Papa Francisko: Familia ni Kanisa Dogo la nyumbani, shule ya upendo, sala, huruma na ukarimu. Papa Francisko: Familia ni Kanisa Dogo la nyumbani, shule ya upendo, sala, huruma na ukarimu. 

Familia Kanisa Dogo la Nyumbani: Shule ya Sala, Huruma na Fadhila

Baba Mtakatifu Francisko anaziombea familia zote, ili Mwenyezi Mungu aweze kuzikirimia Roho wake Mtakatifu, ili kweli ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya sala wanapewa malezi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala, Jumatano tarehe 14 Aprili 2021, amewahimiza waamini kuhakikisha kwamba, Kipindi hiki cha Pasaka, familia zinakuwa ni shule ya sala, ili kugundua na kuonja kwa mara nyingine tena uwepo endelevu wa Kristo Yesu Mfufuka kati pamoja nao!

Kwa njia hii, ataweza kuwakirimia zawadi ya amani, matumaini na furaha ya kweli. Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kupyaishwa kwa njia ya sala, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anaziombea familia zote, ili Mwenyezi Mungu aweze kuzikirimia Roho wake Mtakatifu, ili kweli ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya sala wanapewa malezi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Kwa njia ya imani inayopyaishwa kwa sala, waamini wataweza kugundua nyuso za jirani zao wahitaji, tayari kusikiliza na kujibu kilio chao.

Imani bila sala, anasema Baba Mtakatifu, itazimika kama “Kibatari kisichokuwa na mafuta”. Waamini wajenge utamaduni wa kuchota amana na utajiri wa sala kutoka kwa Mama Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wenye huruma unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kipindi cha Pasaka ni muda muafaka kwa waamini kujiachia na kuzama katika sala kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na Mitume wa Yesu, waliodumu kwa moyo mmoja katika kusali huku wakimngojea Roho Mtakatifu ili aweze kuwashukia na kukaa pamoja nao. Rej. Mdo. 1:14.

Kanisa Dogo

 

 

14 April 2021, 14:57