Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu amekazia kuhusu: Fumbo la Msalaba, Hekalu la Mwili wa Kristo Yesu na kama Kanisa: Hekima na nguvu ya Mungu inayopyaisha maisha ya waamini. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu amekazia kuhusu: Fumbo la Msalaba, Hekalu la Mwili wa Kristo Yesu na kama Kanisa: Hekima na nguvu ya Mungu inayopyaisha maisha ya waamini. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Fumbo la Msalaba!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amejikita zaidi katika: Fumbo la Msalaba ufunuo wa nguvu na hekima ya Mungu; Umuhimu wa waamini kusafisha nyoyo zao kwani ni maskani ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Yesu anawasamehe na kuwapatia waja wake fursa ya kushiriki nguvu na hekima yake. Yesu alizungumzia kuhusu Hekalu la Mwili wake na Hekalu kama Kanisa: Nguvu na Hekima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 7 Machi 2021, mara baada ya chakula cha mchana na mapumziko kwenye Seminari ya Mtakatifu Petro huko Erbil, iliyojengwa kunako mwaka 1859, alikwenda kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Uwanja wa Michezo wa “Franso Hariri” huko Erbil, uliojengwa kunako mwaka 1956. Ulifanyiwa ukarabati mkubwa kunako mwaka 1992, leo hii una uwezo wa kuchukua watu 28, 000 kwa wakati mmoja. Huu ni uwanja wa michezo wa pili kwa ukubwa nchini Iraq. Ibada ya Misa Takatifu ni ile ya Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka B wa Kanisa. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amejikita kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba ufunuo wa nguvu na hekima ya Mungu; Umuhimu wa waamini kusafisha nyoyo zao kwani ni maskani ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Yesu anawasamehe na kuwapatia waja wake fursa ya kushiriki nguvu na hekima yake. Yesu alizungumzia kuhusu Hekalu la Mwili wake na Hekalu kama Kanisa.

Kristo Yesu alifunua nguvu na hekima yake kwa njia ya msamaha na huruma; kwa kuteswa, kufa na kufufuka kwa wafu. Kwa njia hii akaonesha uaminifu wake kwa upendo wa Mungu na Agano lake la Kale lililomwezesha kuwatoa Waisraeli utumwani na kuwaongoza katika uhuru wa watoto wa Mungu. Waamini wanahitaji nguvu na hekima ya Mungu iliyofunuliwa juu la Msalaba. Na kwa njia ya mateso na Madonda yake Matakatifu, binadamu akapata msamaha wa dhambi. Hata leo hii nchini Iraq kuna watu wanaoendelea kubeba madonda ya vita, ghasia na mashambulizi ya kigaidi. Haya ni madonda yanayoweza kuonekana, lakini pia kuna madonda ya ndani! Tabia ya mwanadamu ni kutaka kutenda mintarafu nguvu na hekima ya kibinadamu, lakini Kristo Yesu, anapenda kuwaonesha waja wake dira na mwongozo wanaopaswa kuufuata. Kristo Yesu alipoingia Hekaluni akawatoa wote Hekaluni, akamwaga fedha na kupindua meza kwa sababu walikuwa wamegeuza Hekalu la Baba yake wa mbinguni kuwa ni nyumba ya biashara. Kristo Yesu anataka nyoyo za wafuasi wake zitakaswe na kuondoa uchafu wa dhambi, unafiki na maisha ya kuwa ndumila kuwili.

Haya ni magonjwa hatari kwa nyoyo za waamini kwani yanawafanya kutokuwa wakweli. Waamini wanapaswa kutakaswa kutokana na magonjwa ya uhakika wa usalama unaowapotosha; uchu wa mali na madaraka; magonjwa ambayo yanapaswa pia kuondolewa ndani ya Kanisa. Waamini watambue kwamba, wanawajibika kutokana na mateso na mahangaiko ya ndugu zao na hivyo kuwa na ujasiri wa kumkaribisha Kristo Yesu ili aweze kuwasaidia kusafisha na kujenga tena mahekalu ya nyoyo zao. Ana nguvu ya kuvunjilia mbali utawala wa Shetani, Ibilisi kwa sababu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani kwa sababu Mwenyezi Mungu hafurahii kifo cha mdhambi, bali atubu na kumwongokea Mungu, ili aweze kumwilisha upendo, udugu na huduma ya huruma.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Kristo Yesu anasafisha dhambi na kusamehe dhambi zao na kuwakarimia imani yenye upeo mkubwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni imani inayowaunganisha na kamwe si kichokoo kinachowatenganisha. Ni imani inayowasaidia kujenga na kudumisha Kanisa. Kwa njia ya imani wakristo wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama Mitume wamisionari. Kumbe, wanahimizwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa nguvu ya Mungu inayoleta mageuzi katika maisha ya watu. Kristo Mfufuka anawawezesha waja wake kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na amani; uvumilivu na ujasiri sanjari na wajenzi wa mfumo mpya wa kijamii. Ni kwa njia hii, waamini wanaweza kuona ufunuo wa huruma ya Mungu kwa sababu “upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu”. Jumuiya za Wakristo katika hali yao ya kawaida pasi na makuu ni alama za ujio wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika upendo.

Kristo Yesu anazungumzia pia Hekalu la Mwili wake na Hekalu kama Kanisa. Kwa nguvu ya ufufuko kwa wafu, anaweza kuwakirimia waja wake ngugu ya kuweza kusimama tena kutoka katika ukosefu wa haki, kinzani, migawanyiko, chuki na uhasama. Hii ndiyo ahadi katika mchakato wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kwa jicho la imani, waamini wanamtambua Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na kwamba, Kristo Mfufuka anaendelea kuishi kati pamoja nao! Hekima ya Kristo Yesu iwawezeshe waamini kupata faraja na mapumziko katika Madonda yake Matakatifu; wapate uponyaji na nguvu kuhudumia katika Ufalme wa Mungu hapa duniani. Ni kwa njia ya Madonda yake Matakatifu, waamini wamepata kupona. Huu ni mwaliko kwa waamini kuchota nguvu kutoka katika upendo wenye huruma, ili kufariji, kuganga na kuponya kumbukumbu yenye machungu na mateso makali, ili kuanza kujielekeza zaidi katika amani na udugu wa kibinadamu nchini Iraq.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa nchini Iraq kwa neema ya Mungu linaendelea kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya hekima ya Mungu inayofumbatwa juu ya Msalaba, kwa kuendeleza huruma na msamaha, hasa kwa wahitaji zaidi. Hata katika umaskini, magumu na mahangaiko ya maisha, waamini wengi wameonesha moyo wa ukarimu na mshikamano kwa wahitaji zaidi. Ushuhuda huu anasema Baba Mtakatifu ni kati ya mambo mazito yaliyomsukuma kutembelea Iraq, ili kuwaimarisha katika imani na ushuhuda wa maisha. Leo hii, watu wanaweza kushuhudia kwamba, Kanisa la Mungu nchini Iraq ni hai, Kristo Yesu anaishi kati ya waamini na watakatifu wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka watu wa Mungu nchini Iraq chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyeungana na Mwanaye mpendwa katika njia ya Msalaba na mateso hadi akabahatika kushiriki furaha ya Fumbo la ufufuko. Bikira Maria awe mwombezi wao na awasindikize kwa Kristo Yesu nguvu na hekima ya Mungu.

Papa Misa Franso Hariri
07 March 2021, 17:54