Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: Jubilei ya Miaka 175 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kipapa kwa ajili ya wanafunzi kutoka Ubelgiji. Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: Jubilei ya Miaka 175 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kipapa kwa ajili ya wanafunzi kutoka Ubelgiji. 

Mwaka wa Mtakatifu Yosefu: 2020 - 2021: Fadhila Kuu za Kuzingatia!

Mtakatifu Yosefu alibahatika kuwa na karama ya kupokea, ni Baba Mlinzi na hatimaye, Ni Baba mwenye ndoto! Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, Mtakatifu Yosefu alishinda vishawishi na uasi wote hata kama vilikuwa ni halali katika maisha yake, akapiga moyo konde akampenda na kumpokea Bikira Maria na Mtoto Yesu na hatimaye akawalinda na wakawa salama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa.

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 18 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wanafunzi kutoka Ubelgiji, kinachofanya kumbukizi la miaka 175 tangu kuanzishwa kwake. Hiki ni chuo ambacho kilibahatika kuwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kama mwanafunzi wake. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yosefu ndiye msimamizi wa Chuo hiki cha Kipapa. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha ya Mtakatifu Yosefu. Anasema, huyu ni Baba ambaye alibahatika kuwa na karama ya kupokea, ni Baba Mlinzi na hatimaye, Ni Baba mwenye ndoto! Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, Mtakatifu Yosefu alishinda vishawishi na uasi wote hata kama vilikuwa ni halali katika maisha yake, akapiga moyo konde akampenda na kumpokea Bikira Maria na Mtoto Yesu na hatimaye akawalinda na wakawa salama salimini. Mtakatifu Yosefu hakutafuta sababu yoyote, bali aliyakubali mapenzi ya Mungu katika maisha yake kama kielelezo cha imani. Ni katika mazingira kama haya, Mtakatifu Yosefu anaheshimiwa na Kanisa kama Baba wa mang’amuzi na maisha ya kiroho.

Waamini wanahamasishwa kumkimbilia, pale wanapokumbana na mishale ya mashambulizi, ili kuweza kupokea mapenzi ya Mungu jinsi yalivyo katika maisha. Huu ni mfano bora wa kuigwa kwa Padre anapohamishiwa kwenye Parokia mpya. Jambo la kwanza kwa Padre kama huyu ni kuhakikisha kwamba, anaipenda Jumuiya yake kama ilivyo kwa sababu ameitwa na kutumwa kuihudumia. Kwa kupenda kwa moyo, ataweza kujifunza undani wa maisha ya watu anaowahudumia na hivyo kuweza kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Parokia. Mtakatifu Yosefu ni Baba mlinzi, hali inayoonesha kiini cha wito na utume wake. Dhamana na wajibu huu ulitekelezwa na Mtakatifu Yosefu katika: kimya kikuu, kwa moyo wa unyenyekevu na uaminifu wote hata pale ambapo kwa akili ya binadamu alishindwa kuufahamu mpango wa Mungu. Alijitahidi kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kutekeleza mpango wake katika maisha, na hivyo kuwa na uhuru wa ndani kama mtumishi mwema na mwaminifu anayetamani ustawi na maendeleo ya wale watu ambao Mwenyezi Mungu amemkabidhi!

Dhamana ya kulinda, kama ilivyo kwa kila Padre maana yake ni kuwapenda kwa dhati, watu ambao wamekabidhiwa kwao, kwa kuwatakia mema na furaha, huku wakiwahudumia kwa ukarimu mkuu. Kulinda ni maelekeo ya ndani yanayomwezesha mwamini kuwa na dira, mang’amuzi pamoja na kupima hatua ya kuchukua. Lakini daima anapaswa kuwa makini, huku akikesha na kusali. Huu ni mwelekeo wa kichungaji ambapo, kimsingi mchungaji hapaswi hata kidogo kuwatelekeza Kondoo wake! Daima yuko mbele yao kama kiongozi, ili kuwaonesha njia; yuko kati yao ili kuwafariji na anakwenda nyuma yao, ili kuwapokea na kuwasaidia wale wa mwisho. Huu ndio mwelekeo wa maisha na utume wa Kipadre kwa ajili ya Jumuiya aliyokabidhiwa na Mama Kanisa. Anapaswa kuwa ni Mlinzi ambaye yuko tayari kufanya marekebisho kwa kusoma alama za nyakati, bila ya kuwa na shingo ngumu. Mapadre wawe wepesi kukubali mabadiliko katika maisha na utume wao, kwa kuzingatia mahitaji msingi ya jumuiya wanayoiongoza na kamwe wasitumbukie katika kishawishi cha kutaka kutawala na hivyo kushindwa kutoa huduma makini!

Mtakatifu Yosefu alikuwa ni Baba mwenye ndoto, akabahatika kuwa na upeo mpana kwa kuona mbele zaidi ya kile kilichokuwa kinaonekana machoni! Huu ni mtazamo wa kinabii wenye uwezo wa kuona na kung’amua mpango wa Mungu na lengo linalomsubiri hapo mbeleni. Mtakatifu Yosefu alimwona Bikira Maria kuwa mchumba wake akiwa na Mtoto Yesu. Zaidi sana, aliiona kazi na uwepo wa Mungu katika maisha yake. Akatekeleza dhamana na wajibu wake kama Baba mlishi wa Mtoto Yesu. Kwa kuamini kwake, akashinda hofu na mashaka, akawa ni chombo na shuhuda wa huduma iliyotolewa kwa ukarimu bila kuchoka na zaidi katika hali ya kimya kikuu! Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuwa na ndoto ya upendo kwa jumuiya, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili kuilinda na kuiendeleza, ili kuleta toba na wongofu wa ndani; kwa kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, ili kusaidia jumuiya kukua katika safari ya wafuasi wanaosukumwa na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, anawahimiza kugundua ndani mwake, moyo wa sala, utume na unyenyekevu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu, huku wakionesha utii na ubunifu. Mapadre wajifunze sanaa ya Ubaba inayotekelezwa katika jumuiya sanjari na huduma za kichungaji watakazokabidhiwa na Mama Kanisa kwa siku za usoni!

Mtakatifu Yosefu
18 March 2021, 16:37