Baba Mtakatifu Francisko amezindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya familia: 19 Machi 2021 hadi tarehe 26 Juni 2022: Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu. Baba Mtakatifu Francisko amezindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya familia: 19 Machi 2021 hadi tarehe 26 Juni 2022: Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu. 

Papa: Uzinduzi wa Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye ufunguzi huu, amekazia zaidi kuhusu umuhimu wa Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, Utume wa familia katika kutangaza na kushuhudia ukweli wa maisha ya ndoa na familia, Injili ya familia, familia kama alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu na familia katika changamoto ya UVIKO-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2021, Mama Kanisa amezindua Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Kama sehemu ya maadhimisho haya, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, Taasisi ya Kipapa ya Yohane Paulo wa II ya Sayansi ya Ndoa na Familia pamoja na Jimbo kuu la Roma, wamefanya mkutano kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii pamoja na kusikiliza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika uzinduzi wa Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye ufunguzi huu, amekazia zaidi kuhusu umuhimu wa Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, Utume wa familia katika kutangaza na kushuhudia ukweli wa maisha ya ndoa na familia, Injili ya familia, familia kama alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu na familia katika changamoto ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Baba Mtakatifu anasema, Wosia huu wa kitume “Amoris laetitia” ni dira na mwelekeo wa shughuli za kichungaji katika mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo katika maisha ya ndoa na familia. Kanisa linapaswa kuwa na mtazamo mpya kuhusu ndoa na familia, kwa kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na kwamba, Kanisa kwa namna ya pekee kabisa linapaswa kuwa ni kinga wa uzuri sanjari na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; kwa kuhudumia familia kwa huruma na upendo katika udhaifu wake, sanjari na kujitahidi kuganga na kuponya majeraha yake. Mambo haya msingi ni kiini cha sera na mikakati ya utume wa familia: ukweli wa Injili ya familia unaopaswa kutangazwa na kushuhudiwa pamoja na kuendelea kuzisindikiza familia ili ziweze kutekeleza maisha na utume wake ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wana ndoa na familia wanapaswa kuelewa dhana ya upendo ndani ya familia kuwa ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu na Agano kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake, daima Kanisa likiendelea kupyaisha mafundisho yake kwa kusoma alama za nyakati, ili kuwa na mwelekeo mpya hata katika masuala ya ndoa na familia.

Hii ni fursa makini ya kuvunjilia mbali mahusiano tenge ndani ya familia yanayowafanya baadhi ya wanandoa kuwa watumwa wa hisia zao, kwa kushindwa kutekeleza dhamana na nyajibu zao na matokeo yake ni kutamalaki kwa ubinafsi, woga na wasiwasi kwa yale yanayokuja huko mbeleni. Kanisa linapenda kutangaza na kushuhudia kwamba tunu msingi za ndoa na familia ni sehemu ya mradi wa Mungu kama zawadi na neema inayowataka wanandoa kuishi kwa uaminifu, kwa kujitosa bila ya kujibakiza pamoja na kuendelea kuwa ni sadaka kwa mwenza wao wa ndoa. Katika hija ya maisha ya wanandoa kuna nyakati za kuteleza na kuanguka chari! Kuna nyakati za mabadiliko, ili waweze kuanza tena mchakato wa utimilifu wa furaha na mahusiano yao ya kijamii, ili kweli waweze kuwa ni chachu ya udugu wa kibinadamu na mapendo ndani ya jamii. Kanisa linaishi katika ukweli wa kihistoria, ambao ni Mwalimu wake hata wakati linapotangaza na kushuhudia Injili ya familia, kwa kuzingatia hali halisi ya maisha ya watoto wake, katika ndoa na familia, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa wanazokabiliana nazo katika maisha.

Kongamano la uzinduzi wa Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” limeongozwa na kauli mbiu “Upendo wetu katika maisha ya kila siku”. Huu ni upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa ndoa na familia. Hii ni Injili ya familia inayokita mizizi yake katika Mafundisho tanzu ya Kanisa na wala si kama jambo la kuwalazimishia watu au kanuni maadili “zilizoshuka kutoka mbinguni”. Mama Kanisa anawahimiza viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanasikiliza kwa makini wanandoa na familia; wanawaongoza na kubariki jitihada zao katika maisha, huku wakitembea nao hatua kwa hatua, ili upendo wa familia uweze kupenya zaidi na hivyo kuwawezesha kutambua kwamba, Kanisa liko na linatembea pamoja nao na kwamba, kwa msaada wa Kanisa, Mwenyezi Mungu anapenda kuwasaidia wanandoa kuhifadhi zawadi hii kubwa ambayo wameipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, kwa kuwasindikiza wanandoa sanjari na kuwahudumia wakati wa raha na shida ili waweze kuitikia vyema wito na utume wao, huku wakitambua mahusiano na mafungamano yaliyopo kati yao kwamba, yanapata chimbuko lake katika Upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, Wosia huu wa kitume “Amoris laetitia” ni “Neno hai” linalokita mizizi yake katika upendo wa Mungu, unaotangazwa ulimwenguni kwa ajili ya walimwengu. Wanandoa wanaunganishwa pamoja kama wazazi, watoto na ndugu wamoja kama kielelezo makini cha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Lugha hii inapaswa kunafsishwa katika maneno na matendo, ili watoto waweze kujifunza upendo unaobubujika kutoka katika shule ya familia. Ni katika muktadha huu, familia inakuwa ni mahali pa kurithisha imani kati ya kizazi kimoja kwenda kwa kizazi kingine. Ni mwaliko wa kuratibu kinzani na mipasuko ya kifamilia, ili kweli familia iweze kuwa ni shule ya upendo, amani na ukarimu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika kipindi hiki cha janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, familia nyingi zimeathirika sana kisaikolojia, kiuchumi na kiafya. Lakini familia zimekuwa ni ngome thabiti na rejea kwa watu wengi sehemu mbalimbali za dunia. Familia ni taasisi ambayo haina mbadala katika Jumuiya ya binadamu na jamii katika ujumla wake. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kujizatiti katika kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Waamini waliendee fumbo la upendo wa Mungu kwa uchaji, ari na moyo mkuu. Watu wajitahidi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii ndani ya familia, kati ya wazazi, watoto na mababu na mabibi zao, ili watu waweze kuishi vyema na kuwawezesha wanadamu kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu. Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni fursa nyingine tena ya kusoma, kutafakari na kumwilisha wosia uliotolewa humo. Ni wakati wa kukuza na kudumisha majadiliano kati ya Taasisi ya Kipapa ya Yohane Paulo wa II ya Sayansi ya Ndoa na Familia na taasisi nyingine za elimu, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Lengo ni kukazia kwa namna ya pekee kabisa: Utu, maisha ya kiroho na utume kwa ajili ya kuenzi Injili ya familia.

Amoris laetitia
21 March 2021, 16:21