Baba Mtakatifu Francisko: Ujumbe katika kongamano IV la Kimataifa kuhusu Muziki Mtakatifu: Umuhimu wa muziki mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa! Baba Mtakatifu Francisko: Ujumbe katika kongamano IV la Kimataifa kuhusu Muziki Mtakatifu: Umuhimu wa muziki mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa! 

Papa Francisko: Umuhimu wa Muziki Mtakatifu Katika Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa Kongamano la IV la Kimataifa Kuhusu Muziki Mtakatifu anakazia umuhimu wa Muziki mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, athari za Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19), pamoja na mifumo mbali mbali ya muziki. Tema zilizochaguliwa ni muhimu katika Liturujia ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Muziki Mtakatifu ni chombo cha ibada na uinjilishaji; ni amana na utajiri wa Kanisa; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ibada, uchaji, unyenyekevu na unyoofu wa moyo! Hii inatokana na ukweli kwamba, nyimbo na muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa zinawasaidia waamini kuzamisha Neno la Mungu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Muziki ni chombo cha imani, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Muziki mtakatifu unasaidia sana maboresho na ushiriki wa waamini katika Liturujia na maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa, changamoto kwa wanakwaya ni kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha waamini wengine furaha ya Injili kwa njia ya muziki mtakatifu. Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayowakirimia waamini matumaini ya kuimba huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, hadi pale atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Kardinali Gianfranco Ravasi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema kwamba kwa muda wa siku mbili, yaani kuanzia tarehe 4 hadi 5 Februari 2021, Baraza lake linaadhimisha Kongamano la IV la Kimataifa Kuhusu Muziki Mtakatifu, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Kanisa na Muziki mtakatifu, Muktadha na Maneno Yanayotumika”. Hili ni kongamano linalojielekeza zaidi katika mchakato wa sanaa ya kufasiri, kuchambua tafsiri kwa kuzingatia muktadha na lugha fasaha. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa Kongamano la IV la Kimataifa Kuhusu Muziki Mtakatifu anakazia umuhimu wa Muziki mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, athari za Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19), pamoja na mifumo mbalimbali ya Muziki mtakatifu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza washiriki wote wa Kongamano hili na kwamba, tema zilizochaguliwa ni muhimu sana katika Liturujia ya Kanisa na katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto!

Nabii Isaya katika utenzi wake wa shukrani anasema “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, na sifa zake tokea mwisho wa dunia;” Isa. 42:10. Maandiko Matakatifu yamekuwa yakitumiwa na watunzi wengi wa Muziki mtakatifu sehemu mbalimbali za dunia. Jumuiya mbalimbali za Kikristo zimefanikiwa kutafsiri vifungu vya Biblia kwa kutumia Muziki sanjari na kuzingatia Mapokeo ya Kanisa. Muziki mtakatifu unaendelea kuenea zaidi na zaidi si tu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, bali hata katika matamasha, katekesi, shuleni na vyuoni bila kusahau kumbi za burudani, kwani hata huko Muziki mtakatifu unaendelea kubisha hodi! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, tangu kuibuka na kuenea kwa Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19), tasnia ya Muziki katika ujumla wake, imeguswa na kutikiswa sana. Wanamuziki wamelazimika kufuata itifaki dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Korona, UVIKO-19 (COVID-19).

Wanamuziki wengi wamepoteza fursa za ajira kwa kushindwa kukutana na mashabiki wao. Imekuwa pia ni vigumu kwa wanamuziki kupata majiundo endelevu, elimu pamoja na kushiriki maisha ya kijumuiya. Licha ya changamoto zote hizi, bado wanamuziki wengi wameendelea kutoa mchango na huduma yao kwa kutumia kipaji cha ubunifu. Hiki ni kipaji muhimu sana si tu kwa ajili ya Muziki mtakatifu bali ni muhimu hata katika mtandao mzima ambao unatumia muziki kama huduma kwa jamii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maisha ya kijamii yataendelea kupyaishwa na hivyo kuwawezesha wadau wa muziki kukaa tena pamoja na kufurahia huduma hii. Wahenga wanasema, “mahali penye muziki, hapo hakuna ubaya”. Kwa njia ya muziki, watu wengi wanaendelea kujibidiisha katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu ulimwenguni! Muziki unawaunganisha watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Nabii Isaya katika utenzi wake wa shukrani anaendelea kusema: “Siku nyingi nimenyama kimya, nimenyamaza nikajizuia”. Isa. 42:14.

Mwanamuziki mahiri anatambua na kuthamini umuhimu wa ukimya, ili kumwezesha msikilizaji wake, kuzamisha ujumbe unaokusudiwa ili kuendeleza mchakato wa majadiliano, ili kusikilizana. Hii ni changamoto pevu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, waamini wanahamasishwa kusikiliza Neno la Mungu, ambalo linakuwa ni kiini cha Liturujia na katika muktadha huu, waamini wanakuwa ni walengwa wakuu. Neno la Mungu ni chemchemi na mwanga unaoiongoza jumuiya ya waamini. Kanisa linatambua na kuthamini Simulizi mbalimbali za historia ya wokovu. Muziki Mtakatifu unaweza kulisaidia Neno la Mungu kuzungumza katika mazingira na tamaduni mbali mbali, ili kuzifikia akili na nyoyo za watu wengi zaidi.

Baba Mtakatifu anawahimiza watunzi wa Muziki mtakatifu kuhakikisha kwamba wanazingatia mifumo mbalimbali ya muziki, kama kielelezo cha amana na utajiri unaobubujika kutoka katika tamaduni mbali mbali duniani. Lakini jambo la msingi ni kuzingatia kanuni maadili na utu wema. Watu mahalia wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Muziki mtakatifu usaidie mchakato wa huduma ya uinjilishaji. Ikumbukwe kwamba, muziki pia unagusa mwili wa binadamu. Kumbe, kuimba vyema, kuwasaidie waamini kuishi vizuri zaidi. Mwishoni, Baba Mtakatifu anakazia umoja na mshikamano wa nyoyo na sauti za waimbaji pamoja na vyombo vya muziki visaidie kujenga umoja na udugu wa kibinadamu.

Papa Muziki Mtakatifu
04 February 2021, 15:46