Papa Francisko Jinsi ya Kukabiliana na majanga na maafa asilia: Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza. Pili ni kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu! Papa Francisko Jinsi ya Kukabiliana na majanga na maafa asilia: Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza. Pili ni kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu! 

Jinsi ya Kukabiliana na Majanga: Mungu Kwanza, Pili: Udugu na Utu

Papa anasikitika kusema kwamba, usiku ule wa tetemeko walipoteza kila kitu pamoja na Mwenyezi Mungu na udugu wa kibinadamu. Lakini, mambo haya mawili yamekuwa ni chachu muhimu sana ya kuanza upya kwa ujasiri mkuu. Wameishi kwenye makazi ya muda na baada ya miaka kumi, wamerejea tena katika Monasteri yao ambayo imejengwa na kukarabatiwa vizuri zaidi! Maafa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kesha la Pasaka ni Usiku Mtakatifu ambao Mama Kanisa amekuwa akiuadhimisha kwa heshima kuu kadiri ya Mapokeo yake. Ni Usiku wenye utajiri mkuu wa maisha ya kiroho, mwaliko kwa waamini kuendelea kukesha huku wakisubiri ujio wa pili wa Yesu Kristo, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na kwamba, ufalme wake hauna mwisho. Usiku wa Pasaka ni kielelezo cha waamini kuvuka kutoka katika dhambi na mauti na kuanza hija ya maisha mapya katika Kristo Mfufuka. Katika Kesha la Pasaka, Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka, aliyeshinda dhambi na mauti, ndiyo maana Mama Kanisa anathubutu kuimba sifa za Mshumaa wa Pasaka “Exultet” Yaani Mbiu ya Pasaka. Watawa wa Shirika la Waklara wa Paganica, AQ, nchini Italia, wamekuwa ni msaada mkubwa wa sala kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko na katika maadhimisho ya Mkesha wa Pasaka kwa Mwaka 2021, ndio waliotoa zawadi ya Mshumaa wa Pasaka unaotumiwa katika Kipindi cha Pasaka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo makini cha Kristo Yesu Mfufuka na Yesu ambaye pia ni Mwanga wa Mataifa.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 26 Aprili 2021 amekutana na kuzungumza na Watawa wa Shirika la Waklara wa Paganica, AQ, nchini Italia. Watawa hawa wanatoka katika eneo la Aquila, ambalo tarehe 6 Aprili 2009 lilikumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha watu 309 kupoteza maisha, watu wengine 1,600 kujeruhiwa vibaya na watu 80, 000 wakabaki bila makazi maalum baada ya nyumba zao kubomolewa na kutofaa tena kwa matumizi ya binadamu. Monasteri ya watawa hawa nayo ilibomoka na hivyo kupelekea kifo cha Mama mkuu wa Shirika Gemma Antonucci pamoja na kusababisha majeraha makubwa kwa watawa wengine. Mbele ya macho yao, wakaliona fumbo la kifo likiwanyemelea; wakaonja mateso na mahangaiko makubwa, lakini mwishoni waliweza kuonja upendo wa Baba wa mbinguni kwa njia ya udugu wa mshikamano uliooneshwa na watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, usiku ule wa tetemeko walipoteza kila kitu walichokuwa nacho, pamoja na Mwenyezi Mungu na udugu wa kibinadamu. Lakini, mambo haya mawili yamekuwa ni chachu muhimu sana ya kuanza upya kwa ujasiri mkuu. Wakaanza kuishi katika makazi ya muda na baada ya miaka kumi tangu maafa yale yalipotokea, wamerejea tena katika Monasteri yao ambayo imejengwa na kukarabatiwa vyema.

Leo hii, Jumuiya hii inaendelea kuchanua kwa kuwa na watawa vijana kumi na wawili. Ujumbe, mahususi kwa watu wote walioguswa na kutikiswa na maafa makubwa na kwamba, daima wanapaswa kuanza na Mwenyezi Mungu kwa kujikita katika mshikamano wa kidugu. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kutoa kipaumbdele kwa Mungu na mshikamano wa udugu. Anawahimiza waendelee kusali na kujisadaka kwa ajili ya watu wanaoteseka kutokana na madhara makubwa yaliyosababishwa na tetemeko la mwaka 2009. Kuna watu bado wanahitaji faraja pamoja na kuwatia shime, ili waweze kusonga mbele. Mwenyeheri Antonia awasaidie ili waweze kuwa kweli ni watawa wa shoka wanaoshuhudia ufukara, lakini wakiendelea kudemka kwa furaha na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, kielelezo makini cha ufukara. Mwishoni wa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewataka watawa hawa waendelee kuwa waaminifu kwa karama waliyorithishwa kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi na Mtakatifu Clara, daima waendelee kujibu kwa ukarimu, ile hamu ya wito wao ambayo imepandikizwa katika “sakafu ya nyoyo” zao, huku wakiendelea kuishi kwa ukarimu wito wao wa kuwekwa wakfu kwa kujishikamanisha na Injili ya Kristo!

Papa Watawa
26 April 2021, 14:45