hapa mjini Roma, bila kujali imani na dini zao, lengo kubwa ni kuombea haki na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kwa nyakati mbalimbali ameonesha uwepo wake wa karibu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na watu wa Mungu wanaoteseka kutokana na mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar. Pamoja na kutumia silaha za kidiplomasia ili kupata suluhu ya mgogoro wa kisiasa nchini Myanmar, Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa anajielekeza zaidi katika mapambano kwa njia ya Sala na Sadaka ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa tarehe 16 Mei 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii itakuwa ni Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Myanmar. Huu ni ushuhuda wa upendo wa dhati wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini Myanmar. Ni Ibada itakayowashirikisha watu wa Mungu kutoka Mynamar wanaoishi hapa mjini Roma, bila kujali imani na dini zao, lengo kubwa ni kuombea haki, amani na upatanisho wa Kitaifa.

Ombi la Ibada ya Misa Takatifu kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Myanmar lilitolewa na Padre Joseph Buan Sing, ambaye yuko bado kwenye malezi na makuzi ya kitaalimungu, Shirika la Wayesuit mjini Roma. Inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu 200 wanatarajiwa kushiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu. Padre Joseph Buan Sing anasema, tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu ameonesha upendo wa hali ya juu kwa watu wa Mungu nchini Myanmar. Ameguswa sana na mateso pamoja na mahangaiko ya maskini wa Myanmar. Barua hii iliandikwa kwa matumaini makubwa kwa Baba Mtakatifu naye kwa hakika amejibu bila kusita. Ibada ya Misa Takatifu itaendelea kuwa ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kutoka kwa Baba Mtakatifu kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Myanmar.

Itakumbukwa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kulaani na kushutumu mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Myanmar tarehe 1 Februari 2021 na tangu wakati huo, kumekuwepo na maandamano makubwa kupinga mapinduzi ambao kwa sasa yamekuwa ni kichocheo kikubwa cha: ukatili, mateso, mauaji na uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Wito unaendelea kutolewa na Jumuiya ya Kimataifa wa kurejeshwa tena utawala wa kidemokrasia sanjari na kuachiliwa huru Aung San Suu Kyi kiongozi mkuu wa Chama cha “National League for Democracy, NLD., na wanasiasa wenzake wanaoshikiliwa kizuizini. Ni katika muktadha huu, hivi karibuni Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika barua aliyomwandikia Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo la Yangon ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Myanmar, alimwomba ili awakilishe ujumbe wa udugu wa amani na mshikamano, wasi wasi na upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Parolin anamsihi Kardinali Maung Bo kuhakikisha kwamba, anasaidia mchakato wa kuwakutanisha viongozi wakuu wanaohusika na mgogoro huu wa kisiasa, ili kujadiliana katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Viongozi wa Kanisa wasaidie kuwapatia wananchi na hasa vijana matumaini; walinde na kudumisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu! Amani ni jambo linalowezeka, ikiwa kama masilahi ya kitaifa yatapewa kipaumbele cha kwanza. Jumuiya ya waamini inapaswa kujielekeza zaidi katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani, maridhiano na umoja wa Kitaifa. Ni wakati wa kuanza kujikita katika demokrasia na utawala bora zaidi.

Papa Myanmar

 

09 May 2021, 15:53