Papa Francisko amesali kwa ajili ya ubinadamu ili janga liishe

Papa Francisko katika maombi yake kwenye sala ya Rosari amekumbuka kuanzia chanjo dhidi ya Covid,marehemu na familia zao,watu wanaoishi na umaskini,madaktari na wauguzi,wanasayansi,watu wa kujitolea,wasio na kazi,wanawake waliopata vurugu wakati wa karantini,na watu wasio na matumani tena.Ni katika tukio aliloongoza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Kama ilivyokuwa imekwisha tangazwa kuhusu Mwezi Mei ambao umewekwa na mama Kanisa kwa ajili ya Mama Maria  kusali Rosari ndivyo ilifunguliwa kwa namna hiyo Mei Mosi 2021. Kwa mwaka huu mwezi huu unakuwa wa aina yake, kutokana na maombi ya Baba Mtakatifu Francisko kuomba kusali kwa Mama Maria ili atuombee janga liishe ulimweguni. Kwa maana hiyo hatua ya kwanza kama mnyoyoro wa sala au Marathoni ya sala, kwa mwezi mzima wa Mei unaunganisha ulimwenguni kwa sala moja kupitia madhabahu maalum 30 zilizochaguliwa ili kuongoza waamini wote wasali kwa pamoja. Uzinduzi wa sala kwa matashi ya Baba Mtakatifu, ulifanyika katika Kanisa  Kuu la Mtakatifu Petro Vatican, katika Kikanisa cha Kigregoriana mahali ambamo panahifadhiwa masalia ya Mtakatifu Gregorio wa Nazianso, Mwalimu na Baba wa Kanisa, kwa sala hiyo yenye lengo la kuomba  janga  la covid liweze kuisha ulimwenguni na kuleta faraja kwa wale ambao wameguswa kwa karibu na janga hili.

Kuombea ubinadamu uliojeruhiwa na janga

Katika sala ya Papa akiomba kwa Mama Maria amesema: “Mwanzoni mwa mwezi uliowekwa kwa Mama yetu, tunaungana kwa  maombi na madhabahu  yote ulimwenguni, na waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuukabidhi ubinadamu wote, uliojaribiwa sana na kipindi hiki cha janga. Kila siku ya mwezi huu wa Mei tutakukabidhi Wewe, Mama wa Huruma, watu wengi ambao wameguswa na virusi na wanaendelea kupata mateso yake; kuanzia kwa kaka na dada zetu waliokufa, hadi familia ambazo zinapata uchungu na kutokuwa na uhakika wa kesho; kutoka kwa wagonjwa hadi kwa madaktari, wanasayansi, wauguzi, wanaohusika wakiwa mstari wa mbele katika vita hivi; kutoka kwa watu wa kujitolea hadi  wataalam wote ambao wametoa huduma yao ya thamani kwa ajili ya wengine; kutoka kwa watu walioko kwenye maombolezo na huzuni hadi  wale ambao kwa tabasamu rahisi na neno zuri, wameleta faraja kwa wale wanaohitaji; kutoka kwa wale hasa wanawake, ambao wamepata unyanyasaji nyumbani kwa sababu ya kufungwa kwa nguvu, hadi wale ambao wanataka kuanza tena ile kasi ya maisha ya kila siku kwa shauku. Mama wa Msaada, utupokee chini ya vazi lako na utulinde, utuunge mkono katika saa ya jaribio na uwashe nuru ya matumaini ya siku zijazo mioyoni mwetu”.

Familia,wazee na vijana waliomgeukia Mama

Pamoja na Papa kanisani  hawa walikuwa ni wanawake na wanaume, vijana, wasichana na wavulana kutoka parokia za Roma na Lazio, pamoja na wawakilishi wa vijana wa Harakati Mpya za Uinjilishaji, ambao walisali Salamu Maria  hamsini, baada ya utangulizi wa  kusoma Matendo ya Utukufu. Kwa kadiri ilivyo kuwa na uwepo wa waamini ndivyo watu waliitikia na walimwomba Mama Maria. Baba Mtakatifu Francisko alikaa mbele ya altare akiwa na rosari mikononi anasali kwa ajili ya ulimwengu wote uliojeruhiwa na virusi. Mwisho wa Rosari wimbo wa tunakimbilia ulinzi wako  ewe  Mama wa Mungu, uliimbwa ukifuatia na Litania. Papa Francisko alirudia tena kuomba Mama kwa ajili ya hali halisi ya janga na karibu kwa mateso na huzuni  ambao unakatisha ulimwengu mzima. “tunakimbilia Wewe Mama wa Mungu na mama yetu, tunakimbilia chini ya ulinzi wako. Aliomba wafarijiwe wale waliopotea na kulia kwa ajili ya wapendwa wao waliokufa, wakati mwingine wamezikwa kwa njia inayoumiza roho, ameomba msaada kwa Mama  kwa ajili ya wale wanaofadhaika, kwa ajili  ya watu wagonjwa ambao wanaweza kuzuia kuambukiza na hawawezi kukaa karibu. Awatie imani wale ambao wana wasiwasi juu ya siku zijazo zisizo na uhakika na athari kwa uchumi na kazini.

Maombi ili kuwepo na roho ya mshikamano

Papa Francisko bado amemwomba Mama Maria  kulinda na kuwapa nguvu wale wote ambao kwa njia mbalimbali katika kipindi hiki cha dharura wako mstari wa mbele na wanaweka maisha yao hatarini kuokoa maisha mengine, amewakumbuka pia wale wanaowajali wagonjwa, mapadre na watu waliowekwa wakfu ambao, kwa wasiwasi wa kichungaji na kujitoa kwa Injili, wanatafuta kusaidia na kusaidia kila mtu. Ombi hilo pia limewaendae wanasayansi na watawala ili  roho ya udugu iweze kukua ulimwenguni:

“Bikira Mtakatifu, angaza akili za wanaume na wanawake wa sayansi, ili wapate suluhisho sahihi za kushinda ugonjwa huu virusi. Saidia viongozi wa mataifa kufanya kazi kwa hekima, wasiwasi na ukarimu, kusaidia wale wanaotuma kinachohitajika ili kuishi, kupanga suluhisho za kijamii na kiuchumi kwa kuona mbali na roho ya mshikamano. Mtakatifu Maria, gusa dhamiri ili pesa nyingi za kutumika kuongezea silaha zipangwe kuhamasisha masomo yanayofaa ili  kuzuia majanga kama hayo kwa  siku za usoni yasitokee. Mama mpendwa, hufanye kukua hisia ya kuwa wa familia moja kubwa ulimwenguni, katika ufahamu wa kifungo kinachounganisha kila mtu kwa sababu ya roho ya kidugu na kuunga tunaweza kusaidia umaskini na hali nyingi za shida. Tunaomba utie moyo uthabiti wa imani, uvumilivu katika kuhudumia na  kudumu katika kuomba”.

Baraka za Papa kwenye mataji 30 ya Rozari

Kama ishara ya muungano wa sala, Papa Francisko amebariki rosari ambazo zitatumwa kwenye madhabahu 30 ambazo zimechaguliwa kuongoza sala ya Rosari katika Nchi mbali mbali na ambapo katika sala hizo waamini wanaweze kuungana wote kupitia vyombo vya habari. Mwishowe, Papa Francisko aliwapa kila mtu baraka na akiongozana na Askofu Mkuu  Rino Fisichella, rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, ambaye ana jukumu la kuandaa mpango huo ulimwenguni, waliondoka kwenye Kanisa Kuu. Hata hivyo ikumbukwe, atakuwa ni Papa Francisko tena mnamo tarehe 31 Mei ijayo atakayehitimisha  marathon ya maombi, ambapo anatarajiwa sala ya rosari katika Bustani za Vatican mahali ambapo kuna groto ya Bikira Maria wa Lourdes.

02 May 2021, 14:43