Tafakari ya Njia ya Msalaba Ijumaa Kuu kwa Mwaka 2021 mjini Vatican imeandaliwa na watoto kutoka Jimbo kuu la Roma. Tafakari ya Njia ya Msalaba Ijumaa Kuu kwa Mwaka 2021 mjini Vatican imeandaliwa na watoto kutoka Jimbo kuu la Roma. 

Tafakari ya Njia ya Msalaba Ijumaa Kuu Iliyotungwa na Watoto Roma

Ni watoto wanaoonesha mateso, mahangaiko pamoja na imani na matumaini ya watu wa Mungu hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya UVIKO-19. Watoto hawa wanaliita janga hili kuwa ni kipindi cha giza nene. Wanasikitika kuona wazazi wao wakirushiana maneno makali na hata kupimana nguvu kwa vipigo na hivyo kushindwa kuzungumza pamoja kwa siku kadhaa bila kupatana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa Kuu tarehe 2 Aprili 2021 majira ya 12: 00 jioni kwa saa za Ulaya, anatarajia kuongoza Ibada ya Ijumaa Kuu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Majira ya saa 3:00 Usiku, kutakuwa na Maadhimisho ya Njia ya Msalaba. Tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2021 imeandaliwa na Chama cha Viongozi na Skauti Wakatoliki Italia: “Associazione Guide e Scouts Cattolici Italiani” kutoka Umbria na Roma, hususan Parokia ya Mashahidi wa Uganda, Jimbo kuu la Roma. Michoro ya Tafakari ya Njia ya Msalaba imechorwa na watoto kutoka Roma wanaotunzwa kwenye nyumba ya “Mater Divin Amoris” pamoja na “Tetto Casal Fattoria”. Ni watoto wanaoonesha mateso na mahangaiko ya binadamu, pamoja na imani na matumaini ya watu wa Mungu hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Watoto hawa wanaliita janga hili kuwa ni kipindi cha giza nene katika maisha ya mwanadamu. Wanasikitika kuona wazazi wao kila kukicha wakirushiana maneno makali na hata wakati mwingine, kupimana nguvu kwa vipigo na hivyo kushindwa kuzungumza pamoja kwa siku kadhaa bila kupatana!

Watoto wanagusia umaskini wa hali na kipato; woga uliowashika kiasi cha kushindwa kuzungumza na kutetea ukweli; wamekuwa jeuri na kushindwa kuwaheshimu na kuwatii wazazi na walezi wao. Wakati mwingine hawajisikii hata kidogo kwenda kuhudhuria Katekesi na Sala. Wanawakumbuka na kuwaombea watoto wenzao ambao bado wanateseka na kufa kwa baa la njaa na utapiamlo; watoto wanaoteketea kutokana na ujinga, maradhi na wale wanaonyonywa kwa kutumbukizwa katika biashara ya binadamu pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Watoto wanaopoteza maisha yao kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Yote haya ni sehemu ya Njia ya Msalaba ya Watoto hawa kwa Mwaka 2021. Kristo Yesu anapohukumiwa kifo, wanajiona hata wao kama Pilato, pale waliposhindwa kusema ukweli kwa kumtetea mwenzao alipokuwa ameshutumiwa kwa uwongo kwamba, alimwibia jirani yake peremende. Watoto hawa wanamwomba Kristo Yesu awasaidie ili wawe mashuhuda na vyombo vya haki. Kristo Yesu anapopokea Msalaba, watoto hawa wanaona nyanyaso na madhulumu yanayoendelea kutendeka sehemu mbalimbali za dunia hata leo hii. Kuna watu wanahukumiwa na kutendewa bila haki. Katika muktadha huu, upendo wa Yesu unakuwa ni jibu na changamoto kwa wale wote wanaoteseka na kudhulumiwa.

Katika Kituo cha Tatu Yesu anaanguka mara ya kwanza. Mtoto mmoja anasema, yeye darasani alikuwa ni gwiji wa mahesabu, lakini siku moja, alikuta karatasi ya mtihani wake ameandikiwa “hafifu”. Anasema alijisikia vibaya sana, akataka ardhi ipasuke ili immeze na wala hakutaka faraja kutoka kwa mtu yeyote yule! Alipowaelezea wazazi wake yaliyomsibu shuleni, wakamfariji, wakamwonesha upendo wa dhati na kumtia moyo ili kujifunza zaidi! Hapo akainuka kutoka “mavumbini”, tangu wakati huo, amekuwa rafiki sana wa hesabu mpaka “zina mgwaya”. Watoto hawa wanawaalika waamini wanapoanguka, waombe msaada kutoka kwa Kristo Yesu, ili awasaidie kunyanyuka tena na kuubeba Msalaba wao na kuwawashia moto wa matumaini. Katika Kituo cha Tano, Yesu anakutana na Mama yake Bikira Maria. Watoto hawa kutoka kwa Mama zao, wameonja huruma, upendo na uwepo wao wa daima katika malezi na makuzi yao. Katika shida na wasiwasi mkubwa, wao wamekuwa ni kitulizo na salama yao. Wamewasikiliza na kuwashirikisha tabasamu la kukata na shoka. Katika shida na mahangaiko makubwa, wanasema watoto hawa kwamba, wanakosa maneno, kumbe inatosha tu kumwangalia Mama na faraja inapatikana.

Kituo cha Tano, Simoni wa Kirene anamsaidia Kristo Yesu kubeba Msalaba. Mtoto mmoja anasema, wao walipenda sana kucheza, lakini kulikuwa na mtoto jirani kwao, aliyetamani kucheza nao, lakini hakupata nafasi na daima aliwachungulia walipokuwa wakicheza na kubaki akiwa katika hali ya upweke na majonzi! Kwa ufupi, hakuwa na ujasiri wa kuomba kujiunga kucheza pamoja nao. Siku moja, mtoto huyu alivunja ukimya na kumwendea yule jirani yake na kumkaribisha ili wacheze pamoja. Jina lake lilikuwa ni Walid, akakubali na kweli uwanjani “akaonesha vitu vyake”! Alikuwa anafahamu kusakata kabumbu hadi unamvulia kofia! Lakini alikuwa ni mlinda mlango wa kutupwa! Tangu wakati huo, wamekuwa marafiki, huu ni mwaliko wa kuwafungulia wengine hazina ya nyoyo zao na kuwakaribisha. Kituo cha Sita, Veronika anapangusa Uso wa Yesu. Mtoto mmoja anasema, darasa lake lilijiandaa kwa mchezo wa fainali ya mpira wa miguu. Na kwa mara ya kwanza, alimwona rafiki yake aliyekuwa anaitwa Marko! Lakini huyu hakuwa ni mshabiki sana wa mpira! Siku hiyo walikung’utwa sana kwa “kipigo cha mbwa koko”. Mpira ulipomalizika kwa uchungu walitoka nje na hapo akakutana na yule rafiki yake Marko akiwa amebeba chungwa mkononi mwake. Ni ule muda na chungwa lile anasema, vilivyomsaidia kukubali kushindwa na hivyo kupangusa aibu iliyokuwa imetanda usoni pake!

Kituo cha Saba, Yesu anaanguka mara ya pili kwa kuelemewa na uzito wa Msalaba. Mtoto mmoja anasema, alijiandaa barabara ili kuhakikisha kwamba, anapewa nafasi ya kughani shairi lake mwishoni mwa mwaka wa masomo! Kwa bahati mbaya, hakuchaguliwa na badala yake fursa hii akapewa mwanafunzi ambaye hakufikiriwa hata mara moja. Mwanafunzi huyu aliitwa Giovanni, lakini mwisho wa siku, alifanya vizuri, kiasi kwamba, kila mtu pale darasani aliridhika kwa mafanikio haya makubwa. Mtoto huyu anapotafakari kwa kina anasema, kuanguka kwake “chali kama mende” kumemwezesha mwanafunzi mwingine, kuonesha vipaji na karama alizojaliwa na Mwenyezi Mungu. Kwa hakika, Giovanni alihitaji nafasi hii, kushuhudia karama zake. Kila mtu anapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu. Kituo cha Nane, Akina mama wanamlilia Yesu! Kuna watoto wawili siku moja walicheza na kusahau kufanya kazi ya nyumbani “Home Work”. Na mama yao alipowaulizia wote wakasema kwa ujasiri kwamba, walikuwa wametekeleza wajibu wao, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, hawakuwa wametimiza wajibu wao. Jambo hili lilimtesa sana yule kaka mkubwa, kiasi cha kuacha yote na kwenda chumbani kuanza kujisomea. Mdogo wake, kesho yake, hakuweza kuamka kwa madai kwamba, alikuwa anasumbuliwa na tumbo! Kaka mtu aliporejea kutoka shule, alizungumza na mdogo wake na kukubaliana kimsingi kwamba, wamekosea sana kumdanganya mama yao. Akamsaidia mdogo wake, kufanya ile kazi na ikamalizika kwa wakati na wakaendelea na michezo. Kumrekebisha ndugu yako ni vigumu sana, lakini ni jambo muhimu linalohitaji ujasiri, umakini pamoja na kujali. Waamini warekebishane kwa huruma na upendo!

Kituo cha Tisa, Yesu anaanguka mara ya tatu! Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, limesababisha madhara makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu. Waathirika wakuu katika masuala ya kijamii ni watoto na wazee. Wajukuu wanashindwa kuwatembelea mababu na bibi zao! Shule zimefungwa, hawawezi kukutana na kucheza na watoto wenzao! Kwa hakika watoto hawa wanasema, wanajisikia kuanguka chini, huku wakielemewa na upweke kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu. Wanamwomba, awakirimie mwanga angavu, ili waweze kusonga mbele wanapotumbukia katika giza la mawazo! Kituo cha Kumi, Yesu anavuliwa nguo! Watoto wametumia fursa hii, kuwakumbuka watoto wenzao wanaoteseka kutokana na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii. Mshikamano na udugu wa kibinadamu, unaweza kuwasaidia watoto kuwa wamisionari kwa watoto wenzao wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali. Jambo la msingi ni kujinyima na kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wanaoishi katika mazingira maskini na hatarishi zaidi. Kituo cha Kumi na Moja, Yesu anasulubishwa Msalabani. Watoto wanasema, huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni fursa makini ya kushuhudia furaha, amani na utulivu unaobubujika kutoka kwa watu hawa! Kwa hakika, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa.

Kituo cha Kumi na Mbili, Yesu anakufa Msalabani! Watoto wanajiuliza, inakuaje watu wazima wanafanya vitendo vya mauaji ya kinyama kama yanavyosimuliwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii? Je, katika hali na mazingira ya ukatili mkubwa kiasi hiki, wanahitaji kweli kupewa msamaha? Lakini, waamini wanapaswa kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu kwamba, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko kwa wafu amewakomboa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Wadhambi wanapaswa kutambua ufunuo wa huruma ya Mungu, huku wakiwa na ujasiri wawe tayari kutubu na kumwongokea Mungu! Kituo cha Kumi na Tatu, Yesu anashushwa Msalabani baada ya mateso na kifo chake! Mtoto mmoja anasimulia jinsi ambavyo bibi yake aliyefariki kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 alivyochukuliwa kutoka nyumbani kwao na watu waliokuwa wamevaa mavazi meupe! Hakubahatika kumwona tena, na akafariki dunia huko huko hospitalini katika hali ya upweke! Mtoto huyu anasikitika kwamba, hakuweza kupata nafasi ya kuwa karibu naye, lakini kila siku anamwombea kwa Mwenyezi Mungu, kama njia ya kumsindikiza baada ya kumaliza safari yake huku bondeni kwenye machozi. Kwa hakika Msalaba wa Kristo Yesu, ni chemchemi ya matumaini.

Kituo cha Kumi na Nne, Yesu anazikwa kaburini! Watoto wanasema, wamejifunza kutenda mema kwa niaba ya Kristo Yesu; kuvuka shida na magumu ya maisha kwa kujiaminisha kwake na kuwapenda jirani zao kwa moyo wote kama ndugu zao katika Kristo!. Wanapoanguka, wawe na ujasiri wa kusimama na kuendelea kuhudumia tena jirani zao. Waamini wamwombe Kristo Yesu awaondolee maamuzi mbele na hivyo kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu pamoja na kuunganisha maisha yao! Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni zawadi kubwa kwa binadamu. Ni kielelezo cha upendo usiokuwa na kifani.

Njia ya Msalaba

 

 

31 March 2021, 15:01