Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu kuanzia tarehe 21 Februari hadi tarehe 26 Februari 2021 "Watapanda kwenda Mlimani" ili kujiandaa kwa ajili ya Sherehe ya Pasaka na utume wao kwa ujumla. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu kuanzia tarehe 21 Februari hadi tarehe 26 Februari 2021 "Watapanda kwenda Mlimani" ili kujiandaa kwa ajili ya Sherehe ya Pasaka na utume wao kwa ujumla. 

Papa Francisko na Wasaidizi Wake Kuwa na Mafungo 21-26 Feb. 2021

Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali wanaoishi mjini Roma, pamoja na Viongozi Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia Jumapili jioni tarehe 21 hadi Ijumaa tarehe 26 Februari 2021, wanasitisha shughuli zote za kitume na kwenda “kujichimbia Mlimani”, lakini kwa wakati huu, kila mtu kivyake vyake kutokana na janga la Virusi vya Korana, UVIKO-19. Ni sehemu ya Maandalizi ya Pasaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafungo ya maisha ya kiroho yawasaidie waamini kukuza na kudumisha: Moyo wa Sala, Ibada na Majitoleo kwa Mwenyezi Mungu pamoja na Kanisa lake. Ni wakati wa kufanta tafakari ya kina ya Neno la Mungu, tayari kulimwilisha katika uhalisia wa maisha na wito wa kila mmoja wao. Ni wajibu wa waamini kutambua uwepo wa Mungu katika kazi ya uumbaji, bila ya kumwogopa. Itakumbukwa kwamba, wakati fulani katika maisha yao, Mitume walishikwa na woga, kwa sababu hawakuwa na imani thabiti kiasi cha kumwomba Kristo Yesu awaongezee imani. Hali hii inaweza kumkuta mwamini ikiwa kama hawezi kuzamisha mahusiano na mafungamano yake ya dhati na Yesu Kristo na kusahau kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na msamaha kwa wale wote wanaomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi Cha Kwaresima kwa Mwaka 2021 unanogeshwa na kauli mbiu: “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu:” Mt. 20:18: Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo”. Baba Mtakatifu anakazia: Imani inayowaalika waamini kukubali ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na jirani zao. Matumaini ni sawa kama na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao. Upendo, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali wanaoishi mjini Roma, pamoja na Viongozi Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia Jumapili jioni tarehe 21 hadi Ijumaa tarehe 26 Februari 2021, watasitisha shughuli zote za kitume na kwenda “kujichimbia Mlimani”, lakini kwa wakati huu, kila mtu kivyake vyake kutokana na janga la Virusi vya Korana, UVIKO-19. Katika kipindi hiki chote, Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Februari 2021 imeahirishwa. Huu ni muda muafaka wa kusali na kutafakari, tayari kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Ni muda wa kwenda jangwani ili kujichotea nguvu za maisha ya kiroho, tayari kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuliandama Kanisa na jamii katika ujumla wake! Kwa Baba Mtakatifu Francisko huu ni muda wa kujiandaa na hija yake ya Kitume nchini Iraq kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021. Hija hii ya kitume inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Lengo kuu ni kuendelea kujizatiti katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kisiasa na kitamaduni.

“Jangwa” au "Upweke mtakatifu" ni muhimu sana katika maisha na utume wa waamini ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.  Ni baada ya Yesu kubatizwa na Roho kutua kama njiwa juu yake. Roho huyo huyo aliyetua juu ya Yesu, katika somo la leo, anamtoa Yesu na kumpeleka jangwani. Huko anakaa siku 40 akijaribiwa na Shetani, Ibilisi. Hizi ni alama zenye maana kubwa sana katika utume wa Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwa kuzingatia historia ya Waisraeli waliosafiri jangwani kwa miaka 40 kuelekea nchi ya ahadi, jangwa lilikuwa ni mahala pa kujaribiwa uamifu, mahala pa kutakaswa na mahala pia pa kuonja wema, upendo na huruma ya Mungu. Wakiwa jangwani Mungu aliwaonesha upendo wake mkuu kwa kuwalinda, kuwaongoza na kuwapatia chakula.

Mafungo
20 February 2021, 16:03