Juma Kuu Mama Kanisa anaadhimisha Mafumbo Makuu ya Wokovu wa Mwanadamu: Alhamisi Kuu: Daraja Takatifu, Ekaristi na Huduma ya Upendo, Ijumaa Kuu: Mateso na Kifo cha Kristo! Jumamosi kuu, Kesha kuu! Juma Kuu Mama Kanisa anaadhimisha Mafumbo Makuu ya Wokovu wa Mwanadamu: Alhamisi Kuu: Daraja Takatifu, Ekaristi na Huduma ya Upendo, Ijumaa Kuu: Mateso na Kifo cha Kristo! Jumamosi kuu, Kesha kuu! 

Maadhimisho ya Juma Kuu: Fumbo la Wokovu wa Mwanadamu

Papa: Maadhimisho ya Juma Kuu, iwe ni fursa ya kutafakari Fumbo la Msalaba, ili kuonja wema, huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka katika Msalaba, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waamini wote kwa mshangao mkubwa waweze kusema, “Kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Jumapili ya Matawi, Mateso ya Kristo Yesu, tarehe 28 Machi 2021 umekuwa ni mwanzo wa maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Jumapili ya Matawi, tarehe 28 Machi 2021 amewaambia waamini kwamba, Kristo Yesu alikuwa anaingia Yerusalemu ili kuadhimisha ushindi wa Mungu kwa njia ya Msalaba. Msangao kwa maisha na utume wa Kristo Yesu aliyetangaza: upendo, huruma na msamaha wa Mungu kwa njia ya maisha yake, ulete toba na wongofu wa ndani. Mateso ya Kristo Yesu na kifo cha Msalaba ni kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kumbe kuna uhusiano wa dhati kati ya Matawi ya mitende na Msalaba.

Maadhimisho ya Juma Kuu, iwe ni fursa ya kutafakari Fumbo la Msalaba, ili kuonja wema, huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka katika Msalaba, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waamini wote kwa mshangao mkubwa waweze kusema, “Kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu.” Maadhimisho ya Juma Kuu kwa Mwaka 2021 yanafanyika katika mazingira tete kabisa kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 sehemu mbalimbali za dunia. Haya ni mapambano na adui asiyeonekana kwa macho makavu. Ndiyo maana viongozi mbalimbali wa Kanisa wanasema, hii ni vita inayopaswa kupiganwa kwa kutumia silaha za maisha ya kiroho yaani sala na kufunga. Ni wakati wa kutumia silaha za kisayansi kwa kufuata ushauri na maelekezo ya madaktari na wataalam wa afya. Waamini watumie silaha za kimwili na kijamii ili kujikinga na janga la maambukizi ya Virusi vya Korona, UVIKO-19.

JUMAPILI YA MATAWI. Tarehe 28 Machi 2021, Kanisa lilipaswa kuadhimisha Siku ya XXXVI ya Vijana Ulimwengu katika ngazi ya kijimbo, lakini kutokana na maambukizi makubwa ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, maadhimisho haya sasa yatafanyika katika Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu hapo tarehe 21 Novemba 2021. Wakristo wanakumbuka na kudhimisha siku ile Kristo Yesu alipoingia Yerusalemu kwa shangwe na kulakiwa na maelfu ya watu waliokuwa wakimwimbia kuwa ni Masiha na Mwana wa Daudi, wakimwomba aje kuwaokoa. Hossana maana yake, “Okoa sasa”. Kwa mwaka huu wa 2021, waamini wanamwimbia Kristo Yesu, ili awaokoe kwa namna ya pekee, na janga la maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 linaloendelea kupukutisha maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia.

ALHAMISI KUU. Tarehe 1 Aprili 2021, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu inayopaswa kutolewa kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu, kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Alhamisi kuu, kunaadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki “Mafuta ya Krisma ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu, majira ya Saa 4: 00 Asubuhi kwa Saa za Ulaya, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kubariki: Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa na pamoja na Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu.

Hii ni siku ambamo wakleri wanarudia tena ahadi za utii kwa Askofu mahalia. Ni siku muhimu ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakleri wetu. Alhamisi kuu Jioni, Kanisa linaadhimisha Karamu ya Mwisho, kwa kuweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume waa Kanisa. Ibada ya Misa takatifu mjini Vatican itaanza majira ya saa 12: 000 za jioni kwa saa za Ulaya na yataongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali. Waamini walioandaliwa wataoshwa miguu, kielelezo cha huduma ya upendo, ari na unyenyekevu mkuu hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

IJUMAA KUU: Ulimwengu wote unagubikwa giza la huzuni na majonzi kwa kukumbuka na kuadhimisha: Mateso na Kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Ibada hii ina: Liturujia ya Neno, Ibada ya Kuabudu Msalaba, pamoja na Ibada ya Komunio Takatifu. Msalaba ni Altare ya kwanza ambapo Kristo Yesu aliadhimisha sadaka ya mateso na kifo chake, kielelezo kikuu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Akiwa ametundikwa Msalabani, alichomwa ubavuni kwa mkuki na hapo ikatoka damu na maji, chemchemi ya Sakramenti za Kanisa. Wakristo wanamwabudu Kristo Yesu aliyelazwa hapo Msalabani. Waamini wanakumbushwa kwamba, wasile nyama Siku ya Ijumaa Kuu. Hii ni siku ambayo hakuna maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Katika maadhimisho ya Mwaka huu, 2021, waamini badala ya kubusu Msalaba ishara ya wokovu wa walimwengu watauinamia bila kuugusa. Ikumbukwe kwamba, bado kuna maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kumekuwepo na tafsiri potofu kwamba, kuvaa barakoa kwenye Ibada ya Misa Takatifu ni ukosefu wa imani! Katika mikusanyiko hii mikubwa waamini wachukue tahadhari ya kujilinda wao wenyewe na kuwalinda pia jirani zao.

Majira ya saa 12: 00 za jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuongoza Ibada ya Ijumaa Kuu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Majira ya saa 3:00 Usiku, kutakuwa na Maadhimisho ya Njia ya Msalaba. Tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2021 imeandaliwa na Chama cha Viongozi na Skauti Wakatoliki Italia: “Associazione Guide e Scouts Cattolici Italiani” kutoka Umbria na Roma, hususan Parokia ya Mashahidi wa Uganda, Jimbo kuu la Roma. Michoro ya Tafakari ya Njia ya Msalaba imechorwa na watoto kutoka Roma wanaotunzwa kwenye nyumba ya “Mater Divin Amoris” pamoja na “Tetto Casal Fattoria”. Ni watoto wanaoonesha mateso na mahangaiko ya binadamu, pamoja na imani na matumaini ya watu wa Mungu hasa katika kipindi hiki maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19.

JUMAMOSI MKUU: Hakuna maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa isipokuwa kwa Mpako Mtakatifu wa wagonjwa kwa wale walioko kufani. Mama Kanisa katika Usiku mtakatifu wa Mkesha wa Pasaka, Mama wa mikesha yote kwa sababu ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kanisa katika Kristo Yesu. Kristo Yesu amefufuka kutoka wafu. Kwa kifo chake alishinda mauti, wafu amewapa uzima. Rej. KKK, 638. Mkesha huu ni kiini na chemchemi ya ibada zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Mkesha huu una: Ibada ya Kubariki Moto na Ibada ya Mwanga. Liturujia ya Neno la Mungu ina masomo 7 ya Agano la Kale na 2 ya Agano Jipya. Kuna Liturujia ya Ubatizo ambamo waamini wanarudia tena ahadi zao za Ubatizo pamoja na Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Kumbe, maadhimisho ya Juma Kuu yana uzito wa pekee sana katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kuongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Mkesha wa Pasaka, kuanzia saa 1: 30 kwa Saa za Ulaya. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican

JUMAPILI YA PASAKA YA BWANA: Tarehe 4 Aprili 2021, saa 4:00 Asubuhi majira ya saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na baadaye atatoa baraka zake za kitume kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini “Urbi et Orbi”. Vatican News itaendelea kushirikiana nawe ili kukujuza yanayojiri katika maisha na utume wa Kanisa. Ukiwa na haraka zako, “tinga” kwenye mtandao wetu na ujitahidi pia kuwashirikisha jirani zako matendo makuu ya Mungu yanayoendelea kufunuliwa kwa watu wa nyakati hizi! Waamini wajitahidi kufuatilia vyema katekesi zinazotolewa katika kipindi hiki, ili ziwasaidie kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Ibada Juma Kuu
30 March 2021, 15:07