Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Mei 2021 amepokea Biblia Takatifu iliyotafsiriwa katika lugha asilia. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Mei 2021 amepokea Biblia Takatifu iliyotafsiriwa katika lugha asilia. 

Papa Francisko Apokea Biblia Iliyotafsiriwa kwa Lugha Asilia!

Biblia Takatifu iliyotafsiri kwa lugha asilia ni utume uliotekelezwa kwa sala na sadaka kubwa kwa muda wa miaka 8 kutoka kwa Bwana Luigi Zuccheri. Tafsiri ya Biblia imefanywa kwa kusoma, kusali na kuandika. Baba Mtakatifu amemshukuru na kumpongeza Zuccheri, kwa jitihada zake za kutaka kukirithisha kizazi kipya amana na utajiri wa Neno la Mungu katika lugha yao ya asili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ufasiri wa Biblia, ijapokuwa ni jukumu la pekee la wafafanuzi, lakini si ukiritimba wao, kwa sababu unahusu, katika Kanisa, vipengere ambavyo vyapita uchanganuzi wa kisayansi wa matini. Naam, Kanisa halitazami tu Biblia kama jumla ya hati za kihistoria kuhusu asili yake; linaipokea kama Neno la Mungu linaloelekezwa kwake, na kwa ulimwengu wote, katika siku za leo. Hakika hiyo ya imani ina matokeo yake katika juhudi za kuuhusisha na kuutamadunisha ujumbe wa Biblia, kama vile kuyaratibu matumizi mbalimbali ya matini zilizovuviwa, katika liturujia, katika “lectio divina”, katika huduma ya shughuli za kiuchungaji, na katika harakati za majadiliano ya kiekumene. Katika nchi mbalimbali yalitolewa machapisho, kwa msaada wa wafafanuzi, ili kusaidia wanaohusika na uchungaji kufasiri kisahihi masomo ya Biblia ya Liturujia na kuyahusisha kwa namna ya kufaa. Ni matumaini kuwa juhudi hizo zitaenea zaidi. Wahubiri lazima waepukane na msisitizo wa upande mmoja tu kuhusu nyajibu zinazowapasa waamini. Ujumbe wa Biblia sharti udumishiwe tabia yake maalum ya kuwa Habari Njema ya Wokovu uliyotolewa na Mungu.

Mahubiri yatakuwa na manufaa na yatalingana zaidi na Biblia yakisaidia kabla ya yote waamini “kujua karama ya Mungu” (Yn 4:10), ilivyofunuliwa katika Maandiko Matakatifu, na kufahamu kwa namna iliyo bora masharti yatokanayo. Utume wa Biblia una shabaha ya kujulisha Biblia kama Neno la Mungu na chemchemi ya uhai. Kwanza, huhimiza kazi ya kutafsiri Biblia katika lugha mbalimbali, na kusambaza tafsiri hizo. Huamsha na kutegemeza shughuli nyingi: uundaji wa vikundi vya Biblia, mihadhara kuhusu Biblia, “majuma ya Biblia”, uchapishaji wa magazeti na vitabu, n.k. Mchango maalum hutolewa na vyama na harakati za kikanisa zinazoweka katika nafasi ya kwanza somo la Biblia kwa mtazamo wa imani na wa uwajibikaji wa kikristo. “Jumuiya ndogondogo” nyingi zinatia Biblia kama kiini cha mikutano yao ya sala na kudhamiria lengo la aina tatu: kujua Biblia, kujenga jumuiya na kuwahudumia watu. Na hapo pia msaada wa wafafanuzi unafaa ili kuepa uhusisho usio na misingi. Lakini, ni sababu ya furaha kuona Biblia mikononi mwa watu wanyonge na maskini, wanaoweza kutilia nuru ya ndani kwa ufasiri na uhusisho wake kisasa, kwa upande wa mtazamo wa kiroho na wa kimaisha, kuliko wale wenye sayansi inayojitegemea yenyewe (taz. Mt 11:25).

Umuhimu unaozidi kukua daima wa vyombo vya mawasiliano ya jamii yaani: vitabu na magazeti, radio, televisheni pamoja na mitandao ya kijamii kwa sasa, hudai kuwa ushuhuda, tangazo la Neno la Mungu na ujuzi wa Biblia vienezwe kwa bidii kwa njia ya vyombo hivyo. Dhima maalum sana ya vyombo hivyo, na tena, nguvu ya juu ya kuwaathiri watazamaji wengi hudai matayarisho ya pekee kwa ajili ya utumiaji wake ili kuepa ufaraguzi usiopendeza, na pia matokeo ya kushangaza chapwa. Iwe ni katekesi, iwe ni mahubiri au utume wa kibiblia, matini ya Biblia lazima ionyeshwe daima kwa heshima istahilivyo.  Majadiliano ya kiekumene yalenge zaidi umoja wa Wakristo katika imani, matumaini na upendo (Efe 4:2-5), katika kuheshimiana (Flp 2:1-5) na katika mshikamano (1Kor 12:14-27; Rum 12:4-5), lakini pia, na hasa, umoja hai na Kristo, kama matawi katika mzabibu (Yn 15:4-5), au viungo vya mwili na kichwa (Efe 1:22-23; 4:12-16). Umoja huo sharti uwe mkamilifu, kwa mfano wa ule wa Baba na Mwana (Yn 17:11-22). Maandiko Matakatifu hueleza msingi wake kitaalimungu (Efe 4:4-6; Gal 3:27-28). Jumuiya ya kwanza ya kitume ni mfano wake thabiti na hai (Mdo 2:44; 4:32). Rejea Waraka wa: TUME YA KIPAPA YA BIBLIA UFASIRI WA BIBLIA KATIKA KANISA, Roma, 15 Aprili 1993.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Jumapili tarehe 30 Mei 2021 amekutana na kuzungumza na Kikundi cha waamini kutoka Piacenza, Kaskazini mwa Italia, waliofika mjini Vatican ili kumzawadia nakala ya Biblia Takatifu iliyotafsiri kwa lugha asilia. Huu ni utume uliotekelezwa kwa sala na sadaka kubwa kwa muda wa miaka 8 kutoka kwa Bwana Luigi Zuccheri, mwenye umri wa miaka 78. Tafsiri ya Biblia imefanywa kwa kusoma, kusali na kuandika. Baba Mtakatifu amemshukuru na kumpongeza Bwana Luigi Zuccheri, kwa jitihada zake za kutaka kuhakikisha kwamba, anakirithisha kizazi kipya amana na utajiri wa Neno la Mungu katika lugha yao ya asili. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wawe na ujasiri wa kubeba Biblia Takatifu na kujisomea pale wanapopata nafasi. Ni kwa njia hii, waamini wataweza kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Bwana Luigi Zuccheri ambaye ameamua kutumia muda wake wa uzeeni kwa ajili ya kutafsiri Maandiko Matakatifu ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Maandiko Matakatifu, kwa kusali, kusoma na kutafsiri.

Biblia Takatifu

 

31 May 2021, 15:43