Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 28 Februari 2021 ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kutaka wanafunzi 317 waliokuwa wametekwa nyara kuachiliwa mara moja bila masharti. Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 28 Februari 2021 ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kutaka wanafunzi 317 waliokuwa wametekwa nyara kuachiliwa mara moja bila masharti. 

Sala ya Papa Kwa Wanafunzi Waliotekwa Nyara Nigeria

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, aliungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, CBCN., kutaka wanafunzi wa kike 317 waliokuwa wametekwa nyara Ijumaa tarehe 26 Februari 2021, kutoka Shule ya Sekondari ya Jangebe, iliyoko Kaskazini Magharibi mwa Nigeria kuachiliwa huru mara moja ili waweze kurejea na kujiunga na familia zao. Haki za watoto!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe 28 Februari 2021 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, aliungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, CBCN., kutaka wanafunzi wa kike 317 waliokuwa wametekwa nyara Ijumaa tarehe 26 Februari 2021, kutoka Shule ya Sekondari ya Jangebe, iliyoko Kaskazini Magharibi mwa Nigeria kuachiliwa huru mara moja. Baba Mtakatifu aliwaombea wanafunzi hawa, ili waweze kurejea mara moja majumbani mwao. Ameonesha pia uwepo wake wa karibu kwa familia zilizokumbwa na wasi wasi mkubwa kutokana na watoto wao kutekwa nyara na watu wasiofahamika!

Wakati huo huo, viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuanzia kwa Bwana Antònio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye ametaka shule kuheshimiwa kwani hapa panapaswa kuwa ni mahali salama kwa wanafunzi, ili waweze kujifunza pasi wasi wasi wowwote wa kushambuliwa au kutekwa nyara. Utekaji wa wanafunzi Kaskazini mwa Nigeria ni matukio ambayo Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF linasema, ni ukiukwaji wa haki msingi za watoto. Hii ni hali inayowajengea wanafunzi mang’amuzi mabaya ya maisha, kiasi hata cha kuacha makovu ya kudumu katika afya na maisha yao kwa ujumla. Naye Rais Muhammadu Buhari wa Nigeri amesikika akisema kwamba, Serikali yake haitakubali kuchezeshwa “Sindimba” ili kulipa fedha, kusudi wanafunzi hao waachiliwe huru. Baadaye, taarifa kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari imesema kwamba, wanafunzi hao wa kike, waliachiwa huru bila masharti!

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria limeonya kwamba, kuna hatari kwamba, Nigeria ikameguka hivi karibuni kutokana na ukosefu wa ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Viongozi wa Kitaifa wameshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, ili haki iweze kushika mkondo wake. Kuna migogoro na kinzani za kidini na kikabila inayotishia umoja na mshikamano wa kitaifa. Bado janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 linaendelea kuteketeza maisha ya wananchi wengi wa Nigeria. Zote hizi ni dalili za kukosekana kwa utashi wa kisiasa ili kuiwezesha Nigeria kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu sana katika kuendeleza mustakabali wa taifa la Nigeria wanasema Maaskofu.

Nigeria

 

01 March 2021, 14:42