Jumuiya ya Kimataifa kwa mara ya kwanza tarehe 4 Februari 2021 inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu inayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kitume: Fratelli tutti: Yaani wote ni ndugu! Jumuiya ya Kimataifa kwa mara ya kwanza tarehe 4 Februari 2021 inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu inayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kitume: Fratelli tutti: Yaani wote ni ndugu! 

Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu 4 Februari 2021

Ni katika amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba, kuanzia sasa, tarehe 4 Februari itakuwa ni Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Hizi ni juhudi za ushirikiano wa dhati wa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anakazia umuhimu wa ujenzi wa ushirikiano na mafungamano yanayokita mizizi yake katika mshikamano na maendeleo katika masuala ya: kiuchumi kwa kuzingatia majadiliano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa yaani amani. Kwa sababu vita inasababisha maafa kwa watu na mali zao; vita ina sababisha vifo, inaharibu mazingira pamoja na kufisha matumaini ya watu. Majadiliano katika ukweli na uwazi yanavunjilia mbali kuta za utengano: kiroho na kiakili; yanafungua nafasi ya msamaha na kukoleza upatanisho. Majadiliano ni chombo cha haki kinachochochea na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kukazia amani. Majadiliano yanafumbata uvumilivu, yanajielekeza katika mchakato wa ushuhuda kama chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, upendo na mafao ya wengi. Malengo ya Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anakazia utawala bora kama sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Utawala bora unaozingatia: sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa na wengi. Kumbe, utawala bora unapaswa kuakisi matakwa ya jamii na wala si hisia za mtu binafsi.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inasimama kidete kupambana na hatimaye, kung’oa baa la njaa, umaskini, magonjwa pamoja na kusimamia utekelezaji wa haki msingi za binadamu! Ujenzi wa utamaduni wa udugu wa kibinadamu uisaidie Jumuiya ya Kimataifa kupambana na changamoto mamboleo, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na Maskini katika ujumla wao. Hii ni changamoto ya kuwafunda raia ili waweze kuwa watu wema, mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki na amani ya kudumu. Hapa kila mtu anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake. Mahusiano na mafungamano ya kimataifa yanaweza pia kuangaliwa kwa njia ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanayozingatia haki msingi za binadamu pamoja na diplomasia ya kimataifa. Amani inafungamana na wajenzi wa amani duniani; haki msingi za binadamu zinatekelezwa kwa kuangalia mahitaji msingi ya watu kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, mfano bora wa kuigwa. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yake katika msingi wa utu na udugu wa kibinadamu.

Baba Mtakatifu anapenda kuunganisha athari za uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kijamii; vita na kinzani; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi pamoja na baa la umaskini linalopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaunda mfumo wa uchumi na masuala ya kijamii yanayokita misingi yake katika haki, heshima na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unatoa dira na mwongozo wa kuweza kufikia malengo haya kwa watu kutambuana kwamba, wao ni ndugu wamoja na wanahamasishwa kutegemezana na kusaidiana, kwani wote wako ndani ya mashua moja!

Hili limejidhihirisha wazi zaidi katika janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Vurusi vya Corona, COVID-19. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kutojikatia tamaa na hatimaye, kutumbukia katika kishawishi cha “Mwanadamu kugeuka kuwa Mbwa mwitu” “homo homini lupus” kwa kujenga kuta za utengano na badala yake, wamtazame Msamaria mwema, ili kumwilisha Injili ya upendo inayomwondoa mwanadamu kutoka katika miundombinu iliyopitwa na wakati. Huu ni mwaliko kwa binadamu kutambuana kuwa wao ni ndugu wamoja na kwa namna ya pekee kwa waamini, ni kujitahidi kumwona Kristo Yesu kati ya watu wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013.

Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Ni katika amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limetangaza kwamba, kuanzia sasa, tarehe 4 Februari 2021 itakuwa ni Siku ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu. Hizi ni juhudi zilizotekelezwa kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu: Wajumbe wa Kamati hii ni pamoja na Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Aliyekuwa Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu.

Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu. Kwa upande wao, viongozi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Amiri Jeshi Msaidizi, watahakikisha kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inatekelezwa kwa dhati kabisa na Kamati iliyoundwa, ili kumwilisha malengo yaliyobainishwa kwenye Hati hii. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linapenda kutumia fursa hii, kuitia shime Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu, mintarafu malengo yaliyobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Hati hiyo. Umoja wa Mataifa unazihamasisha Nchi wanachama, Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na Vyama vya kiraia kuhakikisha kwamba, vyote vinasaidia kunogesha Siku ya Kwanza ya Kimataifa ya Udugu wa Kibinadamu, yaani tarehe 4 Februari 2021.

Siku ya Udugu wa Kibinadamu
30 January 2021, 15:54