Madhabahu ya Kilima cha Bikira Maria cha Knock nchini Ireland yamepandishwa hadhi na kuwa ni Madhabahu ya Bikira Maria na Ekaristi Takatifu Kimataifa. Madhabahu ya Kilima cha Bikira Maria cha Knock nchini Ireland yamepandishwa hadhi na kuwa ni Madhabahu ya Bikira Maria na Ekaristi Takatifu Kimataifa. 

Madhabahu ya Kilima Cha B. Maria Cha Knock: B. Maria na Ekaristi!

Madhabahu ya Kilima cha Bikira Maria cha Knock ni chimbuko la ari na mwamko wa kimisionari. Ni kitovu cha imani ambayo, familia nyingi zimejitahidi kuimwilisha kwa watoto wao, kwa kukuza na kudumisha Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi. Ni mahali ambapo sala na tafakari ya kina, vimepewa msukumo wa pekee katika maisha ya waamini nchini Ireland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Madhabahu ni maeneo yanayodhihirisha ufunuo wa: ukuu, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake, mafundisho msingi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Hapa kipaumbele cha kwanza ni uwepo wa Mungu ndani ya Kanisa na maisha ya kila mwamini. Mwenyezi Mungu ndiye anayepanga na kuamua mahali na muda wa kujifunua kati ya waja wake! Waamini wanapaswa kubaki katika ukimya ili kumsikiliza Mungu kwa makini, pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati kwa njia ya matukio mbali mbali, yanayoweza kusaidia mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Sera na mikakati ya uinjilishaji haina budi kumwilishwa katika shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Makanisa mahalia! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, mila na tamaduni njema za watu mahalia zinaheshimiwa na kuendelezwa, kama sehemu ya mchakato wa utamadunisho. Taalimungu ya watu mahalia inayojionesha kwa namna ya pekee katika ibada ya waamini na hasa maskini inapaswa kukuzwa na kudumishwa. Waamini wasaidiwe kufanya hija itakayowasaidia ugundua na kupyaisha tena imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Nyenzo zinazopaswa kuzingatiwa hapa ni: sala na hapa waamini wajizoeshe kusali na kuimba Zaburi sanjari na maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho. Ikumbukwe kwamba, mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unarutubishwa kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Madhabahu pawe ni kimbilio la maskini wa: kiroho na kimwili; pawe ni mahali ambapo mwamini anatambua na kuonja nguvu ya Mungu inayoganga, inayoponya na kuokoa! Hivi karibuni, Vatican imetambua rasmi Madhabahu ya Kilima cha Bikira Maria cha Knock, nchini Ireland “The Sanctuary of Our Lady of Knock” kuwa ni Madhabahu ya Bikira Maria na Ekaristi Takatifu Kimataifa. Tukio hili limeadhimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria hapo tarehe 19 Machi 2021. Tukio ambalo limenogeshwa kwa ujumbe wa video kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Hapa ni mahali ambapo waamini wameonja, wema, huruma, msamaha na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya huduma ya upatanisho na upendo.

Madhabahu haya yanapata chimbuko lake, tarehe 21 Agosti 1879, yaani miaka 142 iliyopita, Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu pamoja na Mwinjili Yohane, walipowatokea waamini katika eneo hili. Tangu wakati huo, waamini wengi kutoka Ireland wamejisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili sehemu mbalimbali za dunia na waamini walei wamekuza na kudumisha Ibada hai kwa Bikira Maria. Vatican imetangaza tukio hili wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani, Jimbo kuu la Dublin nchini Ireland, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia, furaha ya ulimwengu” alitembelea na kusali kwenye Madhabahu haya. Ni maadhimisho yaliyoanza kutimua vumbi tarehe 21 hadi 26 Agosti 2018. Ni katika muktadha huu Baba Mtakatifu alipotembelea Madhabahu haya, akaamua kuyapatia hadhi ya Kimataifa, kama chemchemi ya imani, maboresho ya maisha ya kiroho na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya tarehe 19 Machi 2021 amekazia zaidi: Ari na mwamko wa kimisionari, ukimya katika maisha ya sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na Ibada kwa Bikira Maria. Tangu tarehe 21 Agosti 1879 Bikira Maria alipowatokea waamini wanaozunguka Madhabahu ya Kilima cha Bikira Maria cha Knock, nchini Ireland, hapa pamekuwa ni chimbuko la ari na mwamko wa kimisionari, kwa mapadre na watawa kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili sehemu mbalimbali za dunia.

Hapa pamekuwa ni kitovu cha imani ambayo, familia nyingi zimejitahidi kuimwilisha kwa watoto wao, kwa kukuza na kudumisha Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi. Ni mahali ambapo sala na tafakari ya kina, vimepewa msukumo wa pekee katika maisha ya waamini nchini Ireland. Hapa tafakari na sala katika kimya kikuu ni tunu muhimu sana katika imani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ukimya katika Fumbo la maisha ya sala, kwa kutambua kwamba, katika ukimya, wanasindikizwa na upendo wa Kristo Yesu, ambaye amejisadaka Msalabani kama Mwanakondoo wa Mungu, kwa ajili ya wokovu wa binadamu wote kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kimya kikuu, kinawasaidia waamini kutambua na kuthamini maana ya Fumbo la Upendo, linalowachangamotisha kujiaminisha katika mapenzi na huruma ya Mungu. Ni katika hali ya ukimya, waamini wanaweza kuingia katika undani wa maisha yao na kusali mbele ya Baba yao aliye sirini, anayeona yale yaliyoko sirini anawajazi kadiri ya wema na huruma yake.

Baba Mtakatifu anasema, ameamua kuyapandisha Madhabahu ya Kilima cha Bikira Maria cha Knock, nchini Ireland “The Sanctuary of Our Lady of Knock” kuwa ni Madhabahu ya Bikira Maria na Ekaristi Takatifu Kimataifa. Hii ni dhamana nyeti na tete sana inayowataka uwajibikaji mkubwa. Ni katika muktadha huu, waamini watapaswa kuonesha wema na ukarimu kwa mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakaofika mahala hapa kwa sala na ibada. Hawa ni watu wanaopaswa kutambuliwa kama ndugu wamoja, wanaokuja kushirikishana ule udugu na moyo wa sala. Ukarimu huu, uwe ni ushuhuda wa kupokea Neno la Mungu na neema ya Roho Mtakatifu inayowaimarisha waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, liwe ni daraja linalowaunganisha waamini na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu ni mwamba wa wito wa umisionari wa kitume. Ni kwa njia hii, waamini wanahamasishwa na Kanisa kuwa ni mahujaji wa Injili ya Kristo Yesu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaombea waamini wote ulinzi, tunza na faraja kutoka kwa Bikira Maria.

Madhabahu Knock
21 March 2021, 15:54