Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa PMS yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 200 ya uinjilishaji na ushuhuda wa imani sehemu mbalimbali za dunia. Ni muda wa kuimarisa umoja na mshikamano. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa PMS yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 200 ya uinjilishaji na ushuhuda wa imani sehemu mbalimbali za dunia. Ni muda wa kuimarisa umoja na mshikamano. 

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa Miaka 200 ya Imani na Uinjilishaji!

Tarehe 3 Mei 1922 Papa Pio XI akazipatia kazi zake za kitume, hadhi ya kuwa ni Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa na Makao yake makuu kuhamishiwa mjini Roma. Mtakatifu Yohane XXII akamtangaza Pauline-Marie Jaricot kuwa Mtumishi wa Mungu tarehe 25 Januari 1963. Kumbe, Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa sasa yanajiandaa kuadhimisha miaka 200 ya uinjilishaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni mtandao wenye sura na tamaduni nyingi, changamoto na mwaliko ni kuhakikisha kwamba, imani ya Wakristo inatangazwa na kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni vyombo vya Injili ya huruma na upendo inayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa anasema: kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ni dhamana na utume wa Mama Kanisa unaokwenda kinyume kabisa cha wongofu wa shuruti unaoweza kutekelezwa kwa njia za: kisiasa, kitamaduni, kisaikolojia au kidini. Kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ni zawadi ya bure ambayo Roho Mtakatifu amelikirimia Kanisa lake na wala si matokeo ya nia au tafakari zinazofanywa na watu binafsi. Kupokea furaha inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu ni neema na nguvu ya pekee inayowawezesha waamini kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa.

Wokovu ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake kwa kukutana na ufunuo wa Uso wa Kristo Yesu, anayewaita waja wake, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa shukrani na furaha ya Injili. Kimsingi, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kama utume kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anafafanua mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika uinjilishaji mpya. Jambo la kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linakuwa na mvuto na mashiko yanayowahamasisha watu wa Mataifa kujiunga nalo na wala Kanisa haliwezi kukua na kuongezeka kwa wongofu wa shuruti. Watu wanapaswa kuguswa na chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Pili, ni moyo wa shukrani na majitoleo pasi na kujibakiza hata kidogo, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa kwa njia ya unyenyekevu kwa kutambua kwamba, mafanikio yanayopatikana si kutokana na jasho au juhudi za wamisionari wenyewe. Kimsingi, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya unyenyekevu na wala hakuna sababu ya “kujimwambafai”.

Mihimili ya uinjilishaji inapaswa kuwa karibu zaidi na watu wanaoinjilishwa, kadiri ya hali na mazingira yao pamoja na kuzingatia ufahamu wa watu wa Mungu “Sensus fidei” pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuna haja ya kukuza na kudumisha karama zinazoweza kuboresha ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa wabatizwa. Hiki ndicho kile kinachoitwa “Sensum fidei” yaani “Ufahamu ya waamini” unaofumbatwa katika msingi wa sala na matendo ya huruma. Katika muktadha huu, waamini walei wamekuwa wakiheshimiwa sana na Mama Kanisa, kwa kutambua mchango na ushiriki wao wa kawaida katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Huu ni mtandao unaopaswa kukuzwa na kudumishwa ili kuonesha utajiri unaobubujika kutoka kwa watu wenye mawazo na mitazo tofauti.

Padre Tadeusz J. Nowak, OMI, Katiku mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari “The Pontifical Mission Society” (Pontificium Opus a Propagatione Fidei) anasema, tarehe 3 Mei 2022 Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa yatakuwa yanaadhimisha kilele cha miaka 200 tangu kuanzishwa kwayo. Papa Pio wa XI katika Barua yake Binafsi, “Motu Proprio Romanorum Pontificum” alikazia sana ari na mwamko wa shughuli za kimisionari katika mchakato wa uinjilishaji. Huo ukawa ni mwanzo wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa. Mtumishi wa Mungu Pauline-Marie Jaricot ndiye muasisi wa utume huu wa kimisionari, dhamana aliyoitekeleza kwa muda wa miaka 15 bila kuchoka! Aliteseka sana kiroho na kimwili, lakini akaimarishwa kwa Sakramenti za Kanisa sanjari na mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na sadaka ya maisha yake. Mtumishi wa Mungu Pauline-Marie Jaricot akajipambanua katika huduma kwa Mungu na jirani maskini na wagonjwa. Ni huduma iliyotolewa kwa njia ya sala kwa ajili ya toba na wongofu wa watu kwa njia ya uinjilishaji ulimwenguni. Alitamani sana kuona Kristo Yesu anapendwa kuliko jambo lolote hapa duniani, kama Kristo Yesu alivyowapenda waja wake, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake ili kuwaokoa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ari na moyo wake wa kimisionari bado unaendelea kupenya sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya misaada ya hali na mali katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Tarehe 26 Mei 2020, Baba Mtakatifu Francisko alitambua na kuidhinisha muujiza uliofanyika kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu Pauline-Marie Jaricot. Padre Tadeusz J. Nowak, OMI, Katiku mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari anasema, waamini wanasubiri kwa hamu kusikia ni lini Mtumishi wa Mungu Pauline-Marie Jaricot atatangazwa kuwa ni Mwenyeheri na hatimaye, Mtakatifu. Itakumbukwa kwamba, alizaliwa tarehe 22 Julai 1799 huko Lione, Ufaransa na kuitupa mkono dunia hapo tarehe 9 Januari 1862. Tarehe 3 Mei 1922 Papa Pio XI akazipatia kazi zake za kitume, hadhi ya kuwa ni Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa na Makao yake makuu kuhamishwa kutoka Lione, Ufaransa hadi mjini Roma. Mtakatifu Yohane XXII akamtangaza Pauline-Marie Jaricot kuwa Mtumishi wa Mungu tarehe 25 Januari 1963. Baba Mtakatifu Francisko anayataka Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuondokana na dhana ya kutaka kujitafuta yenyewe, kwa ajili ya kujiendeleza, hali ambayo inaweza kufananishwa na watu “wanaotaka kujipigia debe ili kukuza shughuli zao kwa mafao yao binafsi”.

Viongozi wa Mashirika haya waondokane na uchu wa madaraka kwa kutaka kuamrisha kila jambo, bali watambue kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya watu wa Mungu na wala si vinginevyo! Ubaguzi na tabia ya kuwatenga watu kwa misingi ya matabaka yao, ni jambo ambalo linapaswa “kufyekelewa mbali” katika maisha na utume wa Kanisa. Viongozi wasitafute vigezo vya ufanisi wa mambo ya kidunia. Mashirika haya yawe mstari wa mbele katika sala sanjari na kukusanya fedha kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii ni huduma muhimu kwa ajili ya utume wa Makanisa mahalia, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari. Kuna haja ya kurahisisha miundombinu ya utume huu. Baba Mtakatifu anasema, ni marufuku kwa viongozi kuyageuza Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuwa kama asasi za kujitegemea, kwa kujikita katika mchakato wa ukusanyaji wa fedha. Dhamana na wajibu wa kuchangia shughuli mbali mbali za kimisionari iko mikononi mwa wabatizwa wote. Fedha inayokusanywa, isaidie kugharimia mahitaji msingi ya Kanisa mahalia na kuondokana na mtindo wa kutaka kuligeuza Kanisa kuwa kama “chombo cha kuwanyonya watu”. Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Wakati huo huo, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, amemteua Mheshimiwa Padre Dinh Anh Nhue Nguyen kutoka Vietnam, kuwa Katibu wa Umoja wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa “Pontifical Missionary Union” na ameanza kazi rasmi kuanzia Mei Mosi, 2021. Padre Dinh Anh Nhue Nguyen anachukua nafasi ya Padre Fabrizio Meroni aliyemaliza muda wake wa huduma mjini Vatican hapo tarehe 31 Machi 2021. Padre Fabrizio Meroni ametumia fursa hii kuwashukuru wakurugenzi wote wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kutoka sehemu mbalimbali za dunia walioshirikiana naye katika kipindi cha uongozi wake!

PMS Miaka 200
06 May 2021, 15:12